Thursday, March 26, 2015

NCHI ZA UKANDA WA KATI WA UCHUKUZI ZASHAURIWA KUCHUKUA NIDHAMU YA UTEKELEZAJI YA BRN

Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),  Omari Issa amewashauri Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Kati wa Uchukuzi kuwa mifumo ya ufuatiliaji na utekelezaji itakayoharakisha ukamilishaji wa miradi iliyoko katika nchi zao.

Alisisitiza kuwa bila kuwa na mifumo ya ufuatiliaji, baadhi ya nchi zinaweza kumaliza kwa wakati miradi yake; huku nchi nyingine zikichelewa kukamilisha miradi iliyo upande wake. Hali hii inaweza kuzivunja moyo nchi ambazo zitakuwa zimekamilisha miradi yake, hasa ikizingatiwa kwamba miradi yote ya Uchukuzi ya Nchi za Ukanda wa Kati inategemeana.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa Majadiliano ya Wakuu wa Nchi za Mpango wa Uharakishaji wa Ujenzi wa Miundombinu katika Ukanda wa Kati, Bw. Issa alisema Tanzania imetekeleza miradi mbalimbali katika mwaka wa kwanza wa BRN kuliko ilivyotarajiwa kwa kutumia bajeti kidogo kutokana na nidhamu ya utekelezaji chini ya mfumo huo wa BRN, unaosisitizia katika kuweka vipaumbele, ufuatiliaji madhubuti na utatuzi wa changamoto. Nidhamu hiyo imesaidia kutatua changamoto zilizokuwa na zinazooendelea kujitokeza; na kuifanya Tanzania iweze kutekeleza kwa ufanisi miradi yake ya kipaumbele ikiwemo ile iliyo katika sekta ya uchukuzi.

Aidha, Bw. Issa alisema kuwa utekelezaji wa Miradi ya Uchukuzi ya Ukanda wa Kati nchini Tanzania unaofanyika chini ya uangalizi wa BRN, umeleta mafanikio makubwa. Hii inajumuisha kuongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, kuhuisha usafiri wa reli ya kati, barabara na miradi ya umeme katika maeneo ya ukanda huo wa kati.

Viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka nchi za Ukanda huo walionesha nia ya kuuchukua mfumo wa utekelezaji wa BRN katika sekta zao za uchukuzi ili kusaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyo katika nchi zao.

Mpango wa Kuharakisha Utekelezaji wa Ujenzi wa Miundombinu katika Ukanda wa Kati ulizinduliwa Januari, 2014, kwa lengo la kuhakikisha ujenzi wa reli, barabara, kuboresha usafiri wa majini na anga ili kuiunganisha Dar es Salaam na nchi zisizofikika kwa bahari za Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo (DRC).

Wakati miradi ya miundombinu ikiharakishwa nchini Tanzania, Serikali pia imeanza kuchukua hatua madhubuti za mageuzi katika sekta ya uboreshaji wa mazingira ya biashara ili kuvutia uwekezaji zaidi na hali bora ya uendeshaji wa biashara nchini. Sekta Sita za Kitaifa za Kipaumbele (NKRAs) ziliingizwa katika mfumo wa BRN kwa nia ya kuboresha mazingira ya biashara; ambazo ni:- Kuoanisha Taratibu na Taasisi; Upatikanaji wa Ardhi na Umiliki; Kodi: Kuoanisha Tozo, Ada na Makato; Kupambana na Rushwa, Sheria za Kazi na Ujuzi; Utekelezaji wa Mikataba, Sheria na Usalama.

No comments:

Post a Comment