Sunday, July 5, 2015

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA IBADA YA MAADHIMISHO YA JUBILEE YA MIAKA 125 YA INJILI YA KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI MASHARIKI MBUYUKENDA, TANGA TAREHE 05 JULAI, 2015


Mheshimiwa Baba Askofu, Dkt. Stephen Munga, Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki;
Waheshimiwa Maaskofu;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula;
Waheshimiwa Wageni Wote Toka Ndani na Nje ya Tanzania;
Waheshimiwa Wana-Dayosisi na Wananchi Wote Mliopo Hapa;
Mabibi na Mabwana;
Bwana Yesu Asifiwe:
          Nakushukuru sana Baba Askofu Stephen Munga kwa kunialika na kunishirikisha kwenye ibada hii ya kihistoria ya Maadhimisho ya Miaka 125 ya Injili katika Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.  Kwa kweli  ni jambo la furaha na heshima kubwa kwangu  kujumuika na Maaskofu na waumini wa Kanisa hili kwa tukio hili kubwa na la kihistoria.      Mwaliko wenu huu kwangu ni uthibitisho wa uhusiano mzuri uliopo baina ya KKKT na Serikali nchini.  Uhusiano ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu na watu wake. Uhusiano ambao umejitafsiri katika umoja, upendo, amani, na mshikamano uliopo baina ya Watanzania wa rangi zote, dini zote, makabila yote na wa popote watokako na walipo.
Maadhimisho ya Miaka 125
Mheshimiwa Baba Askofu,
Waumini Wote na Wageni Waalikwa;
          Siku kama ya leo, miaka 125 iliyopita ndio siku ambayo Wamisionari wa Kijerumani wa Bethel wapoliwasili mahala hapa. Kwa maelezo yako, walipachagua hapa kuwa ni mahala pa kuwahifadhi vijana waliokombolewa kutoka utumwani.  Hivyo mahala  hapa paliwapa uhuru, na matumaini mapya watu ambao walikwishakata tamaa. Aidha, kutokea hapa, ndipo kazi ya injili ilipoenea na kusambaa mkoani Tanga. Kusimama na wanyonge, kuwafuta machozi na kuwatua mzigo wao, ni jambo la heri, ni jambo jema na ni  jambo linalompendeza Mungu.  Na huo ndiyo msingi imara wa Kanisa hili.
Huo pia ndiyo msingi ambao juu yake imejengeka kazi na wajibu wa Serikali. Sisi katika Serikali tunao wajibu wa kuwaondolea wananchi unyonge, kuwapunguzi umaskini, kuwalinda na kuwakinga dhidi ya dhuluma na uonevu na kuwajengea msingi bora wa maendeleo yao.  Jitihada zetu za kuondoa umasikini, kutoa fursa za elimu, kuboresha huduma za afya na mambo mengi mengineyo tufanyayo yana malengo hayo.  Jitihada za Serikali zinapounganika na zile za madhehebu ya dini tunatengeza nguvu kubwa ya kuwaondolea wananchi wetu siyo tu unyonge wa kiroho, bali pia kuwapunguzia changamoto za maendeleo zinazowakabili na kusaidia kuinua hali zao za maisha.  
Mchango wa Dayosisi ya Kaskazini  Mashariki
Waheshimiwa Maaskofu, Ndugu Wananchi;
          Ninaposema hivyo,  natambua mchango wa Dayosisi  ya Kaskazini Mashariki katika kuwaletea maendeleo jamii na watu wa Mkoa wa Tanga. Mimi ni shahidi, maana nilifika kule Magamba, Lushoto  mwaka jana kufungua ukumbi wa kisasa katika Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa (SEKOMU) kilichojengwa na Dayosisi hii.  Pamoja na Chuo Kikuu, natambua mnazo shule za sekondari za Lwandai, Bangala na Dinari. Dayosisi hii inatoa pia huduma za kipekee ambazo hazipatikani kwa urahisi hapa nchini. Ninyi mna shule ya wasioona ya Irente, shule ya msingi ya watoto wenye ulemavu wa ubongo (Autism) na kituo cha kutunza wagonjwa wa akili cha Lutindi. 
Kwa upande wa Afya nako mmefanya mambo makubwa. Tunawashukuru kwa hospitali teule ya Wilaya ya Kilindi (Kilindi CDH) ambayo nilishiriki kuweka jiwe la msingi na kuizindua. Aidha nawapongeza kwa Hospitali yenu ya Bumbuli kuwa Hospitali Teule ya Halmashauri ya Bumbuli.  Hatua hiyo itaimarisha pia Chuo cha Waganga Wasaidizi (Clinical Officers Taining College)  cha Bumbuli.  
Napenda pia kupitia sherehe hii kuwashukuru ninyi wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kwa kazi yenu nzuri muifanyayo. Vile vile, nawashukuru sana kwa kuiunga mkono Serikali katika jitihada za kuwaletea maendeleo  Watanzania.  Nawaomba muendelee na moyo huo mwema. Namuomba Mwenyezi Mungu awaongezee pale mlipopunguza na kuendelea kuwashushia baraka tele.  
Mheshimiwa Baba Askofu,
Serikali inatambua na kuthamini sana ushirikiano baina yake na madhehebu na mashirika ya dini. Ndiyo maana tumekuwa tunatengeneza  mazingira mazuri kwa mashirika ya dini kuendesha shughuli zake. Tumekuwa tunatoa msamaha wa kodi, tunatoa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vyenu na kutoa ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa zahanati, vituo cha afya na hospitali ambazo Serikali inaingia ubia na Kanisa katika  kutoa huduma kwa wananchi. Aghalabu hata pale ambapo  Serikali hujenga zake utaratibu huo huachwa kuendelea. Nimetaja baadhi tu ya mambo ambayo tumekuwa tukishirikiana na kusaidiana.
Napenda kutumia nafasi hii kuwahakikishia kuwa tumekuwa tunafanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo kwa kutambua kuwa huduma za kijamii zitolewazo na mashirika ya dini zinawanufaisha Watanzania wote bila ubaguzi.

