Tuesday, July 28, 2015

PSPF NA MAX MALIPO WAUNGANA KUKOMBOA WAJASIRIAMALI

Na Benjamin Sawe,Maelezo

Mabadiliko katika sekta ya hifadhi ya jamii nchini yamepelekea kuwepo na mabadiliko ya sheria ya mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma (PSPF). Sheria ya Mfuko wa pensheni wa PSPF sasa inaruhusu kusajili wanachama katika sekta zote za umma na binafsi. Na kwa sasa mfuko una mipango miwili ya uchangiaji wa lazima yaani PSPF Mandatory Scheme na mpango wa uchangiaji wa hiari yaani PSPF Supplementary Scheme

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwandishi wa Makala hayaBi Mwanjaa Sembe, Meneja Mpangowa Uchangiaji wa Hiari PSPF anasema uwasilishaji michango kwa kutumia huduma ya MaxMalipo itawasaidia wachangiaji kupata huduma za michango yao.

Anasema huduma ya kulipia kupitia mfumo wa Maxmalipo imeanzishwa na mfuko wa pensheni wa PSPF kwa ajili ya kupanua wigo kwa wanachama wa mfuko huo kuchangia na kujua salio la michango yao popote walipo ambapo huduma hiyo itawarahisishia watumiaji kutosafiri kwa umbali mrefu ili kupata huduma hiyo.
Mfuko umeona adha na shida walizokuwa wanazipata wateja wetu ndio maana tukaamua pamoja na huduma nyingine zitolewazo na mfuko wetu tujiunge na wenzetu wa Kampuni ya MaxCom inayotoa huduma ya Max Malipo ili kuweza kuwakomboa wateja waweze kuchangia pamoja na kujua kiasi cha michango yao kwa urahisi kwa kutumia huduma hiyo hivyo kuwafanya kuwa na muda mrefu wa kutafuta kipato badala ya kusafiri kwa umbali mrefu kufuata huduma.Anasema Bi. Sembe.

Anasema masuala ya hifadhi ya jamii yanagusa kiini muhimu sana cha wafanyakazi kwenye sekta rasmi na sekta zisizo rasmi hasa za watu masikini pamoja na sekta ya bima za jumuiya za waajiri.

Uchunguzi unaonyesha kuwaIdadi kubwa ya watu waliomo katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii ni wale ambao wameajiriwa kwenye sekta iliyo rasmi. Hifadhi ya jamii ni haki ya kila mtu ndiyo maana mfuko wa pensheni wa PSPF wana mpango wa uanachama wa hiari kama mkakati wa makusudi juu ya kupanua wigo wa hifadhi ya jamii ili kuhakikisha ya kuwa hata wale waliojiajiri kujiunga na mfuko wa PSPF na hata wale wanachama wa mifuko mingine iliyopo kuweza kuweka akiba ya ziada.

Hili ni jambo ambalo liko wazi kabisa ya kwamba kila binadamu ana uhusiano mkubwa na hifadhi ya jamii iwe kinadharia au kivitendo kutoka kuzaliwa kwake mpaka kufa, binadamu mwenyewe lazima ajishughulishe na kazi hatarishi na kuugua magojwa mbalimbali hivyo binadamu lazima akumbane na majanga mbalimbali kama vile majanga ya kiuchumi na ya kijamii yanayosababishwa na kukoma au kupungua kipato kutokana na maradhi, kujifungua, ukosefu wa ajira, ulemavu, uzee, kifo na kuongezeka kwa gharama za matibabu.

Majanga yote ni matukio ya kila siku kwa binadamu ambayo hayatabiriki na yote yanaaangukia kwenye mpango wa hifadhi ya jamii. Hivyo ni kitu cha asili ya kwamba kila mtu lazima ajue hifadhi ya jamii ni nini kwa sababu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu.

