Wednesday, June 24, 2015

NACTE YAVIFUTIA USAJILI VYUO VITATU (3) NA KUVISHUSHA HADHI VYUO KUMI NA SITA (16)

NACTE yavifutia usajili vyuo vitatu  (3) na kuvishusha hadhi vyuo  kumi na sita (16)
Dar es Salaam, 24 Juni 2015 Katika jitihada za kuinua ubora wa elimu ya ufundi nchini, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limevifutia usajili vyuo  vitatu na kuvishusha hadhi vyuo kumi na sita.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa NACTE Dkt. Adolf B. Rutayuga alisema kuwa, hatua hiyo imefikiwa baada ya vyuo husika kushindwa kurekebisha kasoro zilizobainishwa na NACTE.

“Kwa kutumia Sheria ya Bunge Sura Na. 129 na Kanuni za Baraza za Usajili (2001) na zile za Ithibati na Utambuzi (2001), mnamo tarehe 20 Februari 2015, Baraza lilitoa notisi ya siku 30 kwa taasisi na vyuo vilivyokiuka taratibu na vyenye mapungufu makubwa ya Usajili na Ithibati kupitia taarifa yake kwa Umma. Notisi hii ililenga kuzipa taasisi na vyuo nafasi ya kujitetea na kufanya marekebisho yaliyobainishwa,” alieleza.

Kaimu Katibu Mtendaji huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Ushauri na Malezi ya Taasisi na Vyuo vya Ufundi NACTE aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Baraza linakiri kuwa taasisi na vyuo vingi vilivyopewa maelekezo ya kufanya marekebisho vimechukua hatua mbalimbali za kurekebisha mapungufu yabainishwa. Hata hivyo alisema hadi kufikia leo tarehe 24 Juni 2015 yaani siku 124 baada ya Notisi ya Baraza, kuna vyuo ambavyo havijachukua hatua yoyote ya kurekebisha mapungufu yake.

 
“Baraza limeamua kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zake kwa taasisi na vyuo vyote vilivyoorodheshwa kwa makosa yafuatayo, moja kumalizika kwa muda wa  Usajili wa Awali (Preparatory Registration) na Usajili wa Muda (Provisional Registration); pili kutoanza mchakato wa kupata Ithibati baada ya kupata Usajili Kamili; tatu kumalizika kwa muda wa Ithibati na kutochukuliwa hatua ya kuomba upya Ithibati (re-affirmation); na nne taasisi na Vyuo kuamua vyenyewe kusitisha kutoa mafunzo kwa sababu mbali mbali,” alifafanua

Vyuo vilivyofutiwa usajili ni pamoja na Dar es Salaam College of Clinical Medicine cha jijini Dar es Salaam kilichokuwa kimepatiwa usajili wa awali, Ndatele School of Medical Laboratory Sciences cha Dar-es-Salaam kilichokuwa kimepatiwa usajili wa awali na Institute for Information Technology  cha jijini  Dar es Salaam pia chenye namba za usajili REG/EOS/014

Taassi/vyuo vilivyoshushwa hadhi  baada ya kushindwa kutiza mashart ni pamoja na Sura Technologies – Dar es Salaam,  Institute of Management and Information Technology – Dar es Salaam, Techno Brain - Dar es Salaam, Ministry of Agriculture Training Institute Igurusi – Mbeya, Mbozi School of Nursing – Mbeya, KCMC AMO Ophthalmology School – Moshi, KCMC AMO Anaesthesia School – Moshi, Advanced Pediatrics Nursing KCMC – Moshi.

Vingine ni, AMO Training Centre Tanga – Tanga, CATC – Songea, CATC – Sumbawanga, COTC Maswa – Shinyanga, COTC – Musoma, Dental Therapists Training Centre – Tanga, Ngudu School of Environmental Health Sciences – Kwimba na KCMC AMO General School – Moshi.

Kuhusu NACTE
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni chombo kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Sura ya 129, kwa lengo la kusimamia na kuratibu taaluma zinazotolewa na taasisi na vyuo vva elimu ya ufundi nchini, ambavyo siyo vyuo vikuu au vyuo vikuu vishiriki. Jukumu kubwa la Baraza ni kuendeleza na kuinua ubora wa elimu ya ufundi nchini kwa kusimamia kikamilifu shughuli za kuendesha mafunzo ili tuzo zinazotolewa na taasisi na vyuo ziwe na ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya ufundi(NACTE)Dkt. Adolf Rutayuga(katikati)akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam(hawapo pichani)wakati wa kutangaza ubora wa elimu ya ufundi inayotolewa na baraza hilo.Baraza hilo limevifuta usajili vyuo  vitatu na kuvishusha hadhi vyuo kumi na sita.Kushoto ni Mkurugenzi wa Mitaala wa baraza hilo Twilumba Mponzi na Msaidizi wa katibu Mtendaji Alex Nkondola.
 Wakurugenzi wa Manejimenti ya NACTE wakiwa kwenye mkutano pamoja na waandishi wa habari uliohusu kutangaza ubora wa Elimu ya ufundi inayotolewa na baraza hilo lilitangaza kuvifutia usajili vyuo vitatu na kuvishusha hadhi vyuo kumi na sita.
 Mwandishi wa habari kutoka kituo cha EAT, Noah Laltaila akimuuliza swali Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya ufundi(NACTE)Dkt. Adolf Rutayuga kwenye mkutano  uliohusu kutangaza ubora wa Elimu ya ufundi inayotolewa na baraza hilo lilitangaza kuvifutia usajili vyuo  vitatu na kuvishusha hadhi vyuo kumi na sita.
Baadhi ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wakiwa kwenye mkutano wa Baraza la Taifa la Elimu ya ufundi(NACTE) uliohusu kutangaza ubora wa elimu unaotolewa na baraza hilo.Baraza hilo limevifuta usajili vyuo  vitatu na kuvishusha hadhi vyuo kumi na sita.

No comments:

Post a Comment