Wakati
mwingine migogoro ya ardhi inasababishwa na kutojua. Wengi hawajui taratatibu
na ndio maana hujikuta wanainga katika matatizo. Moja ya maeneo ambako watu
wamekuwa wakipatia matatizo ni huu wakati wa kununua. Yapo mambo mengi unapoununua ardhi, nyumba au
kiwanja ambayo wewe kama mnunuzi unatakiwa kuyajua na kuyazingatia ili usiingie
katika matatizo. Nimefanya utafiti
katika kesi za ardhi mahakamani na kugundua kuwa moja ya eneo baya linalowaingiza watu mkenge
ni hili la mume kuuza nyumba au
kiwanja bila kupata ridhaa ya mke wake . Ikumbukwe kuwa suala la ridhaa hapa sio suala la hiyari
isipokuwa ni suala la lazima na la kisheria ambalo kutolitekeleza kwake
kunaweza kupelekea mnunuzi kupoteza kile alichokinunua. Ni hatari ndugu na
umakini unahitajika.Mume anapouza nyumba/kiwanja kuna kitu huitwa ridhaa ya
mwanandoa ambacho ni lazima akisaini, tutaona.
NINI
MAANA YA RIDHAA YA MWANANDOA.
Ridhaa
ya mwanandoa(Spouses consent) ni ridhaa ambayo anapaswa kuitoa mwanandoa
inapokuwa inauzwa mali( nyumba/kiwanja/shamba) ambayo mwanandoa naye ana maslahi
au anaimiliki kwa pamoja na mme wake au mke wake. Ridhaa hii pia huweza
kutolewa na mume iwapo anayeuza ni mke na huweza kutolewa na
mke iwapo anayeuza ni mume. Ni hatua ya lazima unapokuwa unanunua nyumba ,
kiwanja au shamba.
KWANINI MUHIMU ZAIDI
MKE KUTOA RIDHAA.
Hapo
juu tumeona kuwa pia mume anatakiwa kutoa
ridhaa iwapo mke ndiye anayeuza halafu tukaona kuwa pia mke anatakiwa kutoa ridhaa iwapo mme
ndiye anauza. Lakini utashangaa katika makala yangu naongelea zaidi mke kutoa
ridhaa mume anapouza. Ninamuongelea mke kutoa ridhaa zaidi kwakuwa utafiti unaonesha kuwa migogoro mingi katika hatua hii imetokea baada ya mume kuuza bila ridhaa ya mke. Wanaume wengi
ndio huwazunguka wake zao na kuuza.Hii ndio
maana hata kichwa cha mada hii kinaongelea zaidi mume kuuza bila ridhaa ya mke kwakuwa hapa
ndipo penye tatizo.
NI
NYUMBA/KIWANJA GANI AMBACHO LAZIMA MUME KUPATA
RIDHAA YA MKE.
Nyumba
au kiwanja ambacho mume ni lazima kupata ridhaa ya mke ni ile ambayo
wanaimiliki kwa pamoja. Wanayoimiliki kwa pamoja ni ile ambayo wamejenga kama wanandoa au kununua wakati wakiwa katika ndoa na ile ambayo
mke wakati wa kuolewa amemkuta nayo mwanaume lakini wakati wakiwa wote katika
ndoa kuna maendelezo yoyote waliyofanya
hata yawe kiduchu. Kununua pamoja si lazima iwe huyu analeta hela na huyu
analeta hela hapana hata kukaa nyumbani
kupika, kufagia halafu mwanaume akatafuta
hela na kununua ni kuipata pamoja na haiwezi kuuzwa bila ridhaa ya mke.
JE NYUMBA IKIWA
KATIKA JINA LA MUME NI
LAZIMA KUPATA RIDHAA YA MKE.
Ndio
hata kama ipo katika jina la mume ni lazima
kupata ridhaa ya mke. Nyumba au kiwanja kuwa katika jina la mume haiondoi
matakwa ya sheria ya kuwa ni ya wote . Kuwa katika jina la mume ni taratibu tu lakini bado inakuwa ni ya familia au ya wote. Hapa
wanaume huwalaghai wanunuzi kwa kuonesha majina yao kwenye hati ili wauze bila
ridhaa ya wake. Mnunuzi usidanganywe na jina kwenye hati.
DOCUMENT YA
RIDHAA YA MWANANDOA IWE NA VITU
GANI.
Document
ambayo inaitwa ridhaa ya mwanandoa ambayo wakati unauziwa kiwanja au nyumba ni
lazima mke aisaini inakuwa na jina la
mke wa muuzaji, ikieleza dini yake, anuani yake na ikiapa kuwa yeye ni mke
halali wa muuzaji fulani fulani. Baada ya hapo
kutakuwa na kipengele ambacho
mwanamke ataapa kwa kutoa ridhaa yake ya
kumruhusu mume wake kuuza nyumba au kiwanja
na atakitaja hicho kiwanja/nyumba namba zake(plot no) na eneo kilipo ikiwa ni
pamoja na kiasi cha mita kama ni
kiwanja. Baada ya hapo atasaini kwa chini na kuandika jina lake na mume wake
muuzaji ataandika jina lake naye atasaini.
NINI KITATOKEA MKE ASIPOSAINI
DOCUMENT YA RIDHAA YA KUUZA NYUMBA/KIWANJA.
Ni
rahisi tu kuwa unaponunua nyumba ambayo iko
katika mazingira kama niliyoeleza bila mwananke kusaini ridhaa ya mwanandoa
wewe mnunuzi unakuwa umepoteza kwakuwa
ununuzi huo ni batili na mda
wowote mke akiamua kurudisha ile nyumba
anairudisha na mnunuzi unapata hasara.
UFANYE NINI MNUNUZI
ILI KUEPUKA HILI.
Wanaume
wengi ni wajanja na wanauza nyumba
viwanja bila kujali hili na matatizo utayapata mnunuzi baadae. Na si
rahisi mume akwambie ukweli kuhusu hili akishafanya maamuzi ya kuuza na hivyo
usitegemee kumuuliza ili upate ukweli. La kufanya ni kuwa hakikisha unapepeleza
kama muuzaji mume ana mke na ukijua ana mke hakikisha mwanamke anasaini hiyo document
bila kujali ile mali inayouzwa ni yao wote au ya mume peke yake ili kuwa upande
salama zaidi. Wewe mnunuzi huwezi kujua imepatikanaje hayo ni yao wanan doa
yatakuchanganya. Sasa ili kuweka mambo sawa iwe yao wote au hapana we muombe tu muuzaji mke wake asaini
nyaraka ya ridhaa kwakuwa kwa kufanya hivyo hapotezi lolote kama kweli hakuna
jambo analoficha au kama hakuna utata. Narudia tena, usijaribu wala usinunue
nymba au kiwanja kwa mume bila mke
wake kusaini ridhaa ya mwanandoa utapata
matatizo sana na ulichonunua ipo siku tu kitarudishwa na wewe
utapoteza, ni hayo kwa leo.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA
MSHAURI WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI LA
HABARI LEO KILA
JUMANNE, GAZETI JAMHURI KILA
JUMANNE NA NIPASHE KILA
JUMATANO.
0784482959, -0714047241 bashiryakub@ymail.com
Kwa kweli hapa mwanasheria umeongea jambo zuri sana, Wanaume wengi huwa tunachukua uamuzi bila kuwashirikisha wake zetu. Pia kuna usemi ambao sio rasmi kuwa mume ni kichwa hivyo mwanamke hana maamuzi yeyote yale.Hata ndugu husema inaonekana mwanaume huna sauti mbele ya mke wako au umekamatwa yaani umepewa limbwata kwa kupata ridhaa ya mke kwa jambo lolote lile.
ReplyDeleteShukrani sana
ReplyDelete