Sunday, June 7, 2015

MAALIM SEIF AHUTUBIA KATIKA MKUTANO WA HADHARA ULIOFANYIKA KIBANDAMAITI, ZANZIBAR

Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipokelewa katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, baada ya kuwasili akitokea Dar es Salaam ambako aliteuliwa Rasmi kuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF mwaka 2015.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni mgombea Urais wa Chama hicho, akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Kibandamaiti mjini Zanzibar.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na mkewe Mama Awena Sinani Massoud, wakiwa kwenye jukwaa kuonesha furaha zao baada ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa chama hicho katika viwanja vya Kibandamaiti mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Kibandamaiti mijini Zanzibar.
Wafuasi na wapenzi wa chama cha wananchi CUF wakifuatilia mkutano wa hadhara wa CUF katika viwanja vya Kibandamaiti mjini Zanzibar.(picha na Salmin Said, OMKR).

Na: Hassan Hamad (OMKR).
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema anakusudia kuifanya Zanzibar kuwa visiwa vya fursa za biashara na ajira kwa wananchi.
Maalim Seif ambaye tayari Chama chake kimeshamteua rasmi kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, ameeleza hayo katika viwanja vya Kibandamaiti, wakati akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho kwa ajili ya mapokezi ya mgombea huyo.
Amesema Zanzibar inazo fursa nyingi za kuweza kunyanyua kipato cha wananchi, na kwamba ataweka kipaumbele katika kuziibua na kuziendeleza fursa hizo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji, ataisimamia ipasavyo Mamlaka ya vitega uchumi, ili kuondosha vizingiti vinavyokwamisha uwekezaji nchini.
Amefahamisha kuwa wapo wafanyabiashara wengi wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kuwekeza miradi mikubwa ya kiuchumi, lakini wamekuwa wakipata usumbufu, jambo ambalo ameahidi kulishughulikia muda mfupi baada ya kuingia madarakani.
Sambamba na hilo, Maalim Seif amesema iwapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar, atahakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na shirika lake la ndege ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ili kurahisisha shughuli za kibiashara ikiwemo Utalii.
Amesema hatua hiyo itakwenda sambamba na uboreshaji wa huduma za viwanja vya ndege, ambavyo vitaweza kutoa huduma bora kitaifa na kimataifa.
Aidha amesema chini ya uongozi wake iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, ataitangaza Zanzibar kuwa bandari huru, sambamba na kujenga bandari mpya itakayotoa huduma bora kwa mwambao wa Afrika Mashariki.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amesema anakusudia kuongeza viwango vya mishahara kwa wafanyakazi wote, pamoja na kuzingatia maslahi ya wastaafu na wazee wasiojiweza.
Akizungumzia kuhusu mafuta, Maalim Seif amesema anakusudia kuanzisha Wizara ya Mafuta na Gesi ili kurahisisha uchimbaji wa nishati hiyo, itakayoondosha hali ya umasikini katika visiwa vya Zanzibar.
Maalim Seif pia alizungumzia hali ya amani na utulivu nchini, na kueleza kuwa amani ya kweli itapatikana iwapo vyombo vinavyohusika vitatoa haki kwa wananchi wote.
Mapema akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, amesema Baraza Kuu la Uongozi la CUF limeshawika kumuidhinisha Maalim Seif kuwa mgombea Urais wa Zanzibar, kutokana na uwezo na nia ya dhati ya kuwatumikia wazanzibari.

Amesema viongozi waliopo madarakani wana dhamana na wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao unafanyika katika hali ya amani, sambamba na kuheshimu maamuzi ya wananchi katika uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment