Monday, August 31, 2015

WATANZANIA WAHIMIZWA KUTUMIA HUDUMA ZA BIMA.

Kamishna wa Bima nchini Bw. Israel Kamuzora.

Jovina Bujulu-MAELEZO
WATANZANIA theluthi mbili hawana ufahamu wa kutosha kuhusu namna Bima inavyofanya kazi nchini hasa Bima ya Maisha na Mali.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Bima nchini Bw. Israel Kamuzora alipokuwa akifunga mafunzo ya wiki ya huduma kifedha na uwekezaji mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam.

Kamuzora aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kueneza ujuzi na ufahamu waliopata ili wananchi walio wengi waweze kunufaika na huduma za bima nchini.

“Ninawaomba muwe mabalozi wazuri wa kueneza ufahamu juu ya faida za Bima kwa ndugu, jamaa na marafiki ambayo ni mojawapo ya mbinu za kujilinda kimaisha na kujikwamua katika umasikini”. Alisema Kamuzora.

Kamuzora alisema kuwa kwa upande wao kama waratibu wa huduma za Bima nchini wanao wajibu wa kuendelea kujenga mazingira ambayo ni rafiki na wezeshi kwa watoa huduma  ya Bima ili waendelee kuwa wabunifu katika kufikisha huduma hiyo kwa Watanzania wenye uwezo mkubwa na mdogo.

Aidha, Bw. Kamuzora alisema kuwa mpango wa Taifa wa huduma Jumuishi za kifedha nchini unalenga kuwafikia watu wazima asilimia 50 wanaotumia huduma rasmi za kifedha ifikapo mwaka 2016.

Ili kufanikisha mpango huo, Bw. Kamuzora alitoa wito kwa taasisi za kifedha na za utafiti wa sayansi kuendelea kushirikiana na mamlaka ya Bima kuona namna ya kuendeleaza matumizi ya simu za mkononi kwa ajili ya kuwapatia wananchi fursa ya kupata huduma za Bima ili kulinda mali na maisha ya Watanzania waliowengi.

Hadi sasa nchini, takwimu zinaonyesha kuwa karibu asilimia 90 ya wenye simu za mkononi nchini wanatumia huduma za fedha za simu ziliongeza ndugu Kamuzora.

Mafunzo ya wiki ya huduma za kifedha na uwekezaji yalipambwa kwa kauli mbiu inayosema “Maisha ni Duni Bila Bima” yaliwahusisha wajariamali, benki, na kampuni za Bima yalidhaminiwa na kampuni ya NUEBRAND na Shirika la PESCODE.

No comments:

Post a Comment