Maadili ya Jamii
Mheshimiwa Baba Askofu;
Ndugu Waumini na Wageni Waalikwa;
Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba viongozi wa dini kuongeza  maradufu kazi ya malezi ya jamii kimaadili. Sote ni mashahidi kuwa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili. Nadhani tumefika njia panda tusipofanikiwa kugeuza mwelekeo huu na kuchukua njia hiyo nyoofu tutaharibikiwa zaidi.  Maadili mema ya jamii pamoja na mila na desturi zetu vinapita katika mtihani mkubwa sana hivi sasa. Vitendo vya utovu wa maadili vinaendelea kufanyika na kuchukua nafasi kubwa katika maisha ya watu siku hizi. Inaanza kutaka kujengeka dhana potofu ati  kuwa ni mambo ya kawaida au ndiyo usasa. Hali hii haistahili kuachwa kuendelea kumong’onyoa misingi ya uadilifu ya jamii zetu na ya ubinadamu wetu.
Viongozi wa dini mnalo jukumu zito  na nafasi maalum kwenye hili: kubwa ya kukemea na kurekebisha jamii mkianzia na waumini wenu wanaokwenda kinyume na maadili mema ya dini,  jamii na nchi yetu.  Hamna budi kujitahidi kuwarudisha kwenye mstari mwema na maadili mema wanakondoo mliopewa kuwachunga.  Nasema hivyo kwa kutambua kuwa  wengi wa watu wote isipokuwa wachache sana katika wale wanaofanya maasi na maovu ni waumini wenu na wafuasi wa dini ambazo Mungu amewapa jukumu la kuongoza.  Sisi katika Serikali tuko tayari kutimiza ipasavyo wajibu wetu wa kisheria katika mapambano haya adhimu.  Naomba tuendelee kushirikiana kujenga maadili mema katika jamii na nchini kote kwa manufaa ya watu wetu na nchi yetu.
Dhima ya Viongozi wa Dini na Uchaguzi Mkuu
Mheshimiwa Baba Askofu;
 Waumini Wote na Wageni Waalikwa Wenzangu;    
 Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu ambao pia una umuhimu wa aina yake katika historia ya nchi yetu.  Tunaiaga Awamu ya Nne na kuikaribisha Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu. Niruhusuni nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa dini muiombee nchi yetu ipite kipindi hiki kwa salama na amani.  Uzoefu wa nchi nyingi za Afrika, chaguzi hutoa mwanya kwa uvunjifu wa amani. Haijawa hivyo kwetu, lakini haina maana kuwa tunayo kinga ya milele. Hata na sisi tunaweza kuwa kama wale iwapo yale yaliwafikisha wenzetu hapo hatutayaepuka.
Mafanikio yetu ya  kuendesha uchaguzi kwa amani na usalama yametokana na tahadhari ambazo Serikali na viongozi wa dini tumekuwa tukizichukua.  Tuendelee kufanya hivyo. Tusiwape mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu kuwafarakanisha Watanzania.  Tuendelee kukemea matumizi mabaya ya fedha,  rushwa, hila, ghilba na hujuma katika chaguzi.  Tunapaswa kufanya hivyo tena zaidi sasa, wakati wa michakato ya ndani ya vyama vya siasa na baadae wakati wa uchaguzi.  Tuwakemee wanasiasa  wapenda madaraka kwa gharama yoyote, ambao watataka kutumia fedha kununua ushindi au  ubaguzi wa rangi, kabila, dini na kadhalika, kuwabagua wapinzani wao na kujijenga kisiasa.  Nawaomba msiwasikilize wala kuwaendekeza kwani mchezo wao ni mauti yetu.   Wakatalieni kwa macho makavu na kwa kweli muwanyanyapae.