Bi Matilda Nyallu Meneja Msaidizi wa Mfuko wa Uchangiaji wa Hiari  kutoka PSPF anasema aina za mafao yanayotolewa na mpango huo wa hiari ni kama vile fao la uzeeni, fao la kifo, fao la elimu, fao la ujasiriamali , fao la ugonjwa/ulemavu, na  fao la kujitoa.

Anasema mtu yeyote aliyejiajiri, mkulima, mvuvi, mfanyakazi wa ndani, wafanyabiashara wadogo wanaweza kujiandikisha kwa hiari na kulipa kadri ya uwezo wake wa kipato kwenye mfuko wa pensheni wa PSPF. 

“Uchangiaji katika mpango huu wa hiari wa PSPF Wanachama wana uhuru wa kuchagua jinsi ambavyo wanaweza kuwasilisha michango yao, iwapo ni kwa siku, wiki, Mwezi au kwa msimu kutegemea na upatikanaji wa kipato cha mwanachama.Michango huwasilishwa moja kwa moja kupitia akaunti za benki au wakala wa Maxmalipo, M-pesa, Tigo-pesa na Airtel money, ambapo kiwango cha uchangiaji ni kuanzia shilingi 10,000 za kitanzania au zaidi” Anasema Bi Matilda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko huo Bwana Adam Mayingu anasema makubaliano waliyoyafikia na Kampuni ya MaxCom yatasaidia PSPF kutumia mtandao wa mawakala hao kutoa huduma kirahisi

‘Sasa wateja wetu wanaweza kutumia mawakala wa Maxmalipo waliopo kote nchini kuchangia michango yao ikiwa ni pamoja na kupata risiti na kujua kiwango chake anachochangia kwa muda wowote pasipo kusafiri kwa umbali mrefu.’.Anasema Bw. Mayingu.

Anasema kwa sasa dunia imekuwa kijiji na PSPF imekuwa ikiendana na mabadiliko yanayoendelea popote ulimwenguni ili kuweza kukidhi kiu na matarajio ya wateja wao ikiwa ni pamoja na soko la ushindani wa kibiashara.

Katika mahojiano na mwandishi wa malaka haya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Maxcom Tanzania Juma Rajabu anasema huduma ya Maxmalipo ni rafiki na rahisi kutumia kwa watumiaji na imeenea nchini kote hivyo itawarahisihia na kuboresha utendaji kazi wa PSPF.

Unajua sasa hivi mtandao ndio kila kitu katika ulimwengu wa biashara, watu hawana muda wa kupotezaau kusafiri kwa umbali  mrefu wanataka kufanya jambo la haraka na lenye uhakika na kuendelea na shughuli nyingine za uzalishaji mali na kuchangia katika kipato chao na nchi kwa ujumla, haya ndio mabadiliko yanayoendelea kwa kasi zaidi duniani kote, Anasema Bwana Rajabu.

Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Juma Nkamia ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa huduma hiyo anasema kuanzishwa kwa huduma hiyo kutawasaidia wajasiriamali kuokoa muda.

Kwa upande wake  Hadji Jamadary Afisa uendeshaji wa Mpango wa Uchangiaji wa Hiari wa PSPF   anasema watu wengi wanajiunga na mfuko huo kutokana na ubora wa mafao yake na faida inayotolewa kwa mwanachama wa mpango wa hiari.


“PSPF sasa ni kwa watu wote walio kwenye sekta rasmi na wale ambao hawako kwenye sekta rasmi maana lengo letu ni kuwafikia watu wengi ndani na nje ya nchi kupitia mpango huu wa uchangiaji wa hiari (PSS) ambao kiwango cha chini cha uchangiaji ni sh.10,000.” anasema Bw. Jamadary.

Aidha Mafao katika mpango huo wa hiari mwanachama atastahili kulipwa michango pamoja na riba inayokokotolewa kwa mujibu wa viwango vya riba vilivyoko katika soko kulingana na mfumuko wa bei.

