Wednesday, September 2, 2015

MAASKOFU, WACHUNGAJI KUBARIKI TAMASHA LA AMANI

kushoto Mwenyekiti wa kamati ya tamasha la kuombea Amani hapa nchini,Alex Msama .

Na Mwandishi Wetu
MAASKOFU wa madhehebu mbalimbali na Wachungaji wanatarajiwa kushiriki kwenye Tamasha la Amani linalotarajiwa kufanyika Oktoba 4, mwaka huu Dar es Salaam.

Tamasha la Amani ambalo litahusisha waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili ni maalum kwa ajili ya kuombea amani katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ilieleza kuwa maandalizi muhimu yanaenda vizuri.

“Niseme kwamba Maaskofu na Wachungaji mbalimbali wamekubali kujumuika nasi siku hiyo katika tukio muhimu, ambapo baada ya tamasha la Dar es Salaam tutaelekea pia mikoani,” alisema Msama.

Alisema wasanii mbalimbali wanaendelea kuomba kushiriki katika tamasha hilo alilosema litakuwa la aina yake.

 “Tunaandelea na mazungumzo na wasanii mbalimbali, ambapo tayari Rose Muhando ameshakubali kutumbuiza na wengine tuliowatangaza,” alisema Msama.

Baadhi ya wasanii maarufu ambao wamewahi kushiriki matamasha yanayoandaliwa na Msama ni Rose Muhando, Rebecca Malope, Christina Shusho, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa, Atosha Kissava, Ephraim Sekeleti na kundi la Glorious Celebration.

Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival, Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sohly Mahlangu.

No comments:

Post a Comment