Friday, December 5, 2014

Balozi Seif Idd awaasa wana CCM Zanzibar kuacha tabia ya kupuuza mambo yanayowahusu,ili wasije jutia baadae

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif kizungumza na Viongozi wa Kamati ya Siasa ya Tawi la CCM Upenja.Kushoto yake ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “ B” Nd. Hilika Khamis na kulia yake ni Mwenyekiti wa Tawi la CCM Upenja Nd.Daudi Hasnuu Khamis.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa na Mabalozi wa Nyumba Kumi wa Tawi la CCM Upenja wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani alipokuwa akizungumza nao kwenye ukumbi wa Tawi la hilo Upenja.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe Zanzibar Nd. Said Sarboko Makarani akimfahamisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hatua zilizochukuliwa za kuheshimu hifadhi ya urithi wa Kimataifa wakati wa ujenzi wa Hoteli ya Park Hyatt iliyopo Forodhani Mjini Zanzibar. Nyuma ya Nd. Sarboko ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi, Kulia ya Balozi ni Naibu Waziri wa Ardhi, Maji Nishati na Madini Mh. Haji Mwadini pamoja na Mratibu wa Mradi wa Hoteli ya Park Hyatt Bwana Yaqoub Osman.
Balozi Seif akikagua moja ya vyumba vya watu Mashuhuri { VIP } kwenye Hoteli ya Park Hyatt na kuridhika na kiwango kilichofikiwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkonhwe Zanzibar Nd. Said Sarboko Makarani akikagua hitimisho la ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Park Hyatt hapo Forodhani Mjini Zanzibar. Hoteli hiyo inatarajiwa kufunguli wa rasmi kwenye shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 51 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar zinazotarajiwa kuanza rasmi mapema mwezi ujao wa Januari 2015. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wameonywa kuacha tabia ya kupuuza mambo  yanayowahusu ambayo hatma yake inaweza kuwaletea majuto ya kudumu katika maisha yao ya baadae.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati ya Siasa na Mabalozi wa nyumba Kumi wa Tawi la CCM Upenja Wilaya ya Kaskazini “ B”.

Balozi Seif akiwa katika ziara ya kutekeleza agizo la Chama Wilaya ya Kaskazini        “ B” la kufanya mikutano ya kuhamasisha wana CCM juu ya umuhimu wa daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na kura ya maoni   alisema CCM bado inakubalika na Watanzania walio wengi, lakini chakushangaza ni uvuvu wa wanachama hao katika kuitika maagizo ya viongozi wao.

Alisemja imani ya wananchi wengi nchini inatokana na ilani na sera za Chama cha Mapinduzi walizoziridhia wakati wa uchaguzi uliopita wa mwaka 2010 na kuonyesha ustawi wa maisha yao katika utekelezaji wake.

“ Wana CCM wakiendeleza tabia ya kupuuza masuala yanayowahusu likiwemo suala la upigaji kura kwenye chaguzi mbali mbali iko siku watakuja juta. Hivyo wasijemlaumu mtu kwani majuto ni mjukuu “. Alisema Balozi Seif.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwakumbusha Viongozi hao wa Kamati ya Siasa na Mabalozi wa Tawi la CCM Upenja kuwasimamia vyema wanachama wao katika zoezi la uwandikishaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura mapema mwakani.
Alisema ni busara kwa wtu wote hasa vijana waliofikia umri wa kupiga kura wanelimishwa kuitafuta  fursa hiyo kwa lengo la kutumia haki yao ya kidemokrasia.

Akigusia suala la kura ya Maoni inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa April Mwaka ujao Balozi Seif alisema ni jukumu la kila kiongozi  kuhakikisha kwamba wananchi wanaowaongoza wanashiriki vizuri  kwenye zoezi hilo.

Alisema upigaji kura hiyo ndio njia pekee itakayothibisha kwamba wanachama na wananchi hao wametumia haki yao ya kidemokrasia kufuatia maoni waliyoyawasilisha kwenye tume ya maoni ya Katiba na hatimae kupatikana kwa kwa Katiba inayopendekezwa.
Wakitoa michango yao baadhi ya Viongozi hao wa Kamati ya Siasa ya Tawi la CCM Upenja walisema tabia ya baadhi ya viongozi kusubiri vipindi vya kampeni wakajumuika na wananchi unafaa kupigwa vita kwa nguvu zote.

Walisema kitendo hicho ambacho imekuwa kilema kwa viongozi wengi kupuuza wananchi waliowachagua kinachangia kupunguza kasi ya maendeleo katika utekelezaji wa Ilani na sera zake pamoja na kuwahudumia wananchi.

Wajumbe wa Kamati hiyo ya siasa pia waliwakumbusha viongozi wenye kuweka ahadi kuhakikisha kwamba dhima hiyo wanaitekeleza ili kuwepuka dhambi inayoweza kuwaandama wakati wanapotaka kuona tena nafasi ya uongozi.

Balozi Seif akiwa Mbunge wa Jimbo la Kitope katika Mkutano huo aliwaahidi vijana wa michezo wa Kijiji cha Upenja kuwapatia Fedha taslim shilingi 700,000/- ndani ya saa 24 kwa ajili ya kununulia viata vitakavyowasaidia katika michezo na mashindano ya soka wanayoshiriki.
Wakati huo huo Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya sherehe na maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alitembelea na kukagua hatua za mwisho za ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Park Hyatt iliyopo Forodhani Mjini Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe Zanzibar Nd. Said Sarboko Makarani alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ujenzi wa Hoteli hiyo umezingatia mazingira halisi ya hifadhi ya Mji Mkongwe likiwemo jengo lililokuwa ofisi ya Mrajisi wa Vizazi na vifo ambalo linaendelea kubakia katika mazingira yake ya kiasili.

Nd. Sarboko alisema Uongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni { UNESCO } lilikuwa makini katika kufuatilia ujenzi wa Hoteli hiyo kwa kuzingatia kwamba Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa miaka kadhaa sasa umekuwa miongoni mwa miji iliyopewa hadhi ya kuwa urithi wa Kimataifa.
Mkurugenzi huyo wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe alifahamisha kwamba kazi hiyo ilikwenda sambamba na uhifadhi ya eneo la fukwe iliyopo pembezoni mwa Hoteli hiyo ambayo hutoaa mandhari nzuri na ya kuvutia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Hoteli hiyo na kuupongeza uongozi wa Hoteli hiyo pamoja na wahandisi wa ujenzi huo kutoka Kampuni ya Kimataifa ya  Ujenzi kutoka Jamuhuri ya watu wa China ya CRJ.

Hoteli hiyo yenye hadhi ya kiwango cha Kimataifa inatazamiwa kufunguliwa rasmi katika shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 zinazotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi wa Januari mwaka ujao.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/12/2014.

No comments:

Post a Comment