Anasema mafao yaliyopo katika mpango wa hiari ni ya aina sita (6) kama vile fao la elimu ambalo litatolewa kwa mwanachama ambaye amechangia kwenye mfuko kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na mbili (12). Nusu ya akiba ya mwanachama yaani asilimia 50 ya mchango inatumika kulipa fao hili na nusu yake inayobaki katika akaunti ya mwanachama hutumika kwa ajili ya akiba ya uzeeni. 

Kwa upande wa fao la ujasiriamali linatolewa kwa mwanachama ambaye amechangia kwenye mfuko kwa kipindi kisichopungua miaka kumi na mbili (12). Nusu ya akiba ya mwanachama yaani asilimia 50 ya mchango inatumika kulipa fao hili na nusu yake inayobaki katika akaunti ya mwanachama hutumika kwa ajili ya akiba ya uzeeni. 

Mpango huo wa hiari Mwanachama anapata hata fao la uzeeni ambalo hulipwa kwa mwanachama aliyefikisha miaka 55 au zaidi. Mwanachama analipwa akiba yake ya asilimia mia moja (100%) pamoja na riba itakayokokotolewa. Mwanachama anapaswa kujaza fomu ya maombi na kuambatanisha kitambulisho cha uanachama.

Fao la kifo hulipwa kwa wategemezi wa mwanachama aliyefariki. Malipo yanayolipwa ni ya asilimia mia moja (100%) ya akiba ya mwanachama na riba inayokokotolewa.

Aidha Wategemezi wanapaswa kuwasilisha cheti cha kifo, kitambulisho cha uanachama cha marehemu pamoja na nyaraka za mahakama zinazodhibitisha msimamizi wa mirathi na wategemezi wa marehemu pamoja na mgao wa mirathi.

Fao la ugonjwa au ulemavu huwa linatolewa kwa mwanachama ambaye kutokana na sababu za ugonjwa au ulemavu hataweza tena kumudu kufanya kazi za uzalishaji kwa ajili ya kujipatia kipato cha kila siku.
Mwanachama analipwa asilimia mia moja (100%) ya akiba yake pamoja na riba inayokokotolewa. Mwanachama anawasilisha barua ya maombi, kitambulisho cha uanachama na uthibitisho wa taarifa ya daktari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric Shigongo, ambaye ana washawishi wananchi kujiunga na huduma hiyo aliwaasa wajasiriamali  mbalimbali wakiwemo wanasoka, waendesha bodaboda, wavuvi na wengineo kujiwekea akiba kupitia mpango huo.

Bi. Rahel Chizoza mwanahabari wa Clouds Media anasema Uchangiaji kwa kutumia mfumo wa MaxMalipo unaumuhimu mkubwa katika jamii kwa ujumla kwani unashirikisha sekta rasmina isiyo rasmi na utakuwa ndio nguzo mojawapo ya kujiongezea kipato na hata kujiwekea akiba ya uzeeni ikiwa ni pamoja na kuokoa muda wa mchangiaji kusafiri umbali mrefu.

‘Huduma hii ni nzuri sana ndugu mwandishi kwani tumekuwa tukiacha shughuli zetu za uzalishaji mali na kusafiri kwa umbali mrefu ili kujua kiasi cha michango tunayochangia lakini kwa sasa PSPF wameturahisishia maana hata nikiwa Mafia sina haja ya kuja Dar es Salaam au kutoka Kijijini kuja mkoani kwa ajili ya kupata huduma ya kuchangia.Anasema Bakari Mbilambi mwanachama wa mfuko huo.

Mfuko wa pensheni wa PSPF una uzoefu wa muda mrefu katika sekta ya hifadhi ya jamii tangu Julai 1999 na umekuwa na mafanikio makubwa hadi kuanzisha Mpango wa Uchangiaji wa Hiari mwezi Februari 2013.Hadi kufikia mwezi Juni 2015.Mpango huu umesajili zaidi ya wanachama 38456.


Makala haya yameandikwa na Benjamin Sawe, Afisa Habari, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, email sawebenjamin@gmail.com, simu: 0718028790.

No comments:

Post a Comment