Tuesday, July 21, 2015

WATUMISHI WA UMMA WAASWA KUWA WAADILIFU

Kaimu Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Jasper Mero (Mbele) akiingia katika ukumbi wa Kings way kufungua mafunzo ya awali (Induction course) kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi yanayofanyika katika Hoteli ya Kings Way Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Msadizi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Bibi Eliaika Manyanga (Kulia) akizungumza na waajiriwa wapya wa Ofisi hiyo katika mafunzo ya awali (Induction course) yanayofanyika katika Hoteli ya Kings Way Mkoani Morogoro.
Baadhi ya waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wakiwa katika mafunzo ya awali (Induction course) yanayofanyika katika Hoteli ya Kingsway Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Bw. Gerald Mwanilwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awali ya waajiriwa wapya wa Ofisi hiyo jana Mjini Morogoro.
Kaimu Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Jasper Mero (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awali kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi yanayofanyika katika Hoteli ya Kingsway Mkoani Morogoro.
Baadhi ya waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wakimsikiliza kwa umakini Kaimu Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Jasper Mero (hayupo pichani).
Kaimu Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Jasper Mero (Kushoto) akisisitiza jambo wakati akijibu maswali mbalimbali ya waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
Kaimu Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Jasper Mero (Katikati waliokaa) na baadhi ya viongozi waandamizi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waajiriwa wapya wa Ofisi hiyo. PICHA ZOTE NA SAIDI MKABAKULI.

Na Saidi Mkabakuli

Watumishi wa umma nchini wameaswa kuwa waadilifu na kuzingatia ubora wa kazi wakati wanatoa huduma kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Jasper Mero wakati akifungua mafunzo ya awali ya wiki moja kwa waajiriwa wapya 130  wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi yanayofanyika katika Hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro.

Bw. Mero amesema kuwa udilifu na ubora kwa watumishi wa umma ni kinga dhidi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na ni moja kati ya njia zinazowawezesha watumishi wa umma kuwa wachapakazi hodari.

“Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inaamini katika “Ubora”kwa kila inachokifanya ukianzia ubora wa taarifa za ukaguzi zinazotolewa, huduma bora kwa wadau wake, ubora wa watumumishi kwa maana ya taaluma, maadili, weledi,” alisema Bw. Mero.
Ameongeza kuwa Falsafa hii ya ubora ndiyo iliyoifanya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kupata umaarufu mkubwa kikanda na Kimataifa.   

“Kiwango cha juu cha Ubora wa kazi zetu na utendaji wa kazi unaozingatia weledi vitaweza tu kufikiwa kwa kuajiri watumishi wenye sifa stahiki, maadili, na bidii ya kuchapa kazi na wanaoweza kwenda sambamba na kasi kubwa ya mageuzi katika Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi,” aliongeza Bw. Mero.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi hiyo, Bw. Gerald Mwanilwa alisema kuwa mafunzo elekezi ni matakwa ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, hususani Kanuni Na.103 (1-6) pamoja na Kanuni za kudumu za Utumishi Serikalini za 2009 Kifungu G.3 (a na b).

“Mafunzo haya ni kwa mujibu wa matakwa ya kisheria na yanalenga kutoa uelewa mahususi kwa waajiriwa wapya kulingana na kada zao,’ alisema.

Kwa mujibu wa Bw. Mwanilwa, kupitia mafunzo hayo, washiriki wataweza kuelewa namna ya kutekeleza majukumu yao kama Watumishi wa Umma pamoja na kupata fursa ya kujifunza Miongozo na Nyaraka mbalimbali watakazozitumia kama watumishi wa umma na wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali. 

Pia, kupitia mafunzo hayo watapata fursa ya kujifunza na kuelewa utamaduni wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi unaosisitiza kufanya kazi kwa uweledi, uadilifu na kwa kuzingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa ambapo ofisi yetu ni Mwanachama (Intosai Afrosai na Afrosai-E).

“Mafunzo haya ni ya wiki moja yatatoa fursa kwenu kujua maana ya kuwa mtumishi na kazi za mkaguzi na miiko au maadili yake. Pia mtaelezwa kwa kifupi na kupewa utangulizi kuhusu Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, sheria mbali mbali, Kanuni na taratibu ili kuwawezesha kuelewa na kufanyakazi kama watumishi wa umma,” aliongeza Bw. Mwanilwa.

No comments:

Post a Comment