Friday, October 24, 2014

Wanafunzi Taasisi ya Mufunzo Uanasheria kupata mikopo - Dkt. Migiro

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro akikagua Jengo la Mahakama ya Mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania leo (Ijumaa, oktoba 24, 2014) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na kulia ni Mkuu wa Taasisi hiyo Jaji Dkt. Gerald Ndika.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro akikagua Jengo la Mahakama ya Mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania leo (Ijumaa, oktoba 24, 2014) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na kulia ni Mkufunzi wa Taasisi hiyo Bw. Goodluck Chuwa.
Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania Jaji Dkt. Gerald Ndika (kulia) akiongea na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro nje ya Jengo la Mahakama ya Mafunzo katika Taasisi hiyo leo (Ijumaa, oktoba 24, 2014) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na kulia ni Mkufunzi wa Taasisi hiyo Bw. Goodluck Chuwa. (Picha na Martha Komba, Wizara ya Katiba na Sheria).

Serikali inakamilisha taratibu za kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria unaolenga kurekebisha Sheria ya Bodi ya Mikopo ili kuwawezesha wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) kupata mikopo kwa ajili ya mafunzo yao.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Asha-Rose Migiro amewaambia wanafunzi wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa, Oktoba 24, 2014) kuwa lengo la Serikali kukamilisha mchakato huo katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa.

"Nafahamu kuna changamoto ya baadhi yenu kukosa mikopo, nimeambiwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa Taasisi hii Bw. George Masaju kuwa taratibu za kurekebisha Sheria ya Bodi ya Mikopo umeanza ili wanafunzi wa taasisi wapate mikopo,” amesema Dkt. Migiro.

Waziri Migiro, ambaye aliongozana na Naibu wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na Bw. Masaju, amezungumza na wanafunzi wa Taasisi hiyo iliyopo nyuma ya Jengo la Mawasiliano (Mawasiliano Towers) jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake ambayo ni ya kwanza tangu ateuliwe na Mhe. Rais kuiongoza Wizara ya Katiba na Sheria, Waziri Migiro alikagua ujenzi wa majengo ya kudumu ya taasisi hiyo pamoja na kukutana na watumishi na wanafunzi ili kubadilishana mawazo.

Ujenzi wa majengo hayo ya kisasa ya kudumu, ulianza Mwezi Novemba, 2010 na kukamilika Agosti, 2012 na umegharimu zaidi ya Tshs 16.1/- Bilioni na umefanywa na Serikali kupitia Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria (LSRP) iliyokuwa inatekelezwa chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Ujenzi huo umejumuisha Mahakama ya Mafunzo, Maktaba, Madarasa, Jengo la Utawala, Ukumbi wa shughuli mbalimbali na nyumba za watumishi.

Katika mazungumzo yake na wanafunzi hao, Dkt. Migiro pia aliwakumbusha wanafunzi hao kujiandaa kutoa huduma bora kwa jamii pale wanapohitimu kwa kuzingatia kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kuendesha mafunzo hayo.

“Mkumbuke ule wito wa Mwalimu Nyerere kuwa nyie ni kama yule mtu aliyetumwa na kijiji chenye njaa kwenda kutafuta chakula ili arudi kuwasaida wanakijiji wenzake,” alisema Waziri Migiro na kufafanua kuwa kuna wananchi wengi wanaohitaji huduma za kisheria nchini ambao wanawasubiri.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Jaji Gerald Ndika alimweleza Waziri Migiro kuwa tangu kuanza rasmi kwa mafunzo katika Taasisi hiyo mwezi Machi mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu, jumla ya wanafunzi 4,755 wamedahiliwa katika makundi tofauti na kati yao, wanafunzi 1,715 wamefaulu mafunzo na kupata cheti cha Stashahada ya Uzamili katika Utalaam wa Sheria (Post-Graduate Diploma in Legal Practice).

“Tunafurahi kuwa katika wanafunzi wetu 1,715 waliofaulu tangu kuanzishwa kwa Taasisi hii, wahitimu 1,540 wameorodheshwa kuwa Mawakili wa Kujitegemea baada ya kukamilisha taratbu na waliobaki wanaendelea kukamilisha taratibu,” alisema Jaji Dkt. Ndika.

Pamoja na mafanikio hayo, Mkuu huyo wa Taasisi amesema kumekuwa na malalamiko kuhusu ufaulu mdogo hususan katika hatua ya kwanza (first sitting) na kufafanua kuwa Bodi ya Uendeshaji chini ya Uenyekiti wa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeunda Kamati Maalum ili kufanya utafiti kwa lengo la kubaini kiini cha matokeo hayo.

“Bodi imeunda Kamati Maalum inayoongozwa na Prof. Bonaventure Rutinwa na inajumuisha wadau wengine kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama ya Tanzania, Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) na tunatarajia taarifa yake itakuwa tayari ifikapo mwanzoni mwa mwezi ujao wa Novemba, 2014” amefafanua Mkuu huyo wa Taasisi.

Akiongea katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju amesema lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ni kuwanoa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria ili kukabiliana na changamoto za sasa hususan katika taaluma ya sheria.

“Hapa wanafundishwa vitu vingi ikiwemo namna ya kujadiliana katika mikataba na mengineyo mengi ambayo kwa sasa ni changamoto,” amesema Bw. Masaju ambaye aliongozana na Wajumbe wa Bodi wakiwemo Mawakili Bw. Charles Rwechungura na Bi. Aisha Bade.

No comments:

Post a Comment