Thursday, March 26, 2015

SUDAN KUSINI WAFANAYA ZIARA YA MAFUNZO YA KUBADILISHANA UZOEFU NA WATENDAJI WA SEKTA YA UJENZI NCHINI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga (wa kwanza kulia), akizungumza na viongozi wa ujumbe wa Serikali ya Sudan Kusini waliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es salaam jana.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga, akizungumza katika kikao cha mafunzo ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na viongozi wa Sudan Kusini. (wa pili kushoto) ni Mkurugenzi wa Barabara wa Wizara ya Ujenzi Eng. Venny Ndaymukama, anayemfuatia ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Barabara za Mkoa Eng. Laurent Kyombo.
Naibu Waziri wa Usafirishaji, Barabara na Madaraja wa Sudan Kusini Mh. Simon Mijok, akitoa salamu za Serikali yake kwa viongozi wa Wizara ya ujenzi, kutokana na ziara ya mafunzo ya siku tatu inayoendelea hapa nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) Dr. James Wanyancha, akimkabidhi zawadi Naibu Waziri wa Usafirishaji, Barabara na Madaraja wa Sudan Kusini Mhe. Simon Mijok alipotembelea ofisi za Mfuko wa Barabara kwa ajili ya mafunzo ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya ujenzi wa miundombinu ya barabara jijini Dar es salaam.
Ujumbe wa Sudan Kusini katika picha ya pamoja na viongozi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) walipoitembelea Bodi hiyo jana kujifunza inavyofanyakazi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga amezungumzia umuhimu wa Tanzania kuimarisha uhusiano wake na Sudani Kusini na kueleza kuwa hatua hiyo itawezesha nchi hiyo kuwa na amani na  kupiga hatua za haraka za maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza mara baada ya kupokea ujumbe wa Serikali ya Sudan Kusini ulioitembelea Wizara ya Ujenzi kujifunza namna bora ya kuendesha Wizara inayoshughulikia usafirishaji,ujenzi wa barabara na madaraja Eng. Nyamhanga amesema kuwepo na mipango endelevu,wataalam wa ndani na uhusiano mwema baina ya nchi na nchi ni kigezo muhimu cha kuleta maendeleo katika sekta ya miundombinu.

“Tumieni uzoefu wa Tanzania kuanzisha taasisi zinazosimamia sekta ya ujenzi na usafirishaji na kuongeza idadi ya wahandisi na makandarasi ili kujenga miundombinu mipya na kuiendeleza iliyokwishajengwa”, amesisitiza Eng. Nyamhanga.
Amezungumzia umuhimu wa Serikali ya Sudan Kusini kuwa na mfuko wa ukarabati na ujenzi wa barabara,kuwa na taasisi zinazosimamia makandarasi,wahandisi na wasanifu majengo na wakadiriaji majenzi ili kuimarisha sekta ya ujenzi nchini humo.

Akitoa mada kuhusu hatua za haraka za kuchukua ili kufikia malengo ya maendeleo Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Barabara za Mikoa Eng. Laurent Kyombo, amesema Sudan Kusini itapata maendeleo ya haraka kama itaimarisha taasisi zinazohusika na sekta ya ujenzi na  kujifunza kwa nchi jirani ambazo zimepiga hatua kubwa katika ujenzi wa barabara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo Naibu Waziri wa Usafirishaji,Barabara na Madaraja wa Sudan Kusini Mhe. Simon Mijok, ameishukuru Tanzania kwa jitihada zake kwa nchi hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo diplomasia na ujenzi huku akisisitiza kwamba watatumia ziara yao ya mafunzo kuanzisha taasisi za ujenzi zenye sura ya Tanzania ili kuharakisha maendeleo ya nchi hiyo.

“Tangu enzi za baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania imekuwa kimbilio la raia wa Sudan Kusini na baadhi yao wamepata elimu hapa nchini , hivyo naiomba Tanzania iendelee kuilea nchi yetu changa iliyopata uhuru wake hivi karibuni  baada ya mapambano ya muda mrefu ya kudai uhuru”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Nchini (RFB), Dkt. James Wanyancha ameueleza ujumbe huo umuhimu wa kuwa na mfuko maalum wa barabara utakaowezesha kuendeleza na kukarabati barabara zilizojengwa ili zitumike wakati wote.

“Hakikisheni fedha zitakazotengwa kwaajili ya miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja zinatumika kwa kazi hizo; hii itasaidia barabara zilizojengwa kufanyiwa ukarabati na kuziendeleza ziwiane na mahitaji ya eneo husika”, amesisitiza Dkt. Wanyancha. 

Ziara hiyo ya mafunzo ya siku tatu ambayo imedhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA)upande wa Sudan Kusini na Tanzania, inajumuisha ujumbe wa viongozi 15 waandamizi wakiwemo wa Wizara ya Usafirishaji,Barabara na Madaraja, Wizara ya Mazingira na Wajumbe wa Bodi wa Mamlaka ya Barabara ya Sudan Kusini (SSRA).

Ukiwa hapa nchini, ujumbe huo utapata fursa ya kutembelea taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na kuona zinavyofanya kazi ya utekelezaji wa  miradi ya ujenzi hapa nchini.


Pia utatembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo-Msata,Ruvu chini na kituo cha mizani cha Vigwaza wilayani Bagamoyo mkoani pwani.

No comments:

Post a Comment