Wednesday, September 2, 2015

AFRIKA KUZINGATIA VIPAUMBELE VYAKE WAKATI WA UTEKELEZAJI WA MALENGO MAPYA YA MAENDELEO

 Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akizungumza siku ya Jumanne, wakati  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha Azimio linalowasilisha kwa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali  Malengo na Ajenda mpya za Maendeleo Endelevu ( Ajenda 2030)   Anaonekana pia Rais wa Baraza Kuu la 69, Bw. Sam Kutessa .
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  akiwa na Afisa Mkuu Siongelael Shilla wakati wa upitishaji wa Azimio  namba A/69/L.85   kuhusu Ajenda 2030  ambapo baada ya kupitishwa  kwa kauli moja azimio hilo wazungumzaji  wanaowakilisha  makundi ya kikanda walipata fursa ya kuelezea misimamo yao juu ya  baadhi ya   mambo ambayo walikuwa wakitofautiana kimtizamo na kimsimamo.

Na Mwandishi Maalum,   New York
AFRIKA,  imesisitiza  na kubainisha kwamba  itatekeleza malengo mapya ya maendeleo endelevu kwa  kuzingatia  maslahi, vipaumbele, sera,   mila na tamaduni ambazo nchi za Afrika  zimejiwekea.

Aidha  Afrika inasema kuwa,  utekelezaji wa  malengo hayo    pia utazingatia  sheria za kimataifa  na ambazo nchi  za Afrika  zimeridhia na si vinginevyo.

 Hayo yameelezwa na  Balozi Fode Seek,  Mwakilishi wa Kudumu  wa Senegal katika Umoja wa Mataifa ambaye ni  Mwenyekiti wa    nchi za Afrika   kwa mwezi Septemba.

  Alikuwa  akizungumza  kwa  niaba ya  nchi   za Afrika wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokutana  siku ya jumanne, kupitisha Azimio namba A/69/L.85  ambalo linawasilisha  ajenda ya  Maendeleo Endelevu (ajenda 2030) itakayotekelezwa kwa miaka   15 ijayo.
Ajenda 2030 inachukua nafasi ya   Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) yanayofikia ukingoni  mwishoni mwa  mwaka huu.

Kupitishwa kwa  azimio hilo  la ajenda 2030, inayojumuisgha  malengo 17 na ambalo sasa litawasilishwa  baadaye mwezi huu wa Septemba   kwa Viongozi Wakuu wa  Nchi na Serikali tayari kwa kuridhiwa na  kuanza utekelezaji wake mwakani, kunakamilisha mchakato  uliodumu kwa  zaidi ya miaka miwili ya majadiliano yaliyozaa malengo mapya na ajenda mpya.
“Afrika  itashirikiana na  wadau wa maendeleo katika utekelezaji wa malengo haya  yanayolenga  katika kuondoa umaskini, kuboresha huduma za jamii,  upatikanaji wa fursa za maendeleo na ajira  na bila ya  kumwacha yoyote nyuma. Lakini  tutatekeleza kwa kuzingatia  mipango yetu, vipaumbele vyetu, sera  zetu na kwa  maslahi ambayo  ambayo kila  nchi itaona inafaa  kutoka na mazingira na uwezo wa nchi  yenyewe” akasema Balozi. Seek

Baadhi ya mambo ambayo Afrika inasema  kimsingi haikubaliani katika ujumla wake na ambayo kwayo utekelezaji wake utazingatia utashi wa kila nchi,   kuzingatia Imani za kidini,  mila na tamaduni na  sheria  za nchi husika ni pamoja na  tafsri sahihi ya neno familia ambalo  Afrika na baadhi ya  nchi nyingine  inasema  familia ni  Baba, Mama na  watoto na si  tafsili ile inayopigiwa chapuo na baadhi ya nchi za  magharibi.

Jambo  jingine ambalo   Afrika na   Nchi nyingine   imetoa msimamo ,   linahusu tafsiri ya  jinsia ambayo kwa Afrika inaamini kwamba jinsia ni ya kike na kiume.

  Utolewaji   na upatikanaji wa   huduma za afya, elimu na mafunzo yanayoambatana na eneo hilo  na  hususani uzazi wa mpango, ni eneo jingine ambalo Afrika na mataifa mengine yanayoendelea  yanasisitizia kuwa utekelezaji wake usiwe wa shurutisho na ufanyike kwa kuzingatia mila na desturi za nchi husika.

Mbali ya  msemaji huyo kwa niaba ya nchi za Afrika kuanisha baadhi ya maeneo ambayo  Afrika itayatekeleza  pasipo kushurutishwa.  Wazungumzaji   zaidi ya 30 wakiwakilisha  makundi ya  kikanda  na baadhi wakizungumza kwa niaba  ya nchi zao walichangia maoni yao   kuhusu ajenda 2030.

Mwakilishi wa  Kudumu wa Afrika ya Kusini  Balozi Kingsley Mamabolo ambaye ni   Mwenyekiti wa  Kundi la G77& China. Akizungumza kwa niaba ya kundi hilo anasema.  

  Haikuwa kazi nyepesi   kufikia makubaliano    yaliyopelekea kupitishwa kwa kauli moja  Malengo   na Ajenda  2030
“   Ajenda hii  ambayo tumeipitisha kwa kauli moja,  hatuwezi kusema kwamba haina mapungufu.  lakini tumefika hapa tulipo baada ya  majadilliano marefu na magumu na kukubaliana kuto kukubaliana”.

  Na   akaongeza  Ajenda 2030 ina mambo mengi yakiwamo malengo    17  na viashiria  169. Lakini jambo   moja la msingi na muhimu  ni kwamba, utekelezaji wake  utategemea  kila nchi inavyopanga vipaumbele vyake na sera zake” akasema Balozi Mamabolo.

Awali akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa Azimio hilo, Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban   Ki   Moon,   amesema. Agenda 2030   ni makubaliano ambayo kila   nchi inapashwa kujivunia na kwamba utekelezaji wake utahitaji ushirikiano wa karibu baina ya wadau mbalimbali.
Akasema   Agenda   2030 itapitishwa na Viongozi Wakuu wa   Nchi na Serikali kutoka  Mataifa mbalimbali duniani akiwamo Baba Mtakatifu Francis.


No comments:

Post a Comment