Saturday, April 25, 2015

Wahitimu kidato cha sita Jangwani waaswa kutumia elimu kama silaha ya ukombozi

Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Dreams Foundation Tausi Likokola akisalimiana na baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa mgeni rasmi katika wa mahafali hayo shuleni Jangwani sekondari iliyopo manispaa ya Ilala Jijini Dare s salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Dreams Foundation Tausi Likokola (wa katikati) na baadhi wa viongozi wa shule wakielekea eneo la mahafali ya kidato cha sita ya shule ya sekondari Jangwani yalifanyika mwishoni mwa wiki ambapo Mkurgenzi huyo alikuwa mgeni rasmi. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Shule ya sekondari Jangwani Geraldine Mwanisenga.
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita mwaka huu wa Shule ya sekondari Jangwani wakielekea eneo la mahafali yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Dreams Foundation Tausi Likokola akitoa hotuba yake wakati wa mahafali ya kidato cha sita shule ya sekondari Jangwani mwishoni mwa wiki na kuwaasa watumie nidhamu bora ambayo itawasaidia kufikia malengo yao waliyojiwekea maishani mwao. Kushoto ni Mkuu wa Shule ya sekondari Jangwani Geraldine Mwanisenga.
Mwanafunzi aliyepata vyeti mbalimbali vya taaluma takribani saba kwa kufanya vizuri katika masomo ya Kemia, Biyolojia, Fizikia, Hesabu, cheti cha kuwa mwanafunzi bora katika masomo, uongozi, uongozi bora pamoja na zawadi Rosemary Mushi akipongezwa na Mgeni Rasmi na Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Dreams Foundation Tausi Likokola na kukabidhiwa vyeti vyake wakati wa mahafali ya kidato cha sita yalifanyika shule ya sekondari Jangwani mwishoni mwa wiki.
. Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita mwaka huu wa Shule ya sekondari Jangwani wakimsikiliza Mgeni Rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Dreams Foundation Tausi Likokola wakati wa mahafali yao shuleni hapo mwishoni mwa wiki.
Baadhi ya burudani zinaoongozwa na wanafunzi. 
Msanii Barnaba Boy akitoa burudani shuleni hapo.
Msanii Msami kutoka THT alivyopamba mahafali ya kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Jangwani jijini Dar.
Kikundi cha wanafunzi wa shule ya sekondari Jangwani wakionesha ukakamavu wao huku mmoja wao alyekuwa juu ya wenzake akimakabidhi MC mic kwa ujasiri.
Baadhi ya walimu na wageni waalikwa wakimfuatilia mambo mbalimbali wakati wa mahafali ya kidato cha sita shule ya sekondari Jangwani yaliyofanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo. (Picha na Eleuteri Mangi).

Na Eleuteri Mangi 

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Jangwani wameaswa kutumia muda wao vema wakiwa shuleni kwa kuwekeza kwenye elimu ambayo inasaidia kumbadilisha mtu na hatimaye kubadilisha jamii nzima. 

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Dreams Foundation Tausi Likokola alipokuwa mgeni rasmi wakati wa mahafali ya wanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari Jangwani iliyopo manispaa ya Ilala Jijini Dare s salaam.

“Ukizaliwa mwanamke, tambua kuwa wewe ni kiongozi wa kwanza katika jamii, hivyo tumia vipaji vyako kama ulivyojaliwa na Mwenyezi Mungu ukizingatia suala la nidhamu ambayo ndiyo msingi wa mafanikio yote yatakayowasaidia katika maisha yenu ndani ya jamii” alisema Tausi.

Tausi alisisitiza kuwa watu wengi duniani wanaofanikiwa wanaongozwa na nidhamu bora waliyonayo ambayo imewasaidia kufikia malengo yao waliyojiwekea, wanafunzi hao wametakiwa kuiga mfano huo ili waweze kufanikiwa maisha yao kwa manufaa yao binafsi, jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya sekondari Jangwani Geraldine Mwanisenga alipokuwa akitoa taarifa fupi ya shule kwa mgeni rasmi wakati wa mahafali hayo alisema kuwa shule yake ni miongoni mwa shule kongwe nchini ambazo zinazofanya vizuri kitaaluma na masuala mengine yasiyo ya kitaaluma.

Kuhusu taaluma, Mkuu huyo alisema kuwa shule yake imeendelea kufanya vizuri na kushika nafasi ya juu katika matokeo ya mitihani ya taifa ambapo mwaka huu imeshika nafasi ya kwanza kwenye matokeo ya kidato cha nne miongoni mwa shule za sekondari za serikali katika Mkoa wa Dar es salaam. 

Mkuu huyo wa shule alisema kuwa siri kubwa ya mafanikio yao inatokana na kujiweka malengo, mikakati na kuhakikisha vyote inatekelezwa kwa wakati.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kufundisha masomo ya ziada na rekebishi, kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo, ushirikiano baina ya Bodi ya shule, wazazi, wafanyakazi wanafunzi na wadau wengine wa elimu ikiwa ni chachu ya mafanikio ya shule.

Aidha, Mkuu wa shule mwalimu Geraldine amewaasa wahitimu hao watumie elimu waliyoipata wakiwa shuleni hapo kama silaha ya ukombozi kwenye jamii, maana jamii inahitaji wasomi ili kuikomboa kifikra, kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Naye mwanafunzi aliyepata vyeti mbalimbali vya taaluma takribani saba kwa kufanya vizuri katika masomo ya Kemia, Biyolojia, Fizikia, Hesabu, cheti cha kuwa mwanafunzi bora katika masomo, uongozi, uongozi bora  pamoja na zawadi Rosemary Mushi  alibainisha kuwa ilikuwa ndoto yake kuja kuwa mwanafunzi bora maana alipokuwa kidato cha nne zawadi hiyo ilienda kwa mwanafunzi mwingine ambapo hatua hiyo ilimpa hamasa ya kusimamia azma yake kwa moyo wote.

“Leo ninafuraha sana maana ilikuwa ndoto yangu kuja kuchukua vyeti vyote ambapo ilinilazimu kusoma sana na kufaulu vizuri ili nifikie ndoto yangu ya maisha ya kuwa daktari wa watoto” alisema Rosemary.

Rosemary aliushukuru uongozi wa shule, walimu, wafanyakazi wasio walimu na wanafunzi wenzake kwa ushirikiano mzuri alioupta kutoka kwao wakati wote alipohitaji masaada wao ili kufikia malengo yake ya kufaulu vizuri masomo yake na kumuwezesha kusonga mbele katika hatua nyingine ya elimu.


Shule ya sekondari Jangwani ilinzishwa kwa historia ya kuwekwa jiwe la msingi liliwekwa mnamo Mei 28, mwaka 1928 na Kiongozi Mkuu wa ukoloni wa Mwingereza wakati huo Sir Donald Cameroon na kuifanya shule hiyo kuwa na umri wa miaka 87 ambapo kwa sasa ina jumla ya walimu 102, wafanyakazi wasi walimu 21, wanafunzi 1150 miongoni mwao wanafunzi 70 ni wenye mahitaji maalum kulingana na mahitaji ya sera ya elimu chini ya mataala wa elimu jumuishi uliohimiza kusomesha wanafunzi wenye mahitaji maalum.  

No comments:

Post a Comment