Na Bashir Yakub
Ni ukweli usiofichika kuwa biashara
na ujasirimali kwa pamoja
vimekua kwa kiwango kikubwa. Hili linatokana
na sababu nyingi ikiwemo ya kukua kwa biashara za kimataifa, maendeleo ya
mawasiliano, marekebisho ya baadhi ya sera za nchi na sababu nyinginezo. Hali hii imeleta ugumun kwa wanaofanya biashara nje ya kampuni. Si rahisi kufanikiwa
katika biashara bila kuifanya biashara yako katika mtindo wa kampuni. Hata iwe
ndogo ya kuuza mayai au kufuga kuku mafanikio zaidi ni pale biashara hiyo
utakapoifanya kampuni. Ni kutokana na umuhimu wake ikanilazimu niwajuze, hasa vijana wenzangu, kuhusu kampuni tukijielekeza zaidi katika aina
na uundwaji wake kutokana na Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002.
KAMPUNI NI NINI
Awali ya yote tujue nini maana ya kampuni.
Kwa ufupi sana
twaweza kusema kuwa, Kampuni ni muunganiko
wa kibiashara wa mtu zaidi ya mmoja ulioundwa na kusajiliwa chini ya
Sheria ya Makampuni 2002.
Katika maana hii tunaona kuwa lazima uwe
muunganiko wa watu. Waweza kuwa wawili, watatu na kuendelea. Hii ina maana kuwa
hakuna kampuni ya mtu mmoja. Lazima awe zaidi ya mmoja, uwe na mke wako au mume wako au na rafiki, au
na mtoto wako itategemea lakini huwezi kuwa mmoja.
Pili, lazima iwe imesajiliwa chini ya sheria ya makampuni kama nilivyoonesha. Hiyo
ndio itaitwa kampuni. Zaidi ya hapo hicho ni kitu kingine na sio kampuni.
AINA
ZA KAMPUNI
Kabla hatujaingia katika mchakato wa kuunda
kampuni ni vema kabisa tukajua kuna aina ngapi za kampuni. Hii itakusaidia
kujua sifa za kila kampuni na aina ya kampuni unayotaka. Makampuni
yamegawanyika katika mgawanyo ufuatao.
( a
) Kampuni ya umma (public company). Kampuni hii ni ya umma kama jina lake lilivyo .
Imeitwa kampuni ya umma kwasababu kuu
kuwa unapounda kampuni hii kila mtu au
kila mwanaumma,mwanajamii anaruhusiwa
kuomba uanachama ikiwa tu atatimiza masharti kadhaa. Uanachama katika kampuni ndio
umiliki. Ukisikia mtu mwanachama ( member) ni mmiliki. Na umiliki au uanachama unatofautiana kutokana
na kiasi cha hisa anazomiliki mtu. Hivyo
katika kampumi hii huwezi kumzuia mtu kuwa mmoja wa wamiliki, yeyote mwenye
uwezo awe adui yako au rafiki ilimradi umesajili kampuni kama
ya Umma atakuwa pamoja nawe katika
umiliki wa kampuni.
Pili, ili kampuni ya umma ianzishwe ni lazima iwe na wanachama
wasiopungua saba. Wanachama wakiwa sita , watano na kushuka hawawezi kuanzisha
kampuni hii.
Tatu,Wakurugenzi wake wanaanzia wawili, hii
ni kusema mtu mmoja hawezi kuwa mkurugenzi katika kampuni hii.
Nne, ni kuwa hisa zake ni huru. Hii ina
maana kuwa hisa zinaweza kuhama kutoka
kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Mwanachama mmoja anaweza kumuuzia mwanachama mwingine hisa zake zote au kiasi.
Kila mtu yuko huru na hisa zake anaweza
kumuuzia mwingine au akampa zawadi, haizuiwi.
( b
) Kampuni binafsi(private company). Hii ni aina ya kampuni ambayo watu wengi
huunda.Karibia asilimia kubwa ya makampuni tunayoyaona ni ya binafsi. Kampuni binafsi zina sifa
zifuatazo.
Pili,hisa zake hazihamishiki kirahisi. Ina
maana kuwa huwezi kuuza au kugawa hisa zako kwa mtu mwingine bila ridhaa ya
wanachama wengine. Kwa kuwa ni kampuni binafsi
mtu yeyote anayeingia lazima awe
amekubalika kwa wanachama wengine pengine asiwe adui au yeyote
asiyehitajika.
Tatu, inakatazwa kwa kampuni binafsi
kuwaalika au kuwaita watu kuja kununua hisa.
Nne, inawezekana kuwa hata na mkurugenzi
mmoja. Si lazima wawe wawili au zaidi hata mmoja anatosha.
(c )
Kampuni za kisheria(statutory company). Hizi ni
kampuni zinazoanzishwa na sheria maalum za bunge. Mara nyingi kampuni hizi
huundwa ili kutimiza majukumu maalum katika jamii hasa huduma za kijamii.
Taasisi nyingi za serikali pamoja na mashirika ya umma huwa ni kampuni za aina
hii.
Kwa uchache ni hizo.
JINSI
YA KUUNDA KAMPUNI
Huu ndo mzizi wa mada kwakuwa wengi
wangependa kujua ni kwa taratibu zipi
kampuni inaweza kuundwa .Kwetu hapa Tanzania kampuni inaundwa kwa
kufuata utaratibu huu.
( a
) Kwanza kabisa ni kuchagua jina la kampuni. Kampuni lazima
iwe na jina linalotambulika. Hatua hii huwa inaitwa Name Search ambapo
unatakikwa kuandika barua kwa msajili wa makampuni kwa Dar es salaam ni pale
mnazi mmoja jengo la ushirika. Utaeleza jina la kampuni yako. Hii husaidia
kutokuwa na majina yanayofanana baina ya makampuni. Majina ya makampuni yote
yapo kwa msajili wa makampuni hivyo si rahisi kampuni zaidi ya moja kuwa na
majina yanayofanana.
Msajili wa makampuni baada ya utafiti
atajibu kama jina hilo
halipo uendelee nalo au lipo uachane nalo.
( b
) Baada ya jina kuwa limethibitishwa hatua inayofuata ni kuwasilisha kwa msajili
wa makampuni waraka wa kampuni na katiba ya kampuni. Waraka wa kampuni
(memorandum of association) ni waraka
maalum uliosainiwa na wanachama wote ambao hueleza na kuchambua kile ambacho
kampuni itakifanya. Shughuli za kampuni zinatakiwa kuelezwa vyema ndani ya
waraka huu. Waraka huu lazima uwe na mhuri wa mwanasheria.
Katiba ya kampuni kwa upande mwingine(article
of association) nayo lazima iwe imesainiwa na wanachama wa kampuni . Katiba
ndiyo inayoeleza uendesahaji mzima wa
kampuni . Inaeleza haki na wajibu wa
wanahisa, uongozi wa kampuni, mgao wa mapato, nguvu na mamlaka ya
wakurugenzi, mikutano na utaratibu wake,
umiliki na ugawaji wa hisa, uhamisho wa hisa n.k. Hii nayo lazima iwe
imesainiwa na mwanasheria.
( c
) Lazima kupeleka kwa msajili wa makampuni
maelezo(statement) yanayowahusu wakurugenzi wa kampuni. Katika maelezo hayo
wasifu wa wakurugenzi unatakiwa kuwa umeelezwa vyema.
(
d ) Lazima
pia ijazwe fomu maaalum yenye maelezo yanayohusu anuani kamili ya ofisi za
kampuni.Anuani hapa sio tu S.L.P bali wapi ofisi za kampuni zilipo
inakoendeshea shughuli zake.
( c
) Pia lazima
ijazwe fomu maalum ambayo ipo kama kiapo
kuonesha kuwa matakwa yote ya kisheria yametimizwa hivyo kampuni inatakiwa kupatiwa usajili.
Fomu hiyo inajazwa na wakili au mtu yeyote ambaye jina lake
limetajwa katika katiba kama mkurugenzi wa kampuni au katibu wa kampuni. Fomu hii
inakuwa ni ushahidi kuwa matakwa yote yametimizwa kwa ukamilifu.
Baada ya hapo kampuni inaweza kusajiliwa
kwa kupewa cheti cha kuzaliwa.
Taratibu zote hizi ikiwa ni pamoja na
kuandaa katiba, fomu na waraka kwa wepesi zaidi hufanywa kwa wanasheria.
Kwa kumalizia nishauri kuwa kufanya
biashara kwa mtindo wa kampuni ni muhimu sana kuliko ambavyo baadhi ya watu wanaweza
kufikiria.Na karibia biashara zote za kisasa hufanyika kwa mtindo huu.
Asikudanganye mtu kuwa atatoka mfanyabiashara ulaya , Amerika au hata hapa
nchini mfanyabiashara mkubwa ambaye atakubali kufanya biashara na mtu binafsi .
Labda iwe biashara ya kukufanya kibarua.
Makampuni yote ya nje au ndani huwa
hayafanyi biashara na watu binafsi isipokuwa tu mmejiunga na kuwa kampuni. Na
hapa nieleweke vyema kuwa ninaposema biashara simaanishi biashara kubwa saana.
Hapana ninamaanisha biashara hiyohiyo ndogo unayoifanya. Biashara yako ya
ufugaji kuku kama nilivyosema usikubali kuifanya kama mtu binafsi, biashara ya
kuuza maziwa usikubali kuifanya kama mtu binafsi vivyohivyo biashara yako ya
duka, biashara yako ya huduma ya pesa
kwa njia ya simu, kuuza mazao, kijiwe chako cha ufundi magari au seremala na biashara nyingine ndogo zote usizifanye
wewe kama wewe.
Ukweli ni kuwa hakuna atayekupa kazi ya
maana kama wewe ni mtu binafsi.Biashara ya
sasa haifanywi hivyo. Usikwamishe kukua kwa biashara zako... Unda kampuni sasa!
Mwandishi
wa makala ni Mwanasheria na mshauri wa masuala ya sheria kupitia gazeti la
serikali Habari leo la kila jumanne, gazeti Jamhuri kila jumanne, na Nipashe kila
jumatano.
0784482959
0714047241
bashiryakub@ymail.com
Nimefurahishwa sana na makala yako nzuri na ya kuelimisha. Nina swali moja, ikiwa niliwahi kusajili kampuni zaidi ya miaka kumi iliyopita na sikuwahi kufanya biashara yoyote toka muda huo, na sasa nina wazo la kuanza upya na kuboresha jina la biashara. Kipi kitakuwa rahisi kwangu kusajili kampuni upya au kubadili jina la usajili wa awali? Tafadhali naomba ufafanuzi!
ReplyDeleteNaam! Nimefarijika na makala hii, asante msomi.
ReplyDeleteAsante kwa ufafanuzi
ReplyDeleteNilikuwa natafuta namna ya kusoma kuhusu kampuni uanzishaji na uendeshaji wake asante sana
ReplyDeleteAsante umenisaidia kwa kiwango flani
ReplyDelete