Tuesday, April 7, 2015

Balozi Seif Idd azungumza na Viongozi wa Mkoa wa Magharibi, Zanzibar

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika mkutano wa ujirani mwema kati ya Kata ya Mtoni Wilaya ya Temeka na Wilaya ya Dimani hapo Tawi la CCM Kwerekwe B.
Mkuu wa Msafara wa Ujumbe wa Kata ya Mtoni Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es salaam Nd.Said Kabuma akitoa shukrani kwa mapokezi mazuri waliyopewa na wenyeji wao Wilaya ya Dimani wakati wa kuagana baada ya kumaliza ziara yao ya ujirani mwema Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi na wanachama wa ujirani mwema kati ya Kata ta Mtoni Wilaya ya Temeka mkoa wa Dar es salaam na Wilaya ya Dimani Mkoa wa Magharibi Zanzibar.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtoni ambae pia ni Katibu Mwenezi wa Kata hiyo Wilaya ya bTemeke Mkoa wa Dar es salaam Ndugu Hija Makamba akielezea mafanikio yanayopatikana kutoka na ujirani mwema kati ya pande hizo mbili.
Balozi Seiuf akimfariji na kumpa Pole Bibi Khadija Said Hassan wa Kata ya Mtoni Wilaya ya Temeke ambaye alipata ajali ya kugongwa na vespa wakati wa ziara yake ya ujirani mwema Zanzibar. Picha na –OMPR – ZNZ.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM  Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Watanzania Bara na Zanzibar wataendelea kushirikiana kwa karne kadhaa zijazo kutokana na muingiliano wao wa  kidamu uliopo kati ya pande hizo mbili.

Alisema uwepo wa ushirikiano huo ndio njia pekee itakayotowa fursa kwa Watanzania hao kusaidiana katika kutatua changamoto zinazojichomoza miongoni mwao na vizazi vyao.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa ujirani mwema kati ya Wanachama na Viongozi wa Mkoa wa Magharibi na wageni wao kutoka  Kata ya Mtoni Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es salaam.

Mkutano huo uliofanyika katika Tawi la Chama cha Mapinduzi Kwerekwe “B” unafuatia ziara za ujirani mwema kati ya pande hizo mbili zinazofanyika mwanzoni mwa  mwezi wa Aprili  ya kila mwaka kutegemea upande unaokuwa mwenyeji wa ugeni huo.

Balozi Seif alisema hakuna kikundi wala mtu anayeweza kuung’oa Muungano uliopo wa Tanganyika na Zanzibar kutokana na historia yake kwa jinsi ulivyoimarika  kwa miaka kadhaa iliyopita.

Amewataka na kuwaomba Watanzania wote kuiunga mkono Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba kwa vile inakidhi  mahitaji na haki za makundi yote yaliyopo hapa Nchini.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Katiba iliyopendekezwa yenye muundo wa mfumo wa Serikali mbili ndio itakayolivua Taifa la Tanzania kuendelea kudumu kwa zaidi ya miaka mengine hamsini ijayo.

Akizungumzia suala la Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwataka Wanachama wa CCM Kuheshimu maamuzi ya Vikao vya Chama chao wakati vinapofanya kazi ya kuteuwa wagombea wao.

Alisema ni vyema kwa wanachama hao kukubali maamuzi yanayotolewa na chama chao kwa kuwaunga mkono wagombea waliopendekezwa katika ngazi zote kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu ujao.

Akisoma risala Katibu wa Kamati ya ujirani mwema Ndugu Muhidini Makame Ussi alisema ujirani mwema kati ya Kata ya Mtoni Wilaya ya Temeke na Wilaya ya Dimani umeanza tokea mwaka 1995.

Nd. Muhidini alisema ujirani mwema huo unaojumuisha Viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa pande hizo mbili umeanzishwa kwa lengo la kuimarisha ujirani mwema sambamba na kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964.

Mapema Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtoni ambae pia ni Katibu Mwenezi wa Kata hiyo Ndugu Hija Makamba alisema Viongozi na Wanachama wa CCM wa pande hizo mbili tayari wamekuwa na utaratibu wa kutembeleana hata katika siku za kawaida kwa takriban miaka 20  sasa.

Ndugu Hija alieleza kwamba ziara hizo zimekuwa zikitoa nafasi kwa wanachama na Viongozi wa pande hizo mbili za Wilaya ya Dimani na Wilaya ya Temeke kubadilishana mawazo ya Kisiasa na hata yale ya Kiutamaduni.

No comments:

Post a Comment