Thursday, April 9, 2015

WAZIRI MAGUFULI AHUDHURIA MAHAFALI YA KUMI YA KIDATO CHA SITA KATIKA SHULE YA SEKONDARI YA CHATO, AAHIDI MAJENGO YA KAMBI YA MKANDARASI KUWA MALI YA SHULE YA MAGUFULI

 Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato Mkoani Geita, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapongeza wanafunzi wa kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Chato wanaotarajiwa kuhitimu masomo yao mwezi ujao.
 Wanafunzi wa kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Chato Mkoani Geita wanaotarajiwa kuhitimu masomo yao mwezi ujao wakiimba wimbo maalum wa Shule hiyo katika Mahafali ya 10 shuleni hapo.
 Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi cheti mwanafunzi mmojawapo katika mahafali hayo.
 Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia kazi ya uchanaji wa mbao katika Shule ya Sekondari Chato. Mbao hizo hutumika katika kazi mbalimbali za ujenzi wa shule hiyo. Pia Dkt. Magufuli ameichangia shule hiyo kiasi cha Shilingi Milioni tano.
 Waziri Magufuli akikagua moja ya computer katika shule hiyo.kushoto kwake ni Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Mahendeka Mafele.
 Dkt. Magufuli akipiga ngoma pamoja na kikundi cha Skauti cha Shule ya Sekondari Chato kabla ya kuanza kwa mahafali hayo.
 Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikagua  maabara ya shule hiyo.
 Waziri Magufuli akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Chato Mwalimu Mahendeka Mafele kuhusu Ujenzi wa vyoo unaoendelea.
 Baadhi ya wazazi waliohudhuria katika mahafali hayo ya kumi ya kidato cha Sita shuleni hapo.
 Vijana wanaotarajiwa kuhitimu kidato cha sita katika shule hiyo wakitoa burudani pamoja na Mwenyekiti wa bodi ya Shule hiyo Bi Helena Busumilo.
 Waziri Magufuli akifanya ukaguzi wa mabweni shuleni hapo. P
 Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Chato Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Mwanafunzi bora wa Shule ya Sekondari Magufuli Emanuel Sina Cheti cha Usafi na Utunzaji wa Mazingira kwenye mahafali ya nne ya shule hiyo.
 Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Chato Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wanafunzi pamoja na wazazi kwenye mahafali hayo ya nne katika Shule ya Sekondari  Magufuli.
 Wanafunzi wa kidato cha Sita katika shule ya sekondari  Magufuli wakifurahia hotuba iliyokuwa ikitolewa na Mgeni rasmi  Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Chato Dkt. John Pombe Magufuli.
 Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Chato Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wanaotarajia kuhitimu masomo yao ya kidato cha sita katika shule ya Sekondari ya Magufuli iliyopo Bwanga mkoani Geita.
 Wanafunzi wa shule ya Sekondari Magufuli wakionesha umahiri wao wa kucheza ngoma za asili ya kisukuma katika mahafali hayo.
 Mkuu wa shule ya Sekondari Magufuli Mwalimu Abdalah Haji Siseme akimkabidhi risala mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli.
 Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Chato Dkt. John Pombe Magufuli akitoka kukagua kambi ya mkandarasi anayejenga barabara inayopita karibu na shule hiyo. Dkt. Magufuli ameiahidi shule hiyo kuwa pindi mkandarasi atakapomaliza ujenzi wa barabara hiyo atakabidhi majengo hayo kwa shule hiyo ya kidato cha tano na  sita.
Mandhari ya shule ya Sekondari Magufuli. Shule hiyo toka kuanzishwa kwake mwaka 2010 haijawahi kufelisha mwanafunzi hata mmoja.

DKT. MAGUFULI AHIMIZA WAZAZI KUWASIMAMIA VIZURI WATOTO KATIKA ELIMU.

