Tuesday, January 27, 2015

MAKALA SHERIA: HAITOSHI KUUNDA KAMPUNI, LAZIMA UWE NA LESENI YA BIASHARA, HII NI NAMNA YA KUPATA LESENI YA BIASHARA

Na   Bashir     Yakub

Katika  makala  iliyopita  nilisema  kuwa  vijana  wengi   wajasiriamali  wanaofungua   biashara  za  makampuni   wanao  uwezo  mkubwa   wa kufika mbali   isipokuwa  tatizo  lao  ni  taarifa za  mambo  mbalimbali   kuhusu uendeshaji  wa  kampuni   hizo. 

 Mambo  ya uendeshaji   wa  kampuni  ni  mepesi sana  na  yanawezwa   na  mtu  yeyote isiopokuwa   tatizo   ni   taarifa   na  elimu ya  namna  ya  uendeshaji  kisheria   ili   kampuni   ionekane  ni kampuni.  Nilieleza  namna   kampuni  inavyolipa kodi   na  taratibu  za   kikodi  za kampuni.

  Leo tuangalie  kipengele  kingine  cha  uendeshaji  wa kampuni  ambacho  ni namna  ya   kupata   leseni  ya   biashara.

1. KAMPUNI   ULIYOSAJILI   HAIWEZI   KUANZA   KAZI   BILA   LESENI    YA BIASHARA.

Wajasiriamali   wengi   wanaofungua kampuni   wanajua   kuwa   ukishapata usajili   wa   kampuni   basi    unakuwa umemaliza   kila   kitu   na   unaweza  kuanza   biashara.  Wazo  hili  si   la  kweli kwakuwa  baada  ya  kampuni  kuwa  imepata usajili  na    unataka   kuanza biashara   ni   lazima  uwe   na   leseni   ya biashara (business  licence).  Kwa   maana   hii   kumbe  mchakato   wa kuanza   biashara   na   kampuni   hauishii kwenye  kupata     usajili   wa   kampuni. Cheti  cha  kuzaliwa  kwa  kampuni  yako ( certificate  of  incorporation)  ni  tofauti na  leseni   ya   biashara.Na   ili  biashara  ya  kampuni  ianze  kisheria  lazima  uwe  navyo  vyote  viwili.

2. LESENI   YA   BIASHARA   HUTAFUTWA    WAPI.

Leseni   za   biashara   zote  hupatikana  manispaa.   Kama   wakati  wa  kusajili kampuni   uliandika   kuwa   ofisi    ya kampuni   yako  (Registered  Office) itakuwa   wilaya   fulani  basi   leseni inatakiwa   kufuatwa   katika  manispaa  ya  wilaya  hiyo.   Kwa mfano  uliandika  kuwa   ofisi   za   kampuni    zitakuwa Kinondoni, hii   ina   maana   kuwa  ukitaka   leseni   ya   biashara   lazima uifuate   manispaa   ya   kinondoni   na  si kwingine. 

3. MWENYE   SIFA    ZIPI    ANARUHUSIWA  KUPATA   LESENI   YA    BIASHARA.

Sifa  ya  kwanza  ni kuwa  mtu  yeyote raia wa Tanzania anayo   haki   ya kupatiwa   leseni   ya   biashara.  Pili   Mtu  huyo   awe   ametimiza  umri   wa miaka   kumi   na  nane (18).  Tatu    awe na  akili  timamu.   Nne   awe  na  eneo  la  kufanyia   biashara  linalokubalika   kisheria.   Aidha   utaratibu  uko  tofauti  kidogo  kwa  mtu  ambaye   sio   raia   wa   Tanzania.  Mtu  ambaye   sio  raia  wa Tanzania   hawezi  kutafuta  leseni ya  biashara   ikiwa   hajapata  kibali  maalum   kutoka   idara  ya  uhamiaji.  Kibali  hicho  lazima kiwe  kinaonesha  biashara   aliyokuja  kuifanya  nchini  na  kazi  hiyo hiyo  iliyo  kwenye  kibali  hicho  ndiyo   tu  itakayotolewa  leseni  na  manispaa.

    4. KUPATA   LESENI   BILA   USUMBUFU  NENDA   NA    VIAMBATANISHO   HIVI.

(i)  Kama  ni  mtu  binafsi  nenda  na  jina  la  Biashara  ulilochagua  na  kama  ni kampuni   nenda  na  (Certificate of  Incorporation  or  Registration).

(ii)   Pia  kama  ni kampuni  nenda  na Memorandum  and  Article of Association” .

(iii)  Nenda  na Kitambulisho   cha  mpiga  kura,  Cheti   cha  kuzaliwa   au  Hati  ya  kiapo  kuonyesha   kuwa   ni   Mtanzania   na    kama  ni mgeni   Hati   ya   kuishi  nchini   daraja  la “A” (Residence    Class “A”).

(iv)  Usisahau  hati   ya   kiuwakili  (powers  of  attorney)  kama   wenye   hisa   wote  wa Kampuni wapo   nje  ya   nchi.

(v)   Pia  lazima  uende  na  ushahidi   wa  kimaandishi  kuonesha  kuwa   una  mahali  pa  kufanyia  biashara  . Ushahidi  wa  kimaandishi   waweza   kuwa  hati   za  nyumba  za  mahali  utakapofanyia  biashara , mkataba   wa pango  la sehemu    uliyopanga   kufanyia   biashara,  risiti   za  malipo   ya   kodi   za majengo   au    ardhi  za  mahali utakapofanyia   biashara.

(vi)   Kumbuka  kwenda  na  hati  ya  kujiandikisha   kama   mlipa   kodi   TRA (TIN) .
Ukiwa  na  vitu   hivi   hautapata  usumbufu   kupata   leseni  ya  biashara  na utakuwa  umeepuka   nenda  rudi.

5. FOMU    YA     MAOMBI     YA   LESENI   YA    BIASHARA   NI   HII.

Maombi  ya  leseni  ya  biashara  yana  fomu  maalum  iitwayo   9TFN 2110   kwa jina  la  kitaalam.  Hii   ndiyo  mwombaji  anatakiwa   kujaza  na  kuambatanisha   viambatanisho   nilivyoeleza   hapo   juu. Fomu  hizi  unazikuta  kulekule  manispaa.   Bei  ya  fomu  hizi   ni  Tshs  1 000/=  ( Alfu  Moja  tu ). Tukutane   tena  katika   uendeshaji   wa  kampuni.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

1 comment:

  1. Hellow.
    asante sana kwa elimu unayotupa kwa kutuelewesha kuhusu kufungua kampuni nk.

    Naomba kitu kimoja,nahitaji kuelimishwa kujua jinsi kampuni inavyolipa kodi na taratibu za kikodi za kampuni.

    Kwa maana kuna kampuni natarajia kupewa niisimamie mkoani Kilimanjaro.

    Natanguliza shukurani.

    Nitashukuru ukinitumia kwa email binafsi.

    badvocalz@yahoo.com

    ReplyDelete