Monday, November 3, 2014

Nidhamu ya Bodaboda jijini Hanoi, Vietnam, ni mfano wa kuigwa

Kwa yeyote atayetembelea jiji la Hanoi, makao makuu ya nchi ya Vietnam, lazima atakumbana na changamoto ya bodaboda, hasa hasa kama ataamua kutembea kwa miguu. 
Hanoi, moja ya majiji lenye watu wengi duniani (inakadiriwa kuwa na wakaazi zaidi ya milioni 7), lina mambo yake katika usafiri.
 Idadi ya pikipiki katika jiji la Hanoi, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1996, na kutokana na kukua haraka kwa uchumi wake, zilikuwa milioni 4. Leo hii inakadirika kuwa jijini humo peke yake kuna zaidi ya bodaboda milioni 4. 
Na kwa nchi nzima inakadiriwa kuna bodaboda milioni 39. Hapo ukiondoa vikongwe na watoto, inamaanisha kila mtu wa Vietnam ana pikipiki yake. 
Hivi majuzi nilibahatika kutembelea Hanoi, na kujionea kwa macho yangu wingi wa bodaboda jijini humo. Lakini kwa mastaajabu yangu, pamoja na wingi mkubwa wa usafiri huo kila mahali, sikupata kushuhudia hata ajali moja katika wiki nzima niliyokaa Hanoi. 
Nikawa najiuliza kwa nini hakuna ajali wakati kuna bodaboda kibao. Nikagundua kwamba asilimia takriban 85 ya waendesha pikipiki jijini Hanoi ni watu wenye nidhamu ya hali ya juu. Tofauti ya miji kama Dar es salaam, Arusha, Mwanza ama Mbeya, waendesha pikipiki wa Hanoi, pamoja na wingi wao, wanaheshimu sana sheria za usalama barabarani. 
Ni nadra sana kuona bodaboda linakatisha kwenye taa nyekundu! Vile vile mwendo kasi ni nadra sana pia. Ukiacha sifa za uchapakazi na utii wa sheria vinavyoifanya Vietnam ikue haraka sana kiuchumi (miaka 15 tu iliyopita wao walikuwa hawana tofauti sana na Tanzania tulivyo leo), NIDHAMU ya barabarani ni mfano wa kuigwa kwa kweli.
 Mfanyabiashara wa samaki hai akiwa amepaki pembeni kujibu ujumbe katika simu katikatinya jiji la Hanoi
 Baba akiwapeleka watoto wake shule bila wasiwasi
 Misururu ya bodaboda jijini Hanoi
 Nidhamu ya utii wa sheria za usalama barabarani ni mfano wa kuigwa kwa nchi ya Tanzania ambako waendesha pikipiki hawana muda wa kusimama kwenye taa nyekundu kama wafanyavyo hawa wenzetu hapo pichani
 Bodaboda ni nyingi kulikom magari jijini Hanoi. Lakini ajali ni za nadra mno
 Kila pembe ya jiji la Hanoi mambo yako hivyo
 Taa nyekundu imewaka na kila mmoja anatii kwa kusimama kungoja ya kijani
 Kama si pikipiki basi usafiri mbadala jijini Hanoi ni Taxi
 Sehemu ya jiji la Hanoi
 Kwa haraka haraka unaweza kudhania hapa ni Kariakoo, Dar es salaam
 Nidhamu ya waendesha pikipiki ni mfano wa kuigwa
 Taa nyekundu na kila mwendesha pikipiki kasimama
Baiskeli na pikipiki zote zinatii sheria za usalama barabarani kwa kusimama penye taa nyekundu.

No comments:

Post a Comment