Tuesday, February 3, 2015

Waziri Lukuvi atangaza mapambano dhidi ya wanaodhulumu ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akijibu hoja za kamati na wabunge mjini Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akijibu hoja Bungeni kuhusu wizara yake.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe akijibu hoja za kamati hoja za kamati.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Said Nkumba akiwasilisha taarifa ya kamati yake. Picha na Hussein Makame-MAELEZO,Dodoma.

Hussein Makame-MAELEZO,Dodoma

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema Serikali itahakikisha inapambana na watu wote wanaoendesha vitendo vya dhuluma, matapeli na wanaonyang’anya viwanja, majengo, mashamba na ardhi za wanyonge.

Waziri Lukuvi ametangaza azma hiyo wakati akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliochangia Taarifa ya Kamati ya Bunge, ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyowasilishwa na kupitishwa Bungeni mjini Dodoma.

Alisema anatambua kwamba hasa maeneo ya mijini kuna dhuluma nyingi zinafanyika ambapo masikini, mayatima na wajane wanadhulumiwa na kunyang’anywa ardhi na majengo yao.

“Wizara yangu tutahakikisha tunapambana sana na watu wote, wakubwa na wadogo, matajiri na watumishi wa Serikali waisio waaminifu na matapeli wote wanaoendesha vitendo vya dhuluma na kunyang’anya viwanja, majengo, mashamba na ardhi za wanyonge” alisema Lukuvi.

Aliongeza “Najua mijini hasa kuna dhuluma nyingi, masikini hasa wanadhulumiwa, mayatima na wajane wananyang’anywa ardhi na majengo yao.Tunajua baadhi ya wafanyakazi wa ardhi wasio waaminifu wanashirikiana”

Alisema moja ya kazi kubwa ya Wizara yake ni kuhakikisha kwamba wanashirikiana ili kuhakikisha wanatokomeza udhalimu huo unaoendelea nchini.

Kwa upande wa migogoro ya ardhi ambayo inaripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini, Waziri Lukuvu alisema watashirikiana na Wizara husika na wananchi kwa ujumla ili kuitatua.

“Lakini pia tutashirikiana na wananchi, Wizara ya Maliasili na TAMISEMI.Tutakaa pamoja kuhakikisha tunasuluhisha hii migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali yanayohusu miji na yanayohusu vijiji” alisema Waziri Lukuvi.

Alibainisha kwamba migogoro ni mingi na wanaosababisha migogoro hiyo ni watu, kwa hiyo ameomba ushirikiano na taasisi na watu mbalimbali kumaliza migogoro hiyo.

Alisema badala ya wananchi kwenda Dar es Salaam kushughulikia migogoro yao, yeye pamoja na watendaji wa wizara watatembelea mikoani ili kutatua migogoro hiyo.

“Na mimi nimeamua sasa badala ya watu kuja Dar es Salaam kumfuata Waziri na makamishna, sasa mimi nitapanga ratiba nitakuja huko kila mkoa na watalamu wote muhimu wenye uwezo wa kuamua”alisema na kuongeza:

“Ili tuje tutatue migogoro huko huko kwenye maeneo.Ile ambayo ipo kwenye uwezo tutaitatua palepale, ile ambayo itahitaji kuitolea majibu mafupi tutaitolea majibu, tunaombeni ushirikiano wenu” Waziri Lukuvi alijibu hoja ya Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah aliuliza hatma ya shamba la Utumaini la Mafia, na kusema Serikali imechukua hatua na imetoa notice ikiwa ni hatua za kulichukua shamba hilo lenyewe ukubwa wa hekari 1000.

“Tayari tumeshatuma kwa anayejifanya anamiliki hilo shamba tarehe 28 mwezi huu notice ya kutaka kulichukua hilo shamba ambalo tutasubiri muda wa siku 90 zikiisha hatua zinazofuata zitaendelea” alisema.

Hivyo alimtaka mbunge Shah na wananchi wa Mafia watambue kwamba Serikali imeshaanza kuchukua hatua juu ya shamba hilo na mengine ambapo alibainisha kuwa lengo la Serikali ni kulichukua shamba lote.

Akiwasilisha Taarifa ya Kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati James Lembeli ,alitaja migogoro mbalimbali ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini huku akiishauri Serikali kuimaliza migogoro hiyo.

No comments:

Post a Comment