Monday, February 2, 2015

HOSPITALI YA ENDUIMET WILAYA YA LONGIDO YAPATA MTAMBO WA NGUVU ZA JUA

Paroko wa Kanisa Katoliki,Parokia ya Enduimet,Jimbo Kuu la Arusha,Padri Pius Shao(katikati)akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa Mtambo wa kuzalisha Umeme kwa nguvu za Jua ,kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kusambaza Teknolojia(KAKUTE),Livinus Manyanga na Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Longido,Gerson Mtera.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kusambaza Teknolojia(KAKUTE),Livinus Manyanga akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mtambo wa kuzalisha Umeme kwa nguvu za Jua katika hospitali ya Kanisa Katoliki,Parokia ya Enduimet wilaya ya Longido mkoa wa Arusha,mtambo huo umegharamiwa na Wakala wa nishati Vijijini(REA)na wadau wengine.
Paroko wa Kanisa Katoliki,Parokia ya Enduimet,wilaya ya Longido Jimbo Kuu la Arusha,Padri Pius Shao akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mtambo wa kuzalisha Umeme kwa nguvu za Jua uliogharamiwa na Wakala wa nishati Vijijini(REA)na wadau wengine.

Hospitali ya Kanisa Katoliki Parokia ya Enduimet,Jimbo Kuu la Arusha imekabidhiwa Mtambo wa nishati Jua wenye uwezo kuzalisha 10 KW ,uliofadhiliwa kwa pamoja kati ya Wakala wa Nishati Vijijini(Rea) na serikali ya Ujerumani kwa lengo la kuiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma za afya kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo,Padri Pius Shao alisema kuwa kabla ya mradi huo wa kutumia nishati Jadidifu kuanza walikua wakitumia Genereta dogo ambalo lilikua haliwezi kukidhi mahitaji ya hospitali jambo ambalo lilikua kikwazo katika utendaji kazi kwani halijaunganishwa na Gridi ya taifa.

Alisema kutokana na kiwango cha umeme wanachopata wanakusudia kuanza huduma za upasuaji mwezi huu,hatua itakayowapunguzia gharama wagonjwa kwenda mbali kutafuta huduma hizo.

“Mtakumbuka wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuja kuongoza harambee ya ujenzi wa hospitali hii mwaka 2012, tulimwomba gari la kubeba wagonjwa tayari limeshafika na linatoa huduma hiyo kwenye vijiji vinavyotuzunguka,tutazidi kutafuta fedha zaidi kuhakikisha tunapata huduma bora za kiafya kwa wananchi wetu ili waweze kufanya shughuli za kuwaletea maendeleo,”alisema Padri Pius

Awali Mkurugenzi wa Kampuni ya Kusambaza Teknolojia(Kakute)iliyofunga mitambo hiyo,Livinus Manyanga alisema mradi wa kufunga mtambo wa kufua wa jua kwaajili ya kuboresha huduma ya afya kwenye hospitali ya Enduimet ni matokeo ya shindano la kubuni miradi ya kuendeleza nishati vijijini linalotolewa na REA kila baada ya miaka miwili na kufadhiliwa na Benki ya Dunia.

Alisema fedha zilizotekeleza mradi huo ni ruzuku ya Sh 146 milioni kutoka REA,serikali ya Ujerumani ilitoa kiasi cha Sh 121 milioni na wadau wengine kiasi cha Sh 38 milioni zilizofanikisha mradi huo kwenye jamii ya wafugaji.

Manyanga alisema kuwa malengo ya mradi huo mbali ya kuweka mtambo katika hospitali hiyo pia umewaunganishia umeme wa mkopo nafuu familia 100 ndani ya vijiji vya Kamwanga,Lerangwa na Olmolog.

No comments:

Post a Comment