Sunday, March 1, 2015

SERIKALI YA JAMHURI YA KOREA YAKUBALI KUTOA FEDHA KWA AJILI YA UJENZI WA DARAJA JIPYA LA SALENDER

Muonekano wa Daraja jipya la Salenda litaakalopita baharini kuanzia Coco Beachi (Oysterbay) kwenda Hospitali ya Aga Khan (Maeneo ya Ocean Road/ Baraka Obama Road). Daraja hilo pamoja na barabara zake, litakuwa na urefu wa kilomita 7.2 na uwezo wa kupitisha magari zaidi ya 61,000 kwa siku huku likiwa na njia nne za magari pamoja service road njia za waenda kwa miguu kila upande
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kulia akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Chung Il wapili kushoto kuhusiana na mambo mbalimbali kuhusu sekta ya Ujenzi pamoja na mchakato wa Ujenzi wa Daraja jipya la Salenda litakalopita baharini. Wa kwanza kushoto ni mke wa Balozi huyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe kushoto akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Korea Chung Il kulia. Katikati ni Eng. Consolata Ngimbwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi nchini (CRB).
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kushoto akimkabidhi zawadi Balozi wa Jamhuri ya Korea, Chung Il mara baada ya hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Balozi huyo kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Patrick Mfugale akikaribishwa na Mke wa Balozi wa Jamhuri ya Korea. Kulia ni Balozi huyo Chung Il.
Mkurugenzi wa Miradi wa TANROADS Eng. Victor Seff akisalimiana na Mke wa Balozi.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisaini kitabu cha wageni nyumbani kwa Balozi wa Jamhuri ya Korea, Masaki jijini Dar es Salaam.

Serikali ya Jamhuri ya Korea ya Kusini hatimae imekubali kutoa fedha kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Daraja jipya la kisasa la Salender. Daraja hili litakuwa mbadala wa daraja la Zamani la Salender.

Serikali hiyo imekubali kutoa mkopo wa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Daraja hilo jipya na la kisasa kabisa litakalopita baharini pembezoni mwa Daraja la zamani la Salender kuanzia Coco Beachi (Oysterbay) kwenda Hospitali ya Aga Khan (Maeneo ya Ocean Road/ Baraka Obama Road).

Kauli hiyo ilitolewa na Balozi wa Jamhuri ya Korea ya Kusini nchini Ndugu Chung Il wakati alipomwalika Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Ujumbe wake katika chakula cha jioni nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam

Akizungumza katika hafla hiyo ya chakula cha jioni, Balozi wa Jamhuri ya Korea ndugu Chung Il alisema kuwa fedha hizo za mkopo wa masharti nafuu zitatolewa kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yake na Tanzania.

“Naomba tuendelee kudumisha uhusiano wetu hapa Tanzania pamoja na Korea ya Kusini na ndio maana kuna wananchi zaidi ya 500 kutoka Korea ya Kusini wanaoishi hapa Tanzania” alisema Balozi huyo wa Jamhuri ya Korea ya Kusini.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea ya Kusini kwa kuridhia kutoa fedha hizo kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Daraja hilo la kihistoria nchini.

“Naishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Korea ya Kusini kwa msaada mkubwa katika ujenzi wa Daraja hili jipya litakaloanzia maeneo ya Coco Beachi (Oysterbay) kwenda Hospitali ya Aga Khan (Maeneo ya Ocean Road/ Baraka Obama Road)..” Alisema Waziri Magufuli.

Waziri Magufuli aliongeza kuwa Serikali hiyo ya Jamhuri ya Korea ndio iliyowezesha pia ujenzi wa Daraja la Kikwete katika mto Malagarasi pamoja na ujenzi wa barabara ya kilomita 48 mkoani Kigoma.

“Daraja la Kikwete mkoani Kigoma limekwisha kamilika pamoja na barabara ya kilomita 48 kwa ubora mkubwa hivyo naamini kuwa hata ujenzi wa daraja hili jipya la Salender litakalopita baharini litakuwa mfano wa kuigwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki” Alisema Waziri Magufuli.

Daraja hilo jipya pamoja na barabara, litakuwa na urefu wa kilomita 7.2 na uwezo wa kupitisha magari zaidi ya 61,000 kwa siku. Ujenzi wa Daraja hilo utaanza mwaka huu na wiki ijayo makubaliano kwenye makabrasha ya kimkataba yatamalizika. Daraja hilo litakuwa na njia nne za magari pamoja service road njia za waenda kwa miguu kila upande. Mara baada ya kukamilika kwake daraja la zamani la Selander litaendelea kutumika kama kawaida sambamba na Daraja jipya la Salender.

Hafla hiyo ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Balozi wa Jamhuri ya Korea ndugu Chung Il ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe, Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi nchini Eng. Consolata Ngimbwa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS, Eng. Patrick Mfugale pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Miradi wa TANROADS Eng. Victor Seif.

No comments:

Post a Comment