Wednesday, March 25, 2015

MEYA MANISPAA KINONDONI ATEMBELEA MABONDENI, AWATAKA WATU KUHAMA KUOKOA MAISHA YAO

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda (wa pili kushoto) akimsikiliza Naibu Meya, Songoro Mnyonge wakati akimpa maelezo kuhusu mazingira ya Mto Kiboko uliopo katika Kata ya Tandale wakati wa ziara yake katika Manispaa hiyo, Dar es Salaam jana.
Mkazi wa Mtaa wa Bahi, Jomo Macha akimueleza Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda athari za mafuriko katika Mtaa huo, Kata ya Makumbusho wakati wa ziara ya Meya huyo jana. Wengine ni Watendaji wa Manispaa hiyo na wakazi wa eneo hilo.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akitoa maelekezo kwa watendaji wa Manispaa hiyo kuhusu kutafuta ufumbuzi wa chemba ya majitaka iliyofurika katika Mtaa wa Balozi Msolomi wakati wa ziara yake. Kulia kwake ni Naibu Meya, Songoro Mnyonge na watendaji wa Manispaa hiyo.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda (mbele) akikagua mto Ng'ombe uliopo eneo la Mwananyamala Kisiwani, wakati wa ziara hiyo Nyuma yake ni Naibu Meya,Songoro Mnyonge.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda (kulia) akijadiliana jambo na Naibu Meya, Songoro Mnyonge wakati wa ziara aliyoifanya katika Mtaa wa Kimamba, Kata ya Makurumla kukagua athari za mafuriko na changamoto zake jana. Katikati ni Diwani wa Kata hiyo, Rajab Hassan.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda (kulia) akikagua athari za mafuriko katika moja ya nyumba za Mtaa wa Kimamba, Kata ya Makurumla alipofanya ziara yake katika Manispaa hiyo, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Diwani wa Kata hiyo, Rajab Hassan.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimamba, Kata ya Makurumla, Mohamed shukuru akisisitiza jambo kwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda kuhusu mikakati wanayoifanya kuepuka mafuriko wakati wa ziara ya Meya huyo aliyoifanya katika Mtaa huo jana. Kushoto ni Naibu Meya, Songoro Mnyonge na Diwani wa Kata hiyo, Rajab Hassan.
Msafara wa Meya wa Kinondoni ukijiandaa kuondoka eneo la Mto Ng'ombe baada ya kukagua mto huo, eneo la Mwananyamala Kisiwani.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda amewataka wakazi kwenye mikondo ya maji wahame haraka kwa usalama wa maisha yao na si kusubiri waondolewe kwa nguvu.

Mwenda alisema tayari baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walishalipwa fidia na kutafutiwa maeneo mengine na Serikali lakini wamerejea na kuendelea na maisha yao jambo ambalo alisema sasa Manispaa yake haitasita kuwaondoa kwa nguvu.

Akizungumza wakati wa ziara yake aliyoifanya katika maeneo ya mabondeni na mikondo ya maji katika Manispaa hiyo Dar es Salaam jana Meya huyo alisema anashangaa kuona watu wanajenga makazi katikati ya mkondo wa maji na kusababisha maji hayo kukosa uelekeo na kuingia kwenye makazi yaw engine hususan kipindi hiki cha mvua ilhali tayari walishaondolewa.

“Mfano watu wa Kinondoni Hananasif na Suna tayari walishapewa fidia na kupewa viwanja, lakini wengi wao wameshauza viwanja hivyo na kurudi tena maeneo hayo. Hii inashangaza sana. Tunafanya hivi kwa faida ya maisha yao hatutaki kuona watu wanakufa yanapotokea mafuriko.” Alisema Meya Mwenda.

Mwenda alifanya ziara hiyo katika Kata za Makurumla, Tandale, Makumbusho na Mwananyamala na kushuhudia baadhi ya wakazi wakiwa wamejenga nyumba zao katikati ya mikondo ya maji na kusababisha maji kukosa uelekeo na kuingia katika makazi ya watu ikiwemo Mtaa wa Kimamba eneo la Daraja la Mwinyi.

Katika hatua nyingine Meya huyo alimwagiza Mhandisi Mkuu wa Manispaa hiyo kuwasiliana na Wahandisi wa kampuni ya ujenzi ya Strabag kupata ufumbuzi wa tatizo la mifumo ya majitaka inayopita kwenye  barabara hiyo kutafuta njia ya kupeleka maji hayo ili kuzuia yasiingie katika makazi ya watu hususan katika kipindi hiki cha mvua.

Hata hivyo Meya huyo amesifu jitihada za wataalamu wa Manispaa hiyo kwa kushirikiana na watendaji za kuhakikisha wanasafisha njia za maji ikiwemo mitaro ma mito mbalimbali akitolea mfano Mto Ng’ombe uliopo Mwananyamala Kisiwani ambao awali ulikuwa ukifurika maji na kusababisha mafuriko maeneo mbalimbali ikiwemo Tandale kwa Mtogole kutokana na kujaa taka ukilinganisha na sasa.

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf  Mwenda alifanya ziara yake katika maneo mbalimbali ya mabondeni na kwenye mikondo ya maji yaliyopo kwenye Manispaa hiyo Dar es Salaam jana ili kuona athari za mafuriko zilizojitokeza kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha jijini kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa kuepukana na mafuriko hayo.

No comments:

Post a Comment