Wednesday, April 1, 2015

Kadiri muda wa kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa unavyowadia, wananchi hawajaamua “ndiyo” au “hapana”


Wakati kura ya maoni inakaribia, wananchi wamejigawa katikati. Zaidi ya nusu yao (asilimia 52) wanasema wataunga mkono Katiba Inayopendekezwa. Lakini mwananchi mmoja kati ya wanne (asilimia 26), sawa na nusu ya wanao tayarajia kuiunga mkono katiba, wanasema wataipinga. Mwananchi mmoja kati ya watano (asilimia 22) bado hajamua. 

Mnamo mwaka 2014, wakati rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) inajadiliwa, wananchi wengi (asilimia 65) walisema wangepiga kura kuikubali rasimu hiyo, na wananchi wachache (asilimia 21) walisema wangeipinga. Ingawa takwimu zinaonyesha kuwa Katiba Inayopendekezwa ingepitishwa na wananchi wa Tanzania Bara, tofauti kati ya makundi haya imezidi kuwa finyu. 

Maoni ya wananchi yanaonyesha wazi mashaka yaliyopo katika mchakato mzima wa kuibadili katiba. Mwezi mmoja tu kabla ya siku ya kupiga kura, uandikishaji wa wapiga kura bado haujakamilika. Nusu ya wananchi (asilimia 47) wanafikiri kuwa uchaguzi mkuu ujao utafanyika chini ya katiba mpya, lakini idadi ndogo (asilimia 30) inafikiri kuwa uchaguzi huo utafanyika chini ya katiba ya sasa. 

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wenye jina la: Kuelekea Kura ya Maoni | Maoni ya Watanzania kuhusu Katiba Inayopendekezwa. Muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi (www.twaweza.org/sauti). Muhtasari huu unajumuisha maoni ya wananchi wa Tanzania Bara (Zanzibar haikuhusishwa katika utafiti huu) juu ya Katiba Inayopendekezwa. Takwimu hizi zinatokana na duru la 29 ya Sauti za Wananchi. Jumla ya wahojiwa 1,399 walipigiwa simu kati ya Januari 27 na Februari 17, 2015. Matokeo mengine yanatokana na duru la 5 la Sauti za Wananchi, (iliyowahoji watu 1,708 kati ya Julai 16 na Julai 30, 2013) na duru la 14 la Sauti za Wananchi (iliyowahoji watu 1,550 kati ya Februari 12 na Machi 4, 2014). Takwimu hizi zimetumika kufuatilia mwenendo wa muda mrefu. Ni muhimu kukumbuka kuwa mahojiano haya yalihusisha makundi yote ya wananchi wa Tanzania Bara. 

Tofauti kati ya “ndiyo”’ na “hapana” ulipungua kati ya mwezi Machi 2014 na Februari 2015, kipindi kilichoainisha mabadiliko mengi katika mchakato mzima wa kubadili katiba. Mabadiliko haya yaliyotokea kati ya rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na rasimu ya Katiba Inayopendekezwa  yanaleta wasiwasi baina ya wananchi. Wananchi wanne kati ya kumi (asilimia 39) wameonesha kuipendelea Katiba Inayopendekezwa. Idadi iliyo ni sawa na ile (asilimi 41) ya wanaoipendelea rasimu ya pili ya katiba. 

Hata hivyo, kuna tofauti kubwa kati ya rasimu hizi mbili. Wananchi walipohojiwa kuhusu vifungu maalumu, majibu yao yalikuwa ya uwazi zaidi. Wananchi nane kati ya kumi (asilimia 80) hawakubaliani na kuondolewa kwa kifungu cha kuwawajibisha wabunge wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao. Idadi inayokaribia hiyo Asilimia 78 ya wananchi hawakubaliani na kuondolewa kwa kifungu cha uwazi na uwajibikaji kwenye orodha ya tunu za taifa. Wananchi saba kati ya kumi (asilimia 70) hawakubaliani na kufutwa kwa kifungu cha ukomo (miaka 15) wa mbunge kushika ofisi. Kwa upande mwingine, wananchi wachache (silimia 36) hawakubaliani na kubadili muundo wa Muungano kutoka serikali 3 kubakia kuwa wa serikali 2. 

Je, wananchi wanakubaliana na UKAWA kususia vikao vya Bunge la Katiba na ushawishi wake kwa wananchi kususia kura ya maoni? Kati ya wananchi waliosikia minong’ono juu ya UKAWA kususia vikao vya Bunge la Katiba, asilimia 66 wanapinga hatua hiyo. Asilimia 68 wanapinga ushawishi kwa wananchi kususia kura ya maoni na robo tatu (asilimia 75) ya wananchi wanasema hawatasusia kura ya maoni. 

Elvis Mushi, Mratibu wa Sauti za Wananchi alitoa maoni yake kuhusu matokeo haya nakusema “Mashaka yaliyopo juu ya kukamilika kwa mchakato wa mabadiliko ya katiba na kubadilika kwa mwenendo wa mchakato huo kumesababisha mashaka kwa wananchi. Hali hii ndio inayosababisha maoni ya wananchi kugawanyika katikati kuhusiana na maswala yote muhimu”

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, akaongeza “Kuna mambo matatu yanayojitokeza kutokana na maoni haya ya wananchi. Jambo la kwanza ni kwamba kura ya “ndiyo” kwa Katiba Iliyopendekezwa haina uhakika. Tofauti iliyopo ni finyu na wananchi wameonesha kwamba kura hii inaweza kubadilika wakati wote katika mchakato huu. Pili, kuna kilio kilicho wazi kuhusu umuhimu wa katiba kusisitiza maswala ya uwazi na uwajibikaji. Wananchi wameunga mkono kwa nguvu zote vifungu vinavyoimarisha uwajibikaji. Changamoto kubwa zilizopo katika upatikanaji wa huduma za kijamii na kuwepo kwa tatizo kubwa la rushwa vyote vimekuwa na athari kubwa na wananchi wanatafuta njia za kuwawajibisha viongozi kwa matendo yao. 


Tatu, wananchi hawajashawishika kuchukua hatua za nguvu za kuleta mabadiliko. Wito wa UKAWA wa kususia kura ya maoni haujawavutia na wananchi wengi hawauungi mkono. Mambo haya matatu yatakuwa changamoto kubwa kwa viongozi wa ngazi zote kuamini  kwamba mawazo yao yanawakilisha maoni ya wananchi.”

No comments:

Post a Comment