Waziri wa Ujenzi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chato mkoa wa Geita Dkt. John Pombe Magufuli amewahimiza wazazi na walezi kuwasimamia vizuri watoto wao katika masuala ya elimu ili kuwaepusha na matendo maovu katika jamii. 
Dkt. Magufuli alitoa kauli hiyo leo katika mahafali ya 10 ya Kidato cha Sita katika shule ya Sekondari ya Chato mkoani Geita ambapo jumla ya wanafunzi 84 wanatarajiwa kuhitimu. 
“Wazazi mnataikiwa kuhakikisha mnawafatilia watoto wenu katika masomo yao na kuacha tabia ya kutoa uhuru mkubwa ambao hutumika vibaya. Inabidi muwabane sana hata wakichukia leo kesho watakuja kufurahi na kuona faida yake” alisisitiza Waziri Magufuli 
Waziri Magufuli aliwaasa pia wanafunzi wa kidato cha kwanza mpaka cha nne kuhakikisha kuwa wanasoma kwa bidii ili waweze kufaulu kuingia kidato cha tano. 
“Mnatakiwa kuanzia sasa kupanga  mikakati mizuri ya kujisomea kwa muda huu uliobaki na kwa mwaka huu kusiwe na daraja la nne katika matokeo yenu” aligusia Waziri Magufuli 
Kwa upande wa  Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Chato, Bi. Hellen Busumilo amewasisitiza wazazi kusaidiana na walimu katika malezi ya watoto na pindi mtoto anapokosea aadhibiwe kwani kwa kutofanya hivo ni kosa linalopelekea watoto kufanya matendo maovu. 
“Usimamizi wa watoto ni jukumu la wazazi wote, mzazi nyumbani  na mwalimu shuleni ili tuweze kuwasaidia watoto wetu hasa watoto wa kike” alisema Bi Busumilo 
Bi. Busumilo aliongeza kuwa kuna haja ya kuwaelimisha na kuwafundisha watoto mambo mbalimbali yatakayowajega kwasasa na badae. 
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Chato, Mwalimu Mafere Mahendeka amemshukuru Mbunge wa Chato Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhudhuria mahafali hayo ya 10 ya kidato cha Sita katika shule hiyo.
 “Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa michango yako mbalimbali katika shule yetu, mfano  mwaka 1997 ulisaidia shule hii kumilikiwa na Serikali kwa manufaa ya umma, na kwa mwaka 2003 ulifanikiwa kuweka kidato cha tano na sita”, Alisema Mwalimu Mafere. 
Mwalimu Mafere amemhakikishia Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt. John Magufuli kuwa watatumia kiasi cha Shilingi milioni tano alizowapa katika mahafali hayo kwa ajili ya maendeleo ya Shule hiyo na si vinginevyo. 

Shule ya Sekondari ya Chato ina jumla ya wanafunzi 1018 kuanzia kidato cha I-VI. Shule hii imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kidato cha sita, mfano mwaka 2011 ufaulu ulikuwa asilimia 96 na mwaka 2014 ufaulu ulikuwa asilimia 100.
Wakati huo huo, Dkt. Magufuli ameahidi kuwa majengo ya kambi ya mkandarasi katika barabara ya Bwanga-Uyovu yatakabidhiwa kwa shule ya sekondari Magufuli pindi kazi za ujenzi wa barabara hiyo utakapokamilika. 
Ahadi hiyo ilitolewa na Waziri Magufuli katika mahafali ya nne ya kidato cha sita katika shule ya Sekondari Magufuli ambapo jumla ya wanafunzi 48 wanatarajiwa kuhitimu masomo yao mwezi ujao. 
“Sitafurahi kuona wanafunzi wakipata tabu na walimu wakishindwa kufanya kazi zao vizuri kwa kukosa nyumba za kuishi na madarasa ya kufundishia hivyo huyu mkandarasi akikamilisha kazi za ujenzi wa barabara, hizi nyumba 12 zinabaki kuwa mali yenu”, alisema Dkt. Magufuli. 
Aidha, Waziri Magufuli aliwasihi wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuacha kufikiria changamoto zilizopo shuleni hapo kwasababu wenzao waliowatangulia walifanya vizuri licha ya changamoto hizo
 “Pamoja na changamoto zilizopo mnatakiwa msome kwa bidii na muache mambo mengine kwanza ili ikiwezekana wote hapa mfaulu kuingia chuo kikuu na kuendelea kuiletea sifa shule yenu na Wilaya kwa ujumla”, alisisitiza Waziri Magufuli 
Kuhusu suala la umeme ambalo pia ni changamoto shuleni hapo, Dkt. Magufuli amewataka kuwa na subira kwani tayari suala hilo lipo katika mpango wa Umeme vijiji REA ambapo umeme utafika katika tarafa hiyo ya Bwanga hadi eneo la shule ili kupunguza adha wanayoipata wanafunzi hao. 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo amesema kuwa tarafa ya Bwanga ina watoto 81 ambao mpaka sasa hawajaripoti kwenye shule za Sekondari na ametoa hadi tarehe 13 mwezi huu watoto wote wawe wameripoti shuleni hata kama hawana sare za shule. 
“ili kupata wanafunzi wa kuingia kidato cha tano hatuna budi kuwekeza kwenye elimu ya Sekondari hivyo basi nawasihi sana wazazi mpaka muda huo uliopangwa muwe mmewapeleka watoto shuleni baada ya hapo ni msako utafanyika ili wazazi watakao goma tuwachukulie hatua kali za kisheria.”, alisisitiza Mkuu wa Wilaya ya Chato. 
Shule ya Sekondari Magufuli ilizinduliwa tarehe 21/10/2009 na aliyekuwa Waziri wa Elimu katika kipindi hicho Profesa Jumanne Maghembe. Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 140 wa kidato cha tano na cha Sita na imekuwa ikifanya vizuri kati ya shule zenye wanafunzi zaidi ya 30 katika ngazi za Wilaya, Mkoa na Kitaifa.


No comments:

Post a Comment