Tuesday, April 14, 2015

Umuhimu wa kudhibiti matumizi ya vyombo vya elektroniki kwa watoto na vijana


Zaidi ya asilimia 60 ya watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 17 wanatumia zaidi ya masaa mawili kila siku kuangalia mitandao ya kijamii pamoja na vipindi mbalimbali vya Televisheni. Hii inaweza kuwa njia kubwa ya kuunganisha, lakini pia kuna hatari zinazohusiana na kutumia muda mwingi sana kwenye vyombo vya habari kijamii.

Leo hii ni nadra kukuta familia ambazo watoto na vijana wake hawajaathirika na vyombo vya habari na elektroniki kama vile televisheni, intaneti na michezo mingine tofauti ya kompyuta.
Hata hivyo utumiaji mkubwa na wa masaa mengi wa vyombo hivyo hauwahusu watoto na vijana tu, bali watu wazima pia wameathirika na jambo hilo.

 Kutokana na sababu kadhaa za kimwili, kisaikolojia na kiroho, kuna udharura kwa watoto kusimamiwa vyema na wazazi, mashirika na taasisi za kielimu na kiutamaduni na kadhalika vyombo vya habari ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi mabaya ya vyombo hivyo vya elektroniki. Licha ya kompyuta kuwa na pande chanya tofauti za kimaendeleo, hasa katika nyanja za kielimu na huduma za mawasiliano, lakini chombo hicho pia kina nafasi hasi kwa watoto na hata kwa watu wazima. 

Utumiwaji usio na udhibiti wa chombo hicho na kadhalika vyombo vingine vya elektroniki kama vile televisheni, unaweza kuyaweka hatarini maisha ya watoto kutokana na athari zake mbaya kwa ustawi wa kiroho, kisaikolojia na kijamii wa watoto hao.

Harakati zetu za kifizikia na miamala yetu tofauti ya kijamii, ni umuhimu yenye taathira kubwa kwa afya na tabia za mtoto. Kinyume chake, ikiwa mtoto atatumia muda wake mwingi katika matumizi ya michezo ya kompyuta, basi hawezi kunufaika na upande chanya wa kujenga akili yake wala harakati bora kwa ajili ya kuufikia ukamilifu wake kijamii. 

Mbali na hayo, watoto pia wanaweza kukabiliwa na hatari ya kutekeleza vitendo vya ukatili na visivyo vya kikatili hata katika umri wao mdogo. Hali hiyo ambayo inaweza kufikiwa ghafla au hata kwa makusudi, huwaletea watoto na vijana madhara yasiyoweza kufidika hasa kuhusiana na masuala ya kiafya, kisaikolojia sambamba na kueneza kwa kiasi kikubwa matatizo ya kimwili na kiakili kama vile utovu wa maadili, vitendo vya ukatili, madawa ya kulevya, tabia mbaya katika jamii, kuzorota thamani za familia na kuenea jinai na uhalifu wa kila aina katika jamii.

Ukweli ni kwamba, wazazi hawajawachwa peke yao katika jukumu la kutoa malezi bora kwa watoto wao, bali wataalamu wa mambo wamefanya utafiti wa kina katika uwanja huo na kuwasaidia katika suala hilo kwa kuwasilisha njia bora za malezi ambazo zinawavutia watoto na kuwafanya waishi maisha bora katika jamii. 

Watafiti hao wanasema kuwa, licha ya kwamba haiwezekani kuwatenga watoto na ulimwengu wa michezo ya kompyuta lakini tunaweza kuwaepusha na madhara ya michezo hiyo kwa kutumia njia na mbinu zinazofaa.
Udhibiti fulani wa matumizi ya kompyuta kila siku au kwa wiki, ni moja ya njia hizo. Kwa mbinu hiyo, mtoto anaweza kutumia chombo hicho kwa muda na kiwango kilichoainishwa na kila pale anapokwenda kinyume na kiwango hicho, basi anapasa kuzuiwa na kuadhibiwa. 

Hata hivyo utumiaji mabavu na nguvu hauna nafasi katika hapa. Katika kesi kama hiyo njia ya mazungumzo sanjari na kumzuia kwa muda, kutumia vitu anavyovipenda mtoto huyo, inafaa kutumiwa hapa.

Wakati mwingine mtoto hutumia vyema kompyuta kwa kujinufaisha kielimu na chombo hicho muhimu cha teknolojia na kwa kweli katika hali kama hii wazazi hawapaswi kumzuia mtoto kutumia chombo hicho cha kompyuta. Lakini jambo linalopaswa kuzuiwa ni tabia ya mtoto huyo kutumia wakati wake mwingi katika kichezo isiyofaa ya kompyuta.

Moja ya nyenzo zingine za udhibiti ambazo zinaweza kutumiwa na wazazi katika kusimamia mienendo ya mtoto, ni uwezekano wa kutumia mbinu zinazodhibiti mfumo wa kompyuta. Kwa utaratibu huo watoto hawawezi kuingiza program mpya au kuweka windozi tofauti ambazo ni rahisi kuweza kuwaharibu watoto.

