Saturday, August 1, 2015

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar akutana na ujumbe Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri Mhandisi Amri Alouba akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar michoro iliyotengenezwa na Wataalamu wa ECG ya jinsi linavyoweza kujengwa eneo la Darajani na kuwa katika mazingira ya Biashara ya Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wafanyabiashara pamoja na wataalamu wa ushauri wa Uhandisi kutoka Nchini Misri waliopo Tanzania kuangalia maeneo ambayo wanaweza kuwekeza miradi ya Kiuchumi.
Meneja wa Biashara wa Kampuni ya Kimataifa ya AIKAN ya Nchini Misri Bwana Mohammed Alef Sherief wa kwanza kutoka kushoto akimfahamisha Balozi Seif hayupo pichani fursa zinazotolewa na Taasisi yake katika kuwajengea Vijana uwezo wa kufanya Biashara.
Balozi Seif katika Picha ya pamoja na Wafanyabiashara na wataalamu wa ushauri wa Uhandisi kutoka Nchini Misri mara baada ya kufanya mazungumzo nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kushoto ya Balozi Seif ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri Mhandisi Amri Alouba na Balozi wa Tanzania Nchini Misri Balozi Mohammed Hamza. Kulia ya Balozi Seif ni Mtaalamu wa Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji ya ECG Mhandisi Sherif Meurad pamoja na Meneja wa Biashara wa Kampuni ya Kimataifa ya AIKAN ya Nchini Misri Bwana Mohammed Alef Sherief.
Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Ali akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kabla ya kufanya mazungumzo yao ya Ushirikiano wa kuimarisha uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu wa kidugu uliopo baina ya Oman na Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Ali Abdullah Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.

Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri imeamua kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika azma yake ya kusaidia Uchumi wa Zanzibar na ustawi wa Wananchi wake.

Kiongozi wa Ujumbe wa Wafanyabiashara wa Misri wanaotembelea Tanzania kuangalia maeneo wanayoweza kushirikiana na Serikali katika uwekezaji Mhandisi Amr Allouba alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Mhandisi Amri Allouba ambae pia ni Makamu  Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya  uhandisi ya { ECG } alisema Wataalamu wa Taasisi hizo wako tayari kuelekeza nguvu zao ndani ya ukanda wa Afrika ya Mashariki, Zanzibar ikiwa miongoni mwake kutokana na mazingira mazuri ya rasilmali pamoja na uwekezaji.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya Uhandisi ya ECG alisema Wataalamu wa Taasisi hiyo tayari wameshaandaa michoro ya jinsi linavyoweza kujengwa eneo la Darajani na kubadilishwa kuwa katika mazingira ya kisasa ya Biashara  ya Kimataifa.

Mhandisi Amr alifahamisha kwamba eneo hilo la Darajani upande wa iliyokuwa kituo cha Dala dala pamoja na Makontena linaweza kujengwa Vituo vya Biashara bila ya kuathiri mipango Miji iliyowekwa katika Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao umo katika urithi wa Kimataifa.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Ali Abdulla Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yao Balozi Seif kupitia Balozi Mdogo huyo wa Oman aliishukuru Serikali ya Nchi hiyo kwa jitihada inazochukuwa katika kusaidia harakati za Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar.

Mapema Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Ali Abdulla alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kuelekea kwenye maendeleo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/8/2015.

No comments:

Post a Comment