Tuesday, March 10, 2015

MIAKA 20 BAADA YA BEIJING WANAWAKE WAMEPIGA HATUA -BAN KI MOON

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akifungua Mkutano wa 59 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hadhi ya Wanawake ( CSW), Mkutano huu wa wiki mbili ulioanza siku ya jumatatu, unafanyika ikiwa ni miaka 20 tangu kufanyika kwa mkutano wa kihistoria wa wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995. Mkutano huo uliokuwa chini ya Ukatibu Mkuu wa Dr. Gertrude Mongella, uliweka misingi mbalimbali iliyolenga katika kusimamia na kutetea haki mbalimbali za mwanamke zikiwamo za usawa wa kijinsia na uwezeshwaji.
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akiwa na sehemu ya Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya Wanawake ulioanza jana jumatatu hapa Umoja wa Mataifa.
Sehemu wa washiriki wa mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya Wanawake wakifuatili hotuba za ufunguzi zilizotolewa na viongozi mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu Ban Ki Moon na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Sam Kutessa.

Na Mwandishi Maalum, New York

Mkutano wa 59 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hadhi ya Wanawake maarufu kama CSW umeanza rasmi siku ya jumatatu kwa hotuba za ufunguzi kutoka kwa viongozi mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon Mkutano huu wa wiki mbili, unafanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kufanyika mwaka 1995 huko Beijing , China, mkutano wa kihistoria uliowakutanisha wanawake kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Dr. Gertrude Mongela, ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu wa mkutano huo wa Beijing, uliotoka na tamko lililoweka misingi iliyolenga pamoja na mambo mengine, kutetea na kuimarisha hadhi ya mwanamke, usawa wa kijisia na uwezeshwaji wa wanawake.

Katika siku ya kwanza ya mkutano huo, wajumbe pamoja na kusikiliza hotuba za ufunguzi pia walipitisha kwa kauli moja, Tamko la Kisiasa linalosisitiza dhamira ya ya matokeo ya mkutano wa kihistoria wa wanawake uliofanyika Beijing mwaka 1995.

Akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu, Ban Ki Moon, anasema tangu kufanyika kwa mkutano wa Beijingi miaka 20 iliyopita hali ya wanawake imeimarika katika maeneo mengi kama vile kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi, upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii pamoja na watoto wa kike kuwa na fursa ya kupata elimu.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, anasema pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi, bado kasi ya utekelezaji wa haki za wanawake na watoto wakike unakwenda kwa kusua sua na wakati huo huo wanawake na watoto wa kike wakiendelea kukabiliwa na changamoto nyingi.

Anazitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, mdororo wa uchumi, wanawake na watoto wa kike kuendelea kunyanyaswa na kukandamizwa , kupoteza maisha yao wakiwa mikononi mwa makundi mbali mbali ya kihalifu au wakikimbia machafuko.

Na kwa sababu hiyo Ban Ki Moon anasema wakati Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha miaka 20 tangu kufanyika kwa mkutano huo wa kihistoria inatakiwa kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana ili kukamilisha kazi iliyoanzia Beijing.

Vilevile Akazitaka Serikali duniani kote kushirikiana na makundi mbalimbali ya wanawake pamoja na Taasisi zinazotetea haki za binadamu. Huku akikaribisha utashi unaoonyeshwa na serikali hizo wa kufikia uwiano wa 50:50 ifikapo mwaka 2030.

Ban Ki Moon akasisitiza kuwa katika kipindi hiki ambacho jumuiya hiyo ya kimataifa inaendelea na maandalizi ya malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015, mwanamka na mtoto wa kike wanapashwa kuwa sehemu kamili ya malengo hayo.

Katika mkutano huu wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya Wanawake, wawakilishi wa serikali, Asasi za kiraia na wataalamu mbalimbali, watajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa Beijing, mafanikio yake na changamoto zake.

No comments:

Post a Comment