Tuesday, July 28, 2015

WAKATI UMEFIKA KWA SEKTA BINAFSI KUJENGA UTAMADUNI WA KUTOA RUZUKU ZA TAFI- DR.SHEIN




 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua rasmi Jengo Jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania { COSTECH} Ofisi ya Zanzibar liliopo ndani ya majengo ya zamani ya ilichokuwa kiwanda cha Sigara Maruhubi Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif wa pili kutoka Kushoto akipata maelezo kutoka kwa Wataalamu  wa Chuo cha Utafiti Kizimbani  wakiongozwa na Said Suleiman Bakari jinsi zao la viazi vitamu linavyoweza kutumiwa vyema katika utengenezaji wa Juisi. Wa kwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Majini Magharibi Mh. Abullah Mwinyi.
Watafiti na wawakilishi wa Vikundi vya wajasiri amali waliopata ufadhili kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia wakimpatia maelezo Balozi Seif wakati akiangalia maonyesha mara baada ya kulifungua Jengo la Tume hiyo.
Baadhi ya Wataalamu na wajasiri amali kutoka vikundi tofauti Nchini wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo Jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia { COSTECH }.
Balozi Seif akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Jengo la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia hpo Maruhubi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziI Dr. Ali Mohammed Shein.
 Balozi Seif akiwa katika Picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania { COSTECH } mara baada ya uzinduzi wa jengo la Tume hiyo hapo Maruhubi.
                                               
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema wakati umefika kwa sekta binafsi kujenga Utamaduni wa kutoa ruzuku za tafiti kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ili ijipatie nguvu za ziada za uwezeshaji wa kuendesha shughuli zake za utafiti kama nchi nyengine Duniani zilizofanikiwa kwa kufuata mfumo huo.

Alisema kufanya utafiti kunahitaji nguvu kubwa ya fedha kiasi kwamba Serikali pekee haiwezi kumudu kugharamia bila ya kushirikisha taasisi mbali mbali za sekta binafsi za ndani na nje ya nchi.

Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia { COSTECH } liliopo Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania imeonyesha mwanga wa kusaidia jamii kwenye tafiti za kina za Kimaendeleo zitakazomkomboa Mtanzania kutoka katika dimbwi la umaskini na kuelekea kwenye maendeleo ya kweli. 

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH  Dr. Hassan Mshimba alisema ujenzi wa Ofisi ya Tume hiyo hapa Zanzibar  ni kutekekeza ahadi iliyotoa Uongozi wa Taasisi hiyo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mwaka 2012.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Costech alisisitiza kwamba katika azma ya kukuza ajira Nchini Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imekusudia kuungana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha vitengo vya Utafiti Zanzibar kama alivyosisitiza Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein siku ya Utafiti Tarehe 12 Disemba mwaka 2014.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Kanal Mstaafu Joseph Simba Kalia ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa ukarimu wake wa kutoa Jengo kwa ajili ya Ofisi za Tume hiyo.

Kanal Mstaafu Simba Kalia alisema kitendo hicho kilichofanywa na  SMZ ni uthibitisho wa kuthamini umuhimu wa fani ya Utafiti ambayo ndio chachu ya maendeleo ya jambo lolote lile hapa Ulimwenguni.

Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojiaawali  ilizinduliwa  rasmi mnamo Tarehe 11 Juni Mwaka 2012 katika Majengo ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyopo Tunguu Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuanza kutoa huduma zake hapa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment