Thursday, May 28, 2015

WAZIRI KOMBANI AIPA SOMO MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII NCHINI.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani ( kati kati) akisisitiza jambo.

 Katibu Mkuu wa TSSA, Meshack Bandawe ( kushoto ) akiwa na mwezeshaji wa mafunzi, Patrick Ngwila.

Na John Nditi, Morogoro

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, ameitaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini kuelekeza nguvu zao vijijini kwenye idadi kubwa ya  wananchi na wazalishaji wa mali wanaohitaji huduma zao badala ya kung’ang’ania mijini pekee.

Kombani alitoa changamoto hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku nne yaliyoanza Mei 25 hadi kufikia 28, 2015 mjini Morogoro ya  kuwajengea uwezo na ufahamu wafanyakazi wanaunda Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii Tanzania (TSSA) kutoka katika mifuko ya Hifadhi ya jamii ya PPF,NSSF,LAPF,GEPF,NHIF na ZSSF.

Hata hivyo alisema,  mifuko hiyo imekuwa ikikimbilia kutafuta wanachama katika maeneo ya mijini na kushindwa kubuni mbinu mbadala za kuwafikia wananchi wengi wanaoishi vijijini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo kuwa, dhana iliyojengeka kutoka kwa Mifuko hiyo kuwa vijijini hakuna watu wenye vipato sasa imepitwa na wakati kwa kuwa wananchi wanaishi vijijini  ni wakulima, wafugaji na wafanyabiashara ndogo ndogo ambao  wanaouwezo mkubwa wa kuchangia mifuko hiyo.

Waziri Kombani ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki(CCM) alisema , kutokana na mifuko hiyo kujikita katika maeneo ya mjini imekuwa ikitoa huduma hiyo kwa asilimia 4 na endapo itajitoa kuwafikia  watu wa maeneo ya vijijini inaweza kutoka hapo ilipo na kufikia asilimia 10 na zaidi.

“ Wilaya ya Ulanga pekee kuwa kuna kundi kubwa la wakulima,wafugaji na waendesha bodaboda” alisema na kuongeza kusema.

“ Mfano mfuko wa bima ya afya wao wamejitoa kwenda  kuhamasisha na wananchi wengi wameweza kujiunga na kuchangia huduma za matibabu na sasa  mifuko mingine ya hifadhi ya jamii inafaa  kufuata nyayo hizo za kubuni  mbinu mpya za kwenda maeneo ya vijijini kupata wanachama wengi” alisema Waziri Kombani.

Awali , Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii Tanzania (TSSA), Meshack Bandawe, alisema  malengo ya kuanzisha Jumuiya hiyo ni kufanya kazi kwa pamoja.

Hata hivyo alisisitiza kuwa lengo moja ili kuhakikisha sekta ya Hifadhi ya jamii inaimarishwa ili kuingiza Watanzania katika mifuko hiyo ili waweze kunufaika nayo katika maisha yao.

“ Tunayo mifuko saba ya Hifadhi ya Jamii na imewafikia watu asilimia 4.5 ...lengo ni kutoka hapo angalao kufikia wastani wa asilimia 10 “ alisema Bandawe.

Katibu Mkuu huyo ambaye pia ni Meneja wa PPF Kanda ya Ziwa alisema, kupitia Jumuiya hiyo sasa wataanza kuwaelimisha wananchi wote walioko rasmi katika soko ajira na wale wasio rasmi waweze kukingwa na mifuko ya hifadhi ya jamii .

Kwa upande wake Mwezeshaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, Patrick Ngwila,alisema kwa sasa  wanaangalia namna ya kuiboresha mifuko hiyo kwa kupata uzoefu wa namna ya mifuko hiyo inavyofanya kazi katika nchi hizo ambayo imekuwa ikisaidia wananchi hasa wanaoishi katika maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa Mwezeshaji huyo kuwa,  kupitia mafunzo hayo wanaangalia namna ya kupata wanachama ambao ni Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuweza  kuchangia kwenye mifuko hiyo wakiwa huko na wale wanaoishi maeneo ya vijijini.

No comments:

Post a Comment