Saturday, September 26, 2015

TAASISI, MASHIRIKA NA MAKAMPUNI YAASWA KUTUMIA SEHEMU YA FAIDA WANAYOPATA KUSAIDIA HUDUMA ZA AFYA.

  Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam(CBE) Prof.Emanuel Mjema(kushoto) akizungumza na viongozi  na baadhi ya watumishi wa Hospitali ya wilaya ya Kisarawe leo  kabla ya kukabidhi msaada wa  shuka 176 kusaidia wodi ya Wazazi ya hospitali hiyo.
 Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Dkt.Martin Msokela akiongea na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Kisarawe kabla ya kupokea msaada wa mashuka ya wagonjwa wilayani humo leo. Mashuka hayo yametolewa na chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE). 
 Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam(CBE) Prof.Emanuel Mjema(kushoto) akikabidhi msaada wa shuka 176 kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Dkt.Martin Msokela (kulia) leo. Mashuka hayo yametolewa na chuo hicho kusaidia wodi ya Wazazi ya Hospitali hiyo iliyokuwa ikikabiliwa na uhaba wa mashuka.
 Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam(CBE) Prof.Emanuel Mjema(katikati), Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya  wilaya ya Kisarawe  Dkt.Martin Msokelo(kulia) na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Mohamed Mzige kwa pamoja wakitandika sehemu ya msaada wa mashuka 176 yaliyotolewa na CBE kwenye  wodi ya Wazazi ya hospitali hiyo.
 Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam(CBE) Prof.Emanuel Mjema(wa pili kushoto), Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya  wilaya ya Kisarawe  Dkt.Martin Msokelo(kushoto ) na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Mohamed Mzige (kulia) na baadhi ya watumishi wa hospitali ya Kisarawe wakielekea lilipo jengo la wodi ya wazazi.
Wauguzi wa Hospitali ya wilaya ya Kisarawe wakifurahia msaada wa mashuka yaliyotolewa kwa wagonjwa na Chuo cha Elimu ya Biashara, CBE leo.

Picha/Aron Msigwa - MAELEZO.




TAASISI, MASHIRIKA NA MAKAMPUNI YAASWA KUTUMIA SEHEMU YA FAIDA WANAYOPATA  KUSAIDIA HUDUMA ZA AFYA.

Aron Msigwa -MAELEZO.
26/9/2015. Kisarawe,PWANI.

Wito umetolewa kwa Taasisi, mashirika na makampuni kote nchini kujenga utamaduni  wa kutumia sehemu ya faida wanayoipata katika kuisaidia jamii kupitia sekta ya afya ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Wito huo umetolewa leo mjini Kisarawe na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof.Emanueli Mjema wakati akikabidhi msaada wa shuka 176 zilizotolewa na chuo hicho kusaidia wodi ya Wazazi ya Hospitali ya wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani.

Amesema CBE mwaka huu imetimiza miaka 50 toka kuanzishwa kwake mwaka 1965, hivyo ukongwe na umri wake nchini Tanzania umekua ukiendana na mabadiliko ya kiuchumi  yanayotokea ndani na nje ya nchi ili kukidhi mahitaji na matarajio ya watanzania.

"CBE tukiwa chuo kikongwe nchini tumefanya mengi yenye manufaa kwa uchumi wa nchi yetu na jamii ya watanzania,kwa kuwathamini wananchi tunaowahudumia tuna utaratibu wa kurudisha sehemu ya faida tunayoipata kwa jamii na mwaka huu tulitenga kiasi cha shilingi milioni 9 kusaidia wodi za wazazi katika hospitali zetu" Amesisitiza.

Ameeleza kuwa ndani ya miaka 50, CBE  imewanufaisha wananchi na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kupitia Fani za Biashara, Ugavi na manunuzi, Vipimo, TEHAMA , Utawala katika biashara pamoja na kutoa huduma mbalimbali kwa jamii.

Amesisitiza  kuelekea miaka 50 ijayo chuo chake kimeelekeza nguvu katika kuwekeza kwenye ubora na ujuzi wa kumuwezesha muhitimu kuitumia elimu aliyoipata kuleta manufaa na mabadiliko katika jamii inayomzunguka.

“Sisi kama chuo cha Elimu ya Biashara tumeona uhitaji uliopo nchini wa kukosa wataalam wenye ujuzi wa Biashara ndio maana tumeanza kufuandisha wanafunzi wa Shahada ya Elimu katika Biashara ili tupate wahitimu bora watakaokidhi mahitaji ya soko” Amesisitiza.

Kwa upande,Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Martin Msokela akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa wilaya hiyo, ameushukuru uongozi wa CBE kwa kuwakumbuka wagonjwa wa Hospitali ya wilaya ya Kisarawe.

Amesema msaada uliotolewa na chuo hicho umepunguza uhitaji wa mashuka waliokuwa nao kwani Hospitali hiyo inakabiliwa na tatizo la uhaba wa mashuka kwenye vitanda vya wagonjwa.

Dkt.Msokela amewaomba wadau wengine kujitokeza kwa wingi kuisaidia hositali hiyo kama  walivyofanya CBE ili kuboresha afya za wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kutibiwa.

" Nawaomba wadau wengine wajitokeze kusaidia kama walivyofanya CBE, licha ya hili la mashuka ukiangalia Jiografia ya Kisarawe,Hospitali yetu imekua na tatizo la upatikanaji wa maji  na uchakavu wa mitambo" Amebainisha. 

Aidha katika hatua nyingine Dkt.Msekela ameeleza kuwa hali ya ugonjwa wa Kipindupindu wilayani humo inaendelea kudhibitiwa  kupitia timu ya wataalam iliyoundwa kukabiliana na tatizo hilo na kuongeza kuwa hospitali hiyo    imepokea mgonjwa mmoja  mwenye tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment