Friday, May 29, 2015

Simbachawene aitaka Australia kuimarisha uwekezaji nchini

Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Afya na Utalii kutoka Australia Magharibi Kim Hames (kushoto) akimweleza Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (Kulia) maeneo ambayo nchi ya Australia ingependa kuwekeza.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (Kulia) akimshukuru Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Afya na Utalii kutoka Australia Magharibi Kim Hames (kushoto) mara baada ya kumkabidhi zawadi. Wengine ni ujumbe ulioambatana na Naibu Waziri Mkuu huyo.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ( wa pili kutoka kulia) Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Afya na Utalii kutoka Australia Magharibi Kim Hames ( wa tatu kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Australia uliohudhuria kikao hicho.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ameitaka nchi ya Australia kuimarisha uwekezaji katika sekta za nishati na madini nchini ili ziweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Simbachawene aliyasema hayo katika kikao chake na Naibu Waziri Mkuu wa Australia Magharibi, Kim Hames na ujumbe wake aliyemtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kupata taarifa za maeneo yanayohitaji uwekezaji nchini.

Alisema uhusiano kati ya Tanzania na Australia ni wa muda mrefu, ambapo Australia imekuwa ikiwekeza nchini kupitia sekta ya madini kupitia makampuni yake ya madini na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Aliendelea kusema kuwa kupitia makampuni ya madini ya Australia, huduma za jamii kama vile miundombinu, elimu na afya zimeboreshwa.

Wakati huo huo Afisa Mtendaji kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) Prof. Abdulkarim Mruma akielezea ushirikiano kati ya wakala huo na Australia, alisema kuwa nchi ya Australia kupitia chuo chake cha Cuten ilishirikiana na GST katika kufanya utafiti wa madini katika ukanda wa dhahabu ulioko kusini mwa Dodoma uliopelekea kugundulika kwa madini ya  dhahabu na almasi.

Aliongeza kuwa kupitia utafiti wa madini katika ukanda wa dhahabu ulioko Dodoma watumishi wawili kutoka wakala huo walifanikiwa kupata shahada za uzamifu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Cuten.

Aliongeza kuwa, nchi ya Australia imekuwa ikitoa ufadhili kwa watumishi wake kusomea katika musala ya uchenjuaji madini na maabara katika ngazi za shahada na uzamifu.

Profesa Mruma aliiomba nchi ya Australia kuendelea kusaidia Wakala huo kwa vifaa vya kisasa vya jiofizikia na kemia pamoja na mafunzo yanayohusu madini katika ngazi mbalimbali.

Naye Mkuu wa Chuo cha Madini, Sudian Chiragwile aliongeza kuwa, chuo kilikabidhiwa mgodi wa Resolute uliokuwa unamilikiwa na kampuni ya Golden Pride ya Australia ambapo wamekuwa wakiutumia kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.

Alisema mgodi wa Resolute ulioachwa bado una eneo kubwa linaloweza kuchimbwa madini na kuwataka wawekezaji kutoka Australia kujitokeza na kuwekeza kwenye shughuli za madini.

Naibu Waziri Mkuu wa Australia ambaye pia ni Waziri wa Afya na Utalii kutoka Australia Kim Hames alisema kuwa, nchi ya Australia ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji hususan katika sekta za nishati na madini na kuongeza kuwa katika kuboresha sekta ya madini, kutakuwa na programu za kubadilishana utaalam na uzoefu kwa wataalam kutoka Tanzania na Australia.

Hames alisisitiza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini na kuahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuinua sekta ya madini nchini.

No comments:

Post a Comment