Friday, April 3, 2015

MADEREVA WAFUNDWA NA TANROADS KUHUSU MZANI WA KISASA WA VIGWAZA

Eng. Japhet Kivuyo kutoka kitengo cha mzani wa Vigwaza mkoani Pwani akifafanua jambo kwa waandishi wa habari waliotembelea mzani huo jana jijini Dar es salaam.
Taa ya mzani wa Vigwaza ikielekeza gari lililobeba mzigo mzito kupinda kushoto kwa ajili ya ukaguzi wa kina. Changamoto kubwa iliyopo madereva hawafati taratibu za taa na wengine hawazielewi.
Kamera zilizounganishwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) eneo la mzani wa Vigwaza zikirekodi matukio mbalimbali yanayotokea katika eneo hilo ili kutambua magari yanayotii na kuvunja sheria.
Meneja wa Wakala wa Barabara mkoani Pwani Eng. Tumaini Sarakikya akielezea ufanisi wa mzani wa vigwaza kwa waandishi wa habari (pichani) ambao unapunguza foleni pamoja na rushwa kwa watumiaji wa mzani huo.
Msimamizi wa Mzani wa Vigwaza, Godo Biwi akionesha jinsi mzani huo unavyofanya kazi kwa njia ya teknolojia kwa uwazi na uharaka.
Baadhi ya magari yaliyozidisha uzito yakiwa yameegeshwa ndani ya mzani wa Vigwaza mkoani Pwani, ambapo gari litakaloegeshwa kwa kushindwa kulipa fidia baada ya siku tatu litalipa faini ya dola 20 kwa siku ambazo zitabadilishwa kwa fedha za kitanzania.
Gari lenye mtambo wa kukagua madaraja makubwa linalomilikiwa na Wakala wa Barabara mkoani Pwani kwa ajili ya kupima umadhubuti wa madaraja na kuona ubora na mapungufu yake.


Imeelezwa kuwa ufanisi wa kutumia mzani wa kisasa wa Vigwaza utafikiwa endapo madereva na watumiaji wa barabara watajielimisha taratibu za kutumia mizani hiyo ili kwenda na kasi ya upimaji, kuokoa muda na kuondoa msongamano katika barabara kuu ya Chalinze-Kibaha.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa wa Pwani Eng. Tumaini Sarakikya, wakati akikagua namna mzani huo unavyofanyakazi na kusisitiza umuhimu wa madereva kufuata maelekezo ya alama za barabarani katika eneo hilo ili kujiepusha na uvunjaji wa sheria.

“Mzani huu una urefu wa mita 22 hivyo utasaidia kuondoa msongamano eneo hili kwani unauwezo wa kupima gari lote mara moja na kwa dakika moja tofauti na mizani nyingine zinazopima gari kwa awamu ambazo hutumia dakika 3”, amesisitiza Eng. Sarrakikya.

Eng. Sarakikya amesema  teknolojia inayotumika katika mzani huo itasaidia kuepuka majadiliano yanayoweza kuleta hisia za  rushwa na upendeleo ambavyo ni changamoto katika utendaji kazi wa mizani hapa nchini. 

Akizungumzia utendaji kazi wa mzani huo Eng. Japhet Kivuyo, amesema takriban magari 1800 hupimwa katika mizani ya awali (weigh in motion sensor) ambapo asilimia 60 ya magari hayo hupimwa katika mizani kuu na asilimia 40 huruhusiwa kupita bila kupimwa baada ya kuonekana yamekidhi vigezo.

Naye Mkuu wa mzani wa Vigwaza Eng. Simfukwe Sylvester, amezungumzia umuhimu wa wasafirishaji kupanga vizuri na kubeba mizigo inayowiana na magari yao ili kuepusha usumbufu na uharibifu wa barabara.

Amesema gari litakalokaidi kupima katika mzani huo litaadhibiwa kwa kulipa faini ya dola za kimarekani elfu 2, na pia gari litakaloegeshwa kwa kushindwa kulipa fidia baada ya siku tatu litalipa faini ya dola 20 kwa siku ambazo zitabadilishwa kwa fedha za kitanzania. 

Katika hatua nyingine Eng. Sarakikya amesema ujenzi wa barabara kati ya Mlandizi -Vigwaza na Vigwaza –Chalinze utaanza hivi karibuni baada ya wakandarasi wa kujenga eneo hilo kupatikana. 


IMETAYARISHWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI, WIZARA YA UJENZI.

No comments:

Post a Comment