Friday, January 2, 2015

WANAOKAA KWENYE NYUMBA MBOVU MJI MKONGWE ZANZIBAR WATAKIWA KUHAMA - BALOZI SEIF IDDI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia nyumba iliyoporomoka dari na kujeruhi wakazi wake watatu hapo Mtaa wa Ukutani Mjini Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Mmiliki wa Nyumba Hiyo Bwana Mzee Abdulla Juma.
Balozi Seif akiwaagiza watu wanaoishi ndani ya nyumba iliyoporomoka dari Mtaa wa Ukutani kuhama ili kunusuru maisha yao kutokana na uchakavu wa nyumba hiyo. Aliyepo mwanzo kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mjini Kanali Mstaafu Abdi Mahmoud Mzee.
Balozi Seif akiwa pamoja na Mmiliki wa nyumba iliyoporomoka Dari eneo la Ukutani Bwana Mzee Abdulla Juma na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Kanali Mstaafu Abdi Mahmoud Mzee wakiangalia hali halisi ya mazingira ya nyumba hiyo. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza wananchi wanaoishi kwenye nyumba mbovu na zile zilizochakaa ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar wafanye utaratibu wa kuhama kwenye nyumba hizo mapema iwezekanavyo ili kunusuru maisha yao.

Alisema Serikali kamwe haitakuywa tayari kuachia wananchi wake wanaendelea kuishi katika mazingira ya hatari wakati njia za kuepuka hatari hizo zipo na wala hazina gharama yoyote.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi ya kukagua Nyumba ya Bwana Mzee Abdulla Juma ambayo iliporomoka dari sehemu ya sebule na kujeruhi wakaazi watatu wa nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Ukutani Mjini Zanzibar.

Watu waliojeruhiwa ni wadogo wa Mmiliki wa Nyumba Hiyo Bwana Haroun Abdulla Juma na Fahim Abdulla Juma waliolazwa Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja kwa matibabu pamoja na Peter Monga aliyetibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Balozi Seif aliutaka uongozi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kuendelea kuzifanyia uhakiki nyumba zote zilizomo ndani ya mji mkongwe na hatua zichukuliwe mara moja na taasisi zinazohusika katika kuwahamisha wakaazi wanaoishi kwenye nyumba zisizostahiki kuishi watu.

Mapema Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana Mzee Abdulla Juma alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mkasa huo umetokea majira ya saa 11.00 za asubuhi wkati dari ya nyumba hiyo sehemu ya sebule ilipoporomoka.

Bwana Mzee alisema wakaazi wa nyumba hiyo kwa kushirikiana na majirani walilazimika kuuvunja mlango mkuu wa nyumba hiyo ili kumnusuru Mtoto wa mdogo wake aliyelazwa Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja baada ya kuvunjika mguu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Mussa Awesu Bakari alisema watendaji wa Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na wataalamu wa Taasisi za majengo na ujenzi tayari wameshafanya uhakiki wa Nyumba 75 zilizomo ndani ya Mji Mkongwe .

Nd. Mussa alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba zoezi hilo linaendelea kwa lengo la kubaini nyumba zisizofaa kutumiwa kwa makazi ya kawaida ya binaadamu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment