Monday, January 5, 2015

MAALIM SEIF AKIZINDUA MRADI WA MAJI SAFI,PEMBA

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, alipofika eneo la Vikunguni kwa ajili ya kuzindua mradi wa maji safi na salama katika eneo hilo.
Bango la mradi wa maji Vikunguni baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mradi huo.
Baadhi ya wananchi pamoja na wakandarasi wa kampuni ya SINO-HYDRO LTD ya China, wakimsikiliza Maalim Seif wakati akiwahutubia wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama katika eneo la Vikunguni.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiagana na wananchi baada ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama katika eneo la Vikunguni. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad (OMKR).

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuimarika kwa huduma za maji safi na salama nchini kutasaidia harakati za uzalishaji pamoja na shughuli za kiuchumi.

Umesema huduma hiyo pia husaidia kuokoa muda hasa kwa akinamama ambao mara nyingi hukabiliwa na jukumu la kutafuta maji kwa matumizi ya nyumbani.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati akifungua mradi wa maji safi na usafi wa mazingira katika eneo la Vikunguni jimbo la Wawi katika Wilaya ya Chake Chake, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ameelezea kufarajika kwake kutokana na mradi huo kuanza kuwanufaisha wananchi wengi wa eneo hilo pamoja na vijiji jirani.

Amefahamisha kupatikana kwa huduma hiyo ya uhakika, pia kutasaidia kujikinga na maradhi ya miripuko yakiwemo kipindupindu ambayo mara nyingi husababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.

Amewasisitiza wananchi kuulinda na kuutunza mradi huo, ili uweze kuwa endelevu na kuweza kutumika kwa muda mrefu.

Sambamba na hilo Maalim Seif amewataka wananchi hao kuepukana na uharibifu wa mazingira, ili kujikinga na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kusababisha kukauka na kuchafuka kwa vyanzo vya maji.

Ameeleza kuwa tayari vijiji kadhaa vya Zanzibar kikiwemo kijiji cha Nungwi, tayari kimekumbwa na athari hizo kwa visima vyao kuingiliwa na maji ya chumvi, na kuvitaka vijiji vyengine kuchukua tahadhari juu ya athari kama hizo.

Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdallah Shaaban, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wa Zanzibar wanapata maji kwa asilimia 85 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Amesema tayari ujenzi wa miradi ya maji mijini na vijijini umeshafikia asilimia 90 ambapo kazi ya usambazaji inaendelea vizuri.

Akisoma taarifa ya kitaalamu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Mustafa Aboud Jumbe, amesema zaidi ya shilingi bilioni mbili nukta tatu zimetumika kukamilisha mradi huo wa maji Vitongoji.

Amesema mradi huo ulioanzishwa mwaka 2011 ulijengwa chini ya ukandarasi wa kampuni ya SINO- HYDRO ya China, na uligharamiwa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), UN-Habitat na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Amefahamisha kuwa Serikali imo katika utaratibu wa kulipatia ufumbuzi tatizo la umeme katika visima na matangi ya maji ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inapatikana kwa uhakika.

Katika risala yao wananchi hao wa Vikunguni wameishukuru Serikali na washirika wa maendeleo kwa kuwapelekea mradi huo ambao umeondosha kero ya upatikanaji wa maji safi na salama iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment