Wednesday, January 28, 2015

January Makamba na ndoto ya vituo vya Michezo vya Kanda

Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Bumbuli na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Masoko ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambaye hivi karibuni pia ametangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa January Makamba(Pichani juu)  hivi karibuni ameainisha adhma yake ya kuinua kiwango cha michezo nchini.

Azma hizo zimo katika  katika mazungumzo yake na Padre Privatus Karugendo ambayo yamechapishwa katika kitabu ambacho gazeti hili imekipata nakala yake ambapo ameainisha azma ya kujenga vitua vya michezo vya kanda vyenye hadhi ya kiolimpiki.

Kwenye kitabu hicho, Makamba amejibu swali kwamba kitu gani kifanyike ili Watanzania waweze kujivunia wanamichezo wao. Makamba alisema, “Inafedhehesha sana kuona kwamba asilimia 79 ya Watanzania walikuwa hawajazaliwa mara ya mwisho tumeshiriki katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika.

Mwaka huo huo wa 1980 ndio mara ya kwanza na ya mwisho tuliweza kushinda medali za Olimpiki. Rafiki yangu Mzee Suleiman Nyambui na Mzee wetu Filbert Bayi ndio walitutoa kimasomaso kipindi kile. Ni muhimu kurekebisha hili.” 

Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania imekuwa kama kichwa cha mwendawazimu katika medani ya kimataifa huku tasnia ya michezo ikiendelea kugubikwa na migogoro isiyokwisha. Kutokana na migogoro hii, Tanzania inaendelea kupoteza matumaini ya kung’aa katika medani za kimataifa.

Katika mazungumzo hayo na Padre Karugendo, Makamba  alinukuliwa akisema, “Lazima tutambue kwamba maendeleo ya michezo yanatokana na vitu muhimu vitatu. Kwanza, ni lazima kuwepo na vipaji, bahati nzuri nchi yetu ina vipaji vya kutosha katika aina zote za michezo. Pili, ni miundombinu na mfumo wa kubaini na kuviendeleza vipaji hivyo, hii  bado ni changamoto . Tatu, ni utawala, uongozi, na uendeshaji wa tasnia ya michezo, hii pia ni changamoto. Hivi vitu vitatu ni lazima viwepo ili tuweze kupata mafanikio kwenye medani ya michezo.”

Kama mgombea wa kwanza kutangaza nia yake ya kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, Makamba anaungwa mkono na vijana wengi kutokana na kuendesha siasa zake kisasa, kibunifu na kuepuka malumbano ya jukwaani.

Katika mazungumzo hayo Makamba alielezea fikra zake alizonazo hasa hasa kwenye kuendeleza vipaji vya Watanzania ambapo alisema, “Ni lazima tuanzishe vituo vikubwa vya michezo au ‘sports academies’ kwenye kila kanda ya nchi yetu vyenye hadhi ya Kiolimpiki.” 

Makamba aliongeza  kwamba, “Kutakuwa na vituo sita vya aina hii katika nchi yetu ambavyo vitazungukwa na shule za msingi na sekondari za ‘boarding’. Vituo hivi vitakuwa na lengo la kukusanya wanafunzi wote kwenye kanda husika ambao wameonekana kuonyesha vipaji ambavyo vinapaswa kuendelezwa. Ukweli ni kwamba bila kuendeleza vipaji katika mazingira mazuri, basi tusahau kabisa kufanya vizuri kwenye michezo. Hili linaweza kufanywa kwa ushirikiano wa serikali na sekta binafsi”.

Mheshimiwa January Makamba anakuwa mgombea wa kwanza wa Urais kuweka bayana mipango yake ya Tanzania Mpya katika maandishi. Anaendelea kufunguka kwamba katika tasnia ya michezo ni muhimu sana kuwekeza katika watoto. Zaidi ya hapo, kila timu ya ligi kuu ni lazima iwe na akademi na TFF iendeshe ligi kuu ya timu za watoto.

“Tufikie wakati ambapo timu za taifa za miaka 10 ijayo ziwe zinaandaliwa kuanzia sasa, na serikali itenge bajeti kila mwaka kwa timu hizo  ili kuziwezesha kukaa kambini, kufanya mechi za majaribio na kuziwezesha kushiriki kikamilifu katika mashindano ya kimataifa. Mimi sio muumini wa hizi kamati za zimamoto kusaidia timu ishinde ghafla ghafla wakati siku zote watu hawafanyi maandalizi ya muda mrefu” alimalizia Makamba.

Makamba pia aligusia kuhusu suala la ukata na ufinyu wa bajeti unaokabili tasnia za michezo. Siku zote tunaona timu za taifa za olimpiki au jumuiya ya madola kukosa fedha za kukaa kambini ambapo huchangia katika matokeo hafifu.

“Huko nyuma, taasisi na mashirika ya umma yalikuwa na timu za michezo zilizokuwa zinafanya vizuri na kutoa michango kwenye maendeleo ya michezo. Kwa mfano, Pamba ya Mwanza, Sigara, Reli ya Morogoro, ushiriki huu ulichangamsha sana michezo na ni lazima turudishe utamaduni huu,” alimalizia Makamba. 

1 comment: