Tuesday, January 13, 2015

Saccoss za Vijana katika Halmashauri ni Muhimu: Vijana

Kijana Andrew Mlaki kutoka kikundi cha Akili ni Mwanga akielezea vijana wenzake (hawapo pichani) shughuli zinazofanywa na kikundi chake baada ya kikundi hicho kutembelewa na wawezeshaji waliofika Wilaya ya Mwanga kuhamasisha vijana na kuwapa elimu kuhusu ujuzi na stadi za maisha. Kushoto ni mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa.
Afisa Vijana wa Wilaya ya Mwanga Bibi Subira Mfanga akizungumza na vijana walioshiriki semina ya uhamasishaji kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana Mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Mwanga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bw. Jamhuri David Willium (katikati) akisikiliza mrejesho kutoka kwa wawezeshaji wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo waliofika ofisini kwake baada ya kufunga semina ya uhamasishaji kwa Vijana wa Wilaya za Mwanga na Moshi Vijijini hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bw. Jamhuri David Willium kushoto akipokea Sera ya Maendeleo ya Vijana kutoka kwa mwezeshaji wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa baada ya kufunga semina ya uhamasishaji kwa Vijana wa Wilaya za Mwanga na Moshi Vijijini hivi karibuni.
Wawezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Maafisa Ushirika na Maafisa Vijana kutoka Wilaya ya Mwanga na Moshi Vijijini, katika picha ya pamoja na baadhi ya Vijana wa Wilaya hizo walioudhuria semina ya uhamasishaji kwa vijana kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro. (Picha zote na : Genofeva Matemu – Maelezo)

Vijana wa Mkoa wa Kilimanjaro wameziomba Halmashauri zao kuhamasisha vijana kuanzisha Saccoss za Wilaya zitakazowawezesha vijana kuwekeza na kuwasaidia kuomba mkopo wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana utakaopitishiwa katika Saccoss hizo ili waweze kujiajiri wenyewe na kuondokana na umasikini.

Hayo yamesemwa na Vijana wakati wa kufunga semina ya uhamasishaji kwa vijana kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kuiomba Wizara yenye dhamana na vijana kujitolea kutoa elimu kwa vijana mara kwa mara itakayowawezesha vijana kujitambaua na kuwajengea uwezo.

Akizungumza baada ya kufunga semina hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bw. Jamhuri David Willium ameishukuru timu kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuweza kufika katika Halmashauri yake na kuwaomba kujitolea pale Wilaya itakapowahitaji kwa mara nyingine kwa ajili ya kuelimisha vijana wa Mwanga.

Bw. Willium amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ipo karibu na vijana wake, imeweza kuwaunganisha vijana kwenye vikundi mbalimbali na kuwashirikisha vijana katika shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Halmashauri hiyo hivyo kuwahaidi vijana kushughulikia ufunguaji ya Saccoss ya vijana kwa maendeleo ya vijana wa Mwanga.

“Vijana ni taifa la leo, sisi kama viongozi wa Halmashauri tupo tayari kushirikiana nao kwa jitihada zote kwani umuhimu wa Saccoss ya vijana katika Halmashauri tunaufahamu hivyo tutajitahidi kusimamia suala la ufunguzi wa Saccoss ya vijana itakayowawezesha kujitegemea kwa maendeleo yao na maendeleo ya Wilaya ya Mwanga”, amesema Bw. Willium.


Naye mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa ameuomba uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kushirikiana na wadau wengine wanaojishughulisha na masuala ya vijana kuwasaidia Vijana wa Mwanga huku wakitumia vyombo vya habari kuelimisha vijana na kubadili fikra za vijana kuwa chanya.

No comments:

Post a Comment