Saturday, August 29, 2015

MAFUNZO KUHUSU HUDUMA ZA LESENI ZA MADINI KWA NJIA YA MTANDAO YAANZA RASMI KANDA YA KUSINI

 Mtaalam kutoka  Kitengo cha Leseni, Wizara ya Nishati na Madini, Charles Gombe akielezea hatua za Wizara katika  kuboresha huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao (Online Mining Cadastre Transactional Portal; OMCTP) kwa wachimbaji wa madini (hawapo pichani) mjini Mtwara. Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwapa uelewa  wachimbaji wa madini kuhusu  huduma hiyo pamoja na kuwasajili.
 Baadhi ya wachimbaji wadogo  wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini (hawapo pichani).
 Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Aidan Mhando akifungua mafunzo  kuhusu huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao yaliyoshirikisha wachimbaji wa madini kutoka katika mkoa wa Mtwara.
 Mwenyekiti wa Chama cha  Wachimbaji wa Madini kutoka Mkoa wa Mtwara (MTWAREMA), Festo Balegele akifafanua jambo katika mafunzo hayo.
 Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Aidan Mhando ( wa pili kutoka kushoto, waliokaa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.
 Mtaalam kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mtwara, Juma Namuna akielezea umuhimu wa wachimbaji wa madini kujiunga na mfuko huo  ili kunufaika kwa kupata mikopo.
 Mtaalam kutoka  Kitengo cha Leseni, Wizara ya Nishati na Madini, Pendo Elisha akielezea faida za kujiunga na huduma ya leseni za madini kwa njia ya mtandao katika mafunzo hayo.
 Mchimbaji mdogo wa madini ya chumvi, Hussen Abdalah akichangia mada kwenye mafunzo hayo.
 Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Aidan Mhando ( wa nne kutoka kushoto, waliokaa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na  wataalam wa Wizara  ya Nishati na Madini na wachimbaji wa madini kutoka Lindi walioshiriki mafunzo ya huduma ya leseni  za madini kwa njia ya mtandao yaliyofanyika mjini Lindi.
Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Paul Mtulo akiweka mitambo sawa kwenye  gari la matangazo la Wizara kabla ya kuanza kwa kampeni ya kuhamasisha wachimbaji  wa madini kujiunga na huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao mjini Lindi.


Na Greyson Mwase, Mtwara
Ofisi ya Madini, Kanda ya Kusini yenye ofisi zake mjini Mtwara imeanza kutoa huduma za leseni  za utafutaji na  uchimbaji  wa madini  ndani ya  siku moja  tofauti na ilivyokuwa awali.

Hayo yalisemwa na Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Aidan Mhando  katika mafunzo  kuhusu  huduma za leseni za madini kwa njia  ya mtandao (Online Mining Cadastre Transactional Portal; OMCTP) yaliyoshirikisha wachimbaji wa madini mkoani Mtwara.

Mhando alisema kuwa awali maombi yalikuwa yakichukua muda mrefu kutokana na changamoto mbalimbali  ikiwemo ya  mtandao na kuongeza kuwa ofisi yake imeboresha mtandao na kuanza kutoa leseni ndani ya siku moja.

Alisema ofisi yake ina uwezo  wa kushughulikia ombi moja  la leseni ndani ya nusu saa iwapo mwombaji  atakuwa amekamilisha  vigezo vyote vinavyotakiwa.

Alieleza kuwa tangu huduma ya mtandao iboreshwe ofisi ya madini imekuwa na uwezo wa kushughulikia maombi  20 kwa siku  tofauti na awali ambapo ilikuwa inachukua muda mrefu.

Akielezea mikakati ya ofisi yake katika utekelezaji wa mfumo mpya wa utoaji wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao, Mhando alisema ofisi imejipanga kwa zoezi  la kuhakikisha kuwa wateja wake wote wanaingizwa katika mfumo huu na kunufaika na huduma hiyo.

Aliongeza kuwa ili kuwafikia wachimbaji wa madini ya chumvi ambao idadi yako kubwa ni wazee, ofisi yake imeweka utaratibu  wa kuwatembelea kwenye maeneo yao  ya kazi, kuwapa elimu  pamoja na kuwasajili kwenye mfumo huu.

Akielezea  faida za mfumo mpya wa huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao Mhando alisema kuwa mfumo utawawezesha wamiliki wa leseni za madini kupata taarifa za leseni zao   wakati wowote pamoja na kufanya malipo ya leseni zao kwa njia ya mtandao yaani M-Pesa, Airtel Money na Tigo Pesa.

“Mfumo huu utapunguza migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kati ya wachimbaji na kuondoa dhana ya kwamba kuna upendeleo kwenye  utoaji wa leseni za madini.” Alisema Mhando.

No comments:

Post a Comment