Monday, November 3, 2014

Baraza la michezo ya Majeshi Tanzania ladhamiria kutatua changamoto ya michenzo nchini

Wajumbe wa Kamati Tendaji ya BAMMATA katika picha ya pamoja mara baada ya kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika jijini Mbeya katika Bwalo la Magereza la Chuo Ruanda.Wa tatu kutoka kushoto mstari wa mbele ni mwenyekiti wa Baraza hilo Brigedia Jenerali CIRIL MHAIKI.

Tanzania imekuwa haifanyi vizuri sana katika michezo mingi ya Kimataifa inayoshiriki kwa hivi sasa.Hii inatokana na changamoto nyingi zinanazoikabili Taifa  miongoni mwake ikiwa ni kutokuwapo kwa   michezo ya majeshi kama ilivyokuwa hapo awali. 

Michezo hiyo ambayo ilikuwa inasimamiwa na Baraza la michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) ilikuwa inatumika kubaini na kuendeleza vipaji vya wanamichezo wanajeshi ambao walitumika kuitangaza Tanzania kimichezo nje ya nchi na hivyo kuliletea heshima na sifa maridhawa Taifa letu.

Baadhi ya wachezaji walioliletea taifa sifa kwa uchache ni pamoja na Filbert Bay, Juma Ikangaa, Samson Ramadhan, Iswege Christopher,Nasser Mafuru, Samuel Mwang’a , Hitii Shamba na Restuta Joseph ambao wote ama wametokea Majeshini au wamepata mafunzo na wakufunzi wa majeshini.


Nchi yetu ilisifika sana katika michezo mbalimbali kama vile riadha,ngumi,mieleka,mpira wa miguu,mpira wa kikapu,mpira wa mikono,mpira wa pete,mpira wa ukuta, shabaha na mpira wa wavu. Mafanikio ya michezo hiyo yote yalitokana ama na wanamichezo wa majeshi wenyewe kushiriki, au wanamichezo raia kupata mafunzo na mazoezi kwa msaada wa majeshi.

Kutokana na hali ya kimichezo kudorora, BAMMATA chini ya Mwenyekiti wake Brigedia Jenerali Cyrili Mhaiki wamedhamiria kuchukua hatua  za dhati na madhubuti kupambana na changamoto  za michezo nchini ili kuyafanya majeshi yetu kuwa kitalu cha kukuza na kuendeleza michezo nchini na hivyo kulirudishia Taifa heshima yake ya hapo awali.

Brigedia Jenerali Mhaiki na jopo zima la kamati tendaji ambayo inashirikisha viongozi waandamizi wa michezo kutoka majeshi yote na vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoka Tanzania Bara na Zanzibar katika mfumo wa Kanda za NGOME, JWTZ VISIWANI,Jeshi La Kujenga Taifa, Polisi, Magereza, Idara ya Zimamoto na Uokoaji, Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo (KMKM), Jeshi La Kujenga Uchumi (JKU), Kikosi Cha Valantia (KVZ), Uhamiaji, Mafunzo, Kikosi Cha Zimamoto Na Uokozi (KZU), katika muendelezo wa utekelezaji wa mikakati ya maboresho katika michezo ya Baraza hilo, hivi karibuni walikutana jijini Mbeya katika Bwalo la Magereza la Chuo Ruanda ili kujadili mambo mbalimbali ya kimkakati ya kutatua changamoto  ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya michezo nchini kwa ujumla wake.

Moja ya mambo muhimu ambayo Kamati tendaji hiyo iliyafanya ni kuiangalia upya katiba ya Baraza hilo na kudhamiria kuifanyia marekebisho makubwa na thabiti ambayo yataendana na mahitajio ya sasa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na hivyo kuliongoza Baraza hilo na kulifanya liwe lenye nguvu na imara katika Nyanja mbalimbali za  michezo nchini. Katiba hiyo inatarajiwa kuwa ndio muarobaini wa kutatua changamoto zote  ambazo zinarudisha nyuma juhudi za kuendeleza michezo majeshini na kwa jamii nzima kwa ujumla.

Brigedia Jenerali Mhaiki aliweka wazi madhumuni na shabaha ya Katiba na kusisitiza kuwa itasaidia sana kuleta ushirikiano na Mabaraza ya Michezo ya taifa na vyama vya michezo vya taifa ili kuendeleza michezo kwa ujumla katika majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Bara na Visiwani.

Pamoja na dhamira hiyo, Kamati hiyo tendaji imeazimia kurudisha ushiriki wa majeshi katika michezo ya BAMMATA ambayo hapo awali ilikuwa inafanyika kila mwaka. Aidha, mpango mkakati mwingine ni kuhakikisha ushiriki chanya wa majeshi katika michezo hii ikiwa ni kukuza elimu ya viungo na utimamu wa  mwili na michezo miongoni mwa majeshi yetu, kubadilishana uzoefu na kuendeleza utaalam ili kuinua vipaji vya michezo kwa wanachama wake na jamii kwa ujumla.

BAMMATA imedhamiria kutekeleza hilo kwa kushirikiana na mashirikisho ya michezo ya Majeshi Afrika Mashariki, Kikanda (Kusini Mashariki mwa Afrika), Afrika na Duniani (CISM), ambayo Tanzania ni mwanachama HAI. Dhima ni kuona kuwa  BAMMATA linasimamia mafunzo ya utawala na uongozi katika michezo, Ukufunzi (ukocha), kubaini na kuinua vipaji na Tiba kwa wanamichezo  pamoja na  kuifufua michezo yote ambayo imesahauliwa na kuiendeleza kwa nguvu kubwa ili vijana walio majeshini na uraiani wajifunze na washindanishwe kwa motisha mbalimbali zitakazotolewa kwa washindi.

Katika mtazamo yakinifu, Baraza hilo chini ya uongozi wa Brigedia Jenerali Mhaiki limewakikishia wananchi  kuwa, kwa maelelekezo na  ushirikiano na ngazi za juu litatumia ubunifu, uwezo na maarifa yote ya viongozi katika majeshi kuhakikisha mikakati yote iliyopangwa inatekelezwa kwa asilimia mia na kujitoa kadri ya uwezo wao kushawishi na kuhakikisha michezo Majeshini inarudi kama awali na taifa zima linapata mwamko wa kutosha.

No comments:

Post a Comment