Hatupaswi kukaa kimya dhidi ya watu wanaokiuka maadili na kuchochea mifarakano katika taifa letu. Hawa si watu wema watatufikisha pabaya. Hawaitakii mema nchi yetu.  Kamwe tusiruhusu wachezee dini zetu ambazo ni mhimili muhimu sana wa amani yetu. Tofauti na ukabila ambao pamoja na ubaya wake, lakini unaweza kuhusisha eneo dogo, dini unahusisha nchi nzima.  Hakuna mtu, dini wala eneo litakalonusurika. Tutapoteza ile sifa yetu ya kihistoria ya kuwa lulu na mfano wa amani katika Afrika.  Tusikubali kumchukiza Mungu  akatukasirikia na kutuadhibu kwa jambo ambalo liko ndani ya uwezo wetu kulizuia lisitokee.  Kwa kweli mambo yakiharibika,  hatuwezi kumlaumu mtu mwingine yeyote bali  sisi wenyewe.  Katu hatuwezi kusema ni mapenzi ya Mungu bali itakuwa ni makosa yetu wenyewe.
Nawaomba viongozi wa dini mlisaidie taifa letu.  Limeni mraba wenu vizuri nasi tulime wetu. Msiwape nafasi viongozi wa siasa na hata wa dini kutumia majukwaa ya dini kuendeleza maslahi yao ya kisiasa na  hasa kupandikiza chuki katika jamii.  Tunawategemea  viongozi wa dini msiwe sehemu ya makundi ya wagombea au vyama vya siasa. Mnatakiwa msiwe na upande bali  muwe juu ya pande zote. Hapo ndipo mtakapofanya vizuri kazi yenu ya ulezi na kuponya  taifa iwapo kutatokea matatizo.
Hatuwategemei viongozi wa dini muwapangie waumini wenu vyama au viongozi wa kuwachagua. Tunawategemea kuwahimiza na kuwakumbusha kuutumia  haki na wajibu wao  vizuri, muwahimize na kuwakumbusha kuwa watatakiwa kufanya mambo matatu muhimu. Kwanza, kujiandikisha, pili, kujitokeza kwenda kupiga kura na tatu kuchagua viongozi wazuri, wasiokuwa waovu, wasiofanana na uovu na kuukaribia uovu, watakaosukuma mbele gurudumu la maendeleo na kujali maslahi mapana ya jamii husika na nchi yetu.
Mheshimiwa Baba Askofu;
Ndugu Waumini, Wageni Waalikwa;
Nawaomba muendelee kuiombea nchi yetu iendelee kuwa ya amani na utulivu, watu wake wadumishe upendo na mshikamano miongoni mwao.  Aidha, muuombee Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2015 uwe wa salama, amani na haki ili taifa letu lipate viongozi wazuri na liendelee kuwa tulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Hitimisho
Mheshimiwa Baba Askofu;
Kama mnavyofahamu, nakaribia kumaliza kipindi changu cha uongozi wa nchi yetu. Baada ya uchaguzi wa Oktoba, 2015 tutakuwa na Rais mwingine.  Napenda kutumia fursa hii kuwaaga maana naweza nisipate fursa kama hii tena katika kipindi kilichobaki.  Nawashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa mlionipa mimi binafsi na Serikali yangu katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wangu.  Tumeishi vizuri, tumeshirikiana na kufanikisha mambo mengi mazuri pamoja.  Kwa kweli nafarijika kuwa ninapoondoka madarakani, uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ni mzuri na umeendelea kuimarika.  Ndivyo nilivyoupokea kutoka kwa Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, na ndivyo nitakavyoukabidhi kwa Rais wa Awamu ya Tano. Ningependa sana kuuona uhusiano na ushirikiano huu ukikua zaidi na zaidi, siku hadi siku kwani uhusiano wenye maslahi kwa nchi yetu na watu wake.  Ni uhusiano  wenye kujenga umoja, amani, upendo na mshikamano miongoni wa watu wa Taifa letu hili  moja, na la watoto wa Mungu mmoja.  Daima nitawakumbuka na kuthamini mchango wenu na upendo wenu kwangu.
Nawashukuru tena kwa kunialika na nawatakia maadhimisho mema ya miaka 125 ya Injili. Mungu awabariki.  
Asanteni Sana, na Mungu Ibariki KKKT,
Mungu Ibariki Tanzania na Watu Wake,
Bwana Asifiwe.


No comments:

Post a Comment