Njia nyingine ni pamoja na kuzuia kuondolewa program zilizopo katika kompyuta au kuzizuia zisifanye kazi, ni moja ya njia ambazo zinaweza kutumiwa katika kuwadhibiti watoto. 

Miongoni mwa njia nyepesi zaidi kwa wazazi katika kumlinda mtoto wao wakati wa kutumia njia na nyenzo zinazohusiana na ulimwengu wa intaneti, ni kuweka mfumo wa kompyuta nje ya chumba chake cha kulala. Njia hiyo itawasaidia wazazi wakati wa kutumia mtoto chombo hicho nao waweze kushuhudia na kufuatilia kwa karibu michezo na shughuliza zote za mtoto huyo anapotumia kompyuta.

Kwa hakika vivutio vya kompyuta na michezo mingine ya kielektroniki kwa watoto havina kikomo, na ikiwa hakutakuwepo usimamizi madhubuti wa wazazi kwa mtoto wao, basi huenda mtoto bila kujijua, akatumia wakati mwingi zaidi kuliko inavyotakiwa na hivyo kuathiri lishe, usingizi na hata masomo yake.

 Hapo ndipo wazazi wanapotakiwa kuwa macho na kuhakikisha wanasimamia vyema malezi ya mtoto wao sanjari na kumuandalia ratiba nzuri ya maisha yake na kuchunga sheria watakazomuainishia kila wiki.
Aidha wazazi wanatakiwa kumuweka mbali mtoto wao na ulimwengu wa elektroniki na michezo ya kompyuta wakati wa kipindi cha masomo. 

Watafiti wanasema kuwa,  kuna ulazima mkubwa wa kuzingatiwa wakati wa matumizi ya watoto kwa vyombo vya umeme kama vile kompyuta, labtop na tablet na kile ambacho kinahusiana na ulimwengu wa kielektroniki, kwani utafiti unaonyesha kwamba matumizi mengi ya vyombo hivyo kupita kiasi na kufikia kiwango cha uraibu, hupunguza uwezo wa kifikra wa mtoto.

 Na kukithiri kwa  maradhi hayo kwa watoto ndio mwanzo wa kufeli katika hatua zao za kielimu sanjari na kushindwa kukabiliana na mikikimikiki mingine ya kimaisha ambayo anapaswa kukabiliana nayo katika mustakbali wa maisha yake ya mbeleni.

 Katika matumizi ya michezo ya kompyuta au ulimwengu wa intaneti, kuna udharura wa kujitenga na mambo machafu yasiyofaa. Aidha inaelezwa kuwa, kutumia sana kompyuta na intaneti, taratibu huibua tatizo la unene, ambalo mara nyingi hupelekea watoto na hasa vijana wengi kujichukia wenyewe kutokana na tatizo hilo. Hivyo kuna haja kwa wazazi kuwaepusha watoto wao na unene na uzembe unaosababishwa na matumizi ya muda mrefu ya vyombo vya umeme hasa michezo ya kompyuta.

Wataalamu wengi wanaamini kuwa, ni muhimu kuwatenga watoto walio na umri wa chini ya miaka mitatu na aina yoyote ya matumizi ya kompyuta. Kwa maana nyingine ni kwamba, umri huo hauoani na matumizi ya kompyuta au video.

 Hata hivyo ikiwa mtoto aliye na umri wa chini ya miaka mitano ataingia katika ulimwengu wa matumizi ya vyombo hivyo na kuvizoea, basi lazima awekewe sheria na vidhibiti maalumu vya kumuwezesha kukabiliana na hatari ya ulimwengu huo. Kwanza anapasa kufahamishwa ni kwa kipindi gani anatakiwa atumie vyombo hivyo na kisha baada ya hapo ajishughulishe na kazi nyingine.

Watafiti wanapendekeza kuwa, mtoto mwenye umri wa kuinukia anatakiwa atazame kwa saa moja au masaa mawili filamu na katuni, upekuzi katika intaneti na michezo mingine ya video katika kompyuta. Ikiwa mtoto kwa siku atatumia dakika 45 kucheza mchezo wa kompyuta na muda mwingine mdogo kutazama televisheni na mwingine mfupi kujishughulisha na harakati za kifizikia, basi hakutakuwepo na wasi wasi wa kuathirika afya yake. Lakini ikiwa atatumia masaa mengi kujishughulisha na michezo ya kompyuta zaidi ya kiwango kinachotakiwa, basi hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na hali hiyo.

Madaktari wanashauri kwamba, watoto wanatakiwa kutumia masaa mawili tu kwa siku kutazama televisheni. Televisheni ina athari nyingi muhimu kwa watoto wengi wanaosoma na hasa katika kupumzisha mwili na fikra zao.
Hivyo wazazi na walimu wanatakiwa kusimamia ni kiasi gani watoto wanapaswa kutazama televisheni. Hii ni katika hali ambayo katika miaka ya awali watoto wanaosoma shule za msingi, huwa hawana uwezo wa kupanga vyema ratiba za kutazama televisheni.

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari na Afisa Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo anapatikana kwa barua pepe; sawebenjamin@gmail.com.

No comments:

Post a Comment