Na Bashir Yakub
Vijana wengi wajasiriamali wadogo wamefungua makampuni. Hakika wote waliofanya hivi wamefanya jambo jema linaloendana na wakati. Niliwahi kuandika wakati nikielekeza namna nyepesi kabisa ya kufungua kampuni kuwa, ni vigumu kwa leo kufanya biashara na ukawa na mafanikio nje ya kampuni. Nikasema hata kama unauza maziwa, mama ntilie, unauza mayai, kibanda cha huduma ya fedha kupitia simu,unauza mihogo, haizuiwi kufungua kampuni.
Kuna kampuni hata za mtaji wa milioni moja na pesa hiyo si lazima uwe nayo mkononi ila ni katika maandishi tu. Nikasema anayetaka mafanikio kwa sasa ahakikishe hiyo biashara yake ndogo kabisa anaifungulia kampuni.
Kwakuwa wapo wengi ambao tayari wamefungua makampuni basi zipo changamoto nyingi wanazokumbana nazo na kubwa zaidi ni taarifa au ujuzi wa mambo mbalimbali ya namna ya kuendesha kampuni ili kampuni iwe kampuni kweli.
Moja ya eneo lenye shida au ambalo wajasiriamali wadogo hawana taarifa nzuri kuhusu ni taarifa za kodi zinavyolipwa na kampuni kisheria. Hawajui ni kiasi gani, kwa muda gani na vipi. Leo hapa nitaeleza kwa uchache kuhusu kodi za kampuni. Kampuni hulipa kodi ya mapato, swali ni kodi ya mapato nini.
1. KAMPUNI HULIPA KODI YA MAPATO, JE KODI YA MAPATO NINI ?
Kodi ya mapato Tanzania ni tozo kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana na vyanzo vitatu ambavyo ni ajira, biashara pamoja na uwekezaji. Aina hii ya kodi inatozwa kwa mamlaka ya Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004, kama ilivyorekebishwa.Kwa upande wetu wa kampuni kodi inayolipwa kwa tafsiri hiyo hapo juu ni kwakuwa kampuni ni biashara na pia ni kwakuwa ndani kampuni waweza kuwamo uwekezaji.Hii ndio sababu kampuni hulipa kodi ya mapato.
2. JE WAJUA KUWA SI KILA KAMPUNI HUTAKIWA KULIPA YA MAPATO.
Mjasiriamali anatakiwa kujua kuwa si kampuni zote hutakiwa kulipa kodi ya mapato. Kampuni zinazotakiwa kulipa kodi ya mapato ni kampuni zenye Dhima ya ukomo. Kampuni zenye dhima ya ukomo ni zile zote ambazo ni Limited. Kama kampuni yako ni Limited (LTD) basi inatakiwa kulipa kodi ya mapato. Nyingine zinazotakiwa kulipa kodi ni kampuni za kudumu za ndani na matawi ya Kampuni za wageni/wasio wakazi. Hizi hazihusiki na wajasiriamali sitazifafanua zaidi.
Aidha,kama kampuni umeiunda na umeingia ubia na kampuni nyingine basi hutakiwi kulipa kodi ya mapato.
3. USIOGOPE KODI HUTOZWA KATIKA FAIDA TU NA SI KUTOKA KILA FEDHA UNAYOINGIZA.
Kodi ya mapato ya kampuni hutozwa kwenye faida tu iliyotokana na shughuli za biashara za kampuni au faida uliyoipata kutokana na uwekezaji. Umeunda kampuni umempata mtu ana mtaji akawekeza mtaji, faida inayopatikana hapo ndiyo faida kutoka katika uwekezaji. Ifahamike kuwa si kweli kuwa kila unachoingiza lazima kilipe kodi.
4. JE MAMLAKA YA MAPATO WANAJUAJE FAIDA ULIYOPATA ILI WAKUTOZE KODI SAHIHI.
Hapo juu tumeona kuwa faida tu ndio hutozwa kodi ya mapato lakini tujiulize swali, biashara unafanya wewe ,akaunti za kampuni unazo wewe, kila kitu kuhusu kampuni yako ni wewe, je hawa watu wa mapato wanajuaje faida unayopata ili wakutoze kodi sahihi .Kuna yafuatayo ;
( a ) Kuna kitu kinaitwa utangazaji wa Mapato na Kodi ambacho ni tamko linalowasilishwa TRA kuonesha mapato na kodi inayopaswa kulipwa kwa kila mwaka wa mapato. Kwa mujibu wa sheria ya kodi, kampuni inalazimika kuwasilisha makisio hayo hata kama haina faida. Wewe mwenyewe unajitathmini umepata nini na unatakiwa kulipa nini na unapeleka mwenyewe makadirio hayo. Kinyume chake ni kosa na asiyefanya hivyo adhabu inamsubiri.
( b ) Hesabu za makadirio hayo unayopeleka TRA lazima ziwe zimefanywa na mhasibu ambaye anatambuliwa na bodi ya uhasibu Tanzania na kukaguliwa na mkaguzi wa hesabu anayetambulika pia. Hawa ndio wanaotegemewa na TRA kupeleka ukweli wa umepata faida kiasi gani na unatakiwa ulipe kiasi gani. Ndio maana wanaitwa wahasibu wanaotambulika.
5. KODI YA KAMPUNI NI 30% TU YA FAIDA.
Kiwango kinachotumika cha kodi ya mapato ya kampuni ni kukatwa asilimia 30 ya faida, na kwa kawaida hulipwa katika hatua mbili. Kodi ya kwanza hulipwa kulingana na makadirio ya mlipa kodi mwenyewe mwanzo wa mwaka wa biashara kama nilivyoonesha hapo juu, na kodi ya mwisho hulipwa baada ya utathmini rasmi wa mapato kamili mwisho wa mwaka wa mapato.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
UBARIKIWE SANA MTUMISHI WA BWANA KWA ELIMU NZURI KAMA HII.
ReplyDeleteMUNGU AKUONGEZEE HEKIMA NA MAARIFA.
AKUJAALIE AFYA NJEMA DAIMA!
Je ni aina hii tu ya kodi inayokipwa na makampuni? Na je kama kodi iliyolipwa kwenye mwanzo wa mwaka sijafanikiwa kufikisha yale mauzo kadalio mwisho wa mwaka, je vipi pesa hiyo niliyolipa infanywaje?
ReplyDelete