Friday, August 28, 2015

RAIS KIKWETE ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA FAMILIA ZA WALIOPATWA NA AJALI YA MOTO

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Said Meck Sadik kufuatia vifo vya watu tisa wa familia moja ya Bwana Masoud Matal vilivyotokea alfajiri ya tarehe 27 Agosti, 2015 kwa ajali ya moto.

Wanafamilia hao wakiwemo watoto watano walipoteza maisha baada ya nyumba yao iliyoko katika Mtaa wa Gulam, eneo la Buguruni Malapa katika Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam kuungua na kuteketea kabisa kwa moto.  Baba wa familia, Bwana Masoud Matal alisalimika kwa vile hakuwamo katika nyumba hiyo wakati ikiungua.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na nimesikitishwa mno kutokana na taarifa za kupoteza maisha kwa watu tisa wa familia moja ya Bwana Masoud Matal baada ya nyumba yao kuunguzwa na kuteketezwa kabisa na moto alfajiri ya tarehe 27 Agosti, 2015”, amesema kwa huzuni Rais Kikwete akiomboleza vifo vya wanafamilia hao.

“Kwa hakika hili ni pigo kubwa kwa Bwana Masoud Matal, lakini namuomba awe mvumilivu kwa machungu yote ya kupotelewa ghafla na familia nzima, lakini  yote amwachie Mwenyezi Mungu muweza wa yote”, ameongeza kusema Rais Kikwete.

Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amemwomba Mheshimiwa Sadik kumfikishia Salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa Bwana Masoud Matal kutokana na msiba huo mkubwa uliompata, na amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za Marehemu wote, Amina.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
28 Agosti,2015


No comments:

Post a Comment