Tuesday, May 12, 2015

Mwana Habari Luqman Maloto azindua kitabu cha wagombea Urais

Mwandishi wa habari mzoefu, Luqman Maloto akikitambulisha kitabu chake kijulikanacho kwa jina la “The Special One 2015 Nani Ajaye?” wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mwandishi wa habari mzoefu, Luqman Maloto akimkabidhi mwandishi wa habari wa televisheni ya TBC, Angella Msangi kitabu chake kijulikanacho kwa jina la “The Special One 2015 Nani Ajaye?”.
Mwandishi wa habari mzoefu, Luqman Maloto akimkabidhi mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Tatu Mohamed kitabu chake kijulikanacho kwa jina la “The Special One 2015 Nani Ajaye?”.
Mwandishi wa habari mzoefu, Luqman Maloto akimkabidhi mwandishi wa habari wa televisheni ya Azam, Temeluge Kasuga kitabu chake kijulikanacho kwa jina la “The Special One 2015 Nani Ajaye?”

Na Mwandishi wetu
Mwanahabari mzoefu nchini, Luqman Maloto amezindua kitabu kinachoelezea wasifu wa wagombea Urais wa uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba kijulikanacho kwa jina la ‘The Special One 2015 Nani Ajaye?’ ambacho kwa sasa kipo mitaani.

Akizungumza jijini, Maloto amesema kuwa ameamua kuandika kitabu hicho kutokana na kutambua wajibu wake na kutoa mchango kwa nchi yake kama raia hasa kwa kutumia taaluma yake ya uandishi wa habari ili kuwawezesha wapiga kura kumchagua kiongozi bora.

Maloto alisema kuwa kitabu hicho kitawarahisishia wapiga kura kumchagua kiongozi huku wakiwa na ufahamu wa kutosha kwani ameweza kuwachambua wasifu wa viongozi ambao wamejitangaza au kutajwa kuwa mstari wa mbele kukielekea kiti cha urais.

“Kwa mujibu wa kalenda iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imebaki miezi mitano tu ili Watanzania kwa utashi wetu, tuweze kumchagua Rais Ajaye, vilevile wabunge na madiwani wetu. Kwa kutambua umuhimu wa uchaguzi na kwa kuona nami ninao wajibu wa kutoa mchango kwa nchi yangu,” alisema Maloto.

Alisema kuwa kusudio kubwa la kitabu “The Special One 2015 Nani Ajaye” ni kumfanya Mtanzania kutambua kwamba tupo kwenye kipindi cha mabadiliko kutokana na ukweli kuwa kwa sasa tunatoka kwenye maisha ya mazoea na lengo la sasa ni kujenga nchi yetu katika misingi ya ukweli unaojitosheleza.

“Lazima kuondokana na kasumba ya kufanya uamuzi kama kuuziwa mbuzi kwenye gunia. Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni dhamana kubwa sana, hivyo lengo kuandika kitabu hiki ni kuwatambua japo kwa ukaribu wagombea wanaotajwa, kuelekea kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu 2015,” alisema.

Alifafanua kuwa Kitabu hiki kimegusa majina 25, miongoni mwao wapo waliojitangaza kwa nia zao, wengine wanapendekezwa na wapo ambao wanatajwa chini kwa chini. Wote wameandikwa ili wajulikane. Lengo ni kumsaidia Mtanzania kufanya uamuzi sahihi.

Kwa mujibu wa Maloto, kila jina limemulikwa katika pande mbili. Upande uliojaa utukufu, upo ule wenye kasoro ambazo zinatambulika. Hili limefanyika kwa ajili ya kutengeneza mzani wenye ulinganifu. Kitabu hiki siyo jukwaa la kumsaidia mtu kisiasa, ila ni tochi la kuwaangazia Watanzania kuwajua wale wenye uelekeo wa kushika hatamu ya uongozi  mkuu wa nchi yao.

Alisema kuwa ni kitabu cha vyama vyote, majina ya wanaotajwa au kufikiriwa kuwa mmoja wao anaweza kusimamishwa kugombea Urais 2015, katika ushirika wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), yamechambuliwa.

Alisema kuwa ameweza kuchambua majina manne yaliyochomoza katika Ukawa; Freeman Aikaeli Mbowe, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, James Francis Mbatia na Dk. Willibroad Peter Slaa, yamechambuliwa. Utafiti wa kuwatambua wahusika umefanyika na utakachokisoma ndani ni uchambuzi baada ya utafiti.

Pia ameyachambua kwa kina majina 20 ya CCM yamechambuliwa baada ya utafiti. Edward Ngoyai Lowassa, Dk. Asha-Rose Mtengeti Migiro, Profesa Mark James Mwandosya, Stehen Masato Wasira, William Mganga Ngeleja, Lazaro Samuel Nyalandu, Dk. Hamisi Andrea Kigwangalla, Zakhia Hamdan Meghji, Emmanuel John Nchimbi na Fredrick Tluway Sumaye.

Wengine ndani ya CCM ni Samuel John Sitta, January Yusuf Makamba, Anne Semamba Makinda, Jaji Augustino Mathew Ramadhan, Charles Makongoro Nyerere, Mwigulu Lameck Nchemba, Dk. Ali Mohamed Shein, Mizengo Peter Pinda, John Pombe Magufuli na Bernard Kamillius Membe.

“Ni imani kubwa kwamba miongoni mwao, ndiyo atapatikana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hiyo vema kuwasoma na kuwaelewa, kwani hatutarajii kupata Rais kutoka mbinguni kwamba Mungu atamteremsha,” alisema.

Alisema kuwa kitabu kimeonesha kwa upana kabisa kila mmoja na ubora wake. Kisha udhaifu wake. Hii inamaanishwa kuwa hatwendi kumchagua malaika. Ni binadam, kwa hiyo lazima kumuelekea yule mwenye afadhali, kwa maana ubora wake unakuwa mkubwa kuliko udhaifu.

Maloto alisema kuwa kila mwisho wa uchambuzi wa kila jina kuna hitimisho ambalo linaweka ulinganifu kwa kutaka apimwe kwa mazuri yake na kuoanisha kasoro alizonazo. Kwamba je, uzuri na ubaya upi unakuwa mkubwa zaidi? Kwa maana hutampata asiye na kasoro. Huyo ambaye hana kasoro utampataje?

Kitabu hiki kisaidie Watanzania kuwajua viongozi wao na kufanya uamuzi kwa uhakika na siyo kwa kubahatisha.

“Natumaini kupata ushirikiano mzuri kutoka kwako, ili taarifa za kitabu hiki ziweze kuwafikia watanzania, vivyo hivyo kiweze kusomwa na wengi na kuwawezesha wapiga kura kumchangua mgombea wanayemjua,” alisema.

No comments:

Post a Comment