Tuesday, October 7, 2014

TMAA imeiwezesha Serikali kukusanya mrabaha wa jumla ya shilingi billioni 5.2

Na Georgina Misama-MAELEZO 

 Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) imeiwezesha Serikali kukusanya mrabaha wa jumla ya shilingi billioni 5.2 tangu kuanzishwa kwa wakala huo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi uzalishaji na usafirishaji wa madini Bwn Conrad Mtui wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembelea migodi ya Lugoba na Msolwa Chalinze, hivi karibuni.

“Wakala umefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 5.2 kutokana na madini hayo yaliyozalishwa na kuuzwa na wamiliki halali wa leseni katika mikoa mbalimbali kwenye kanda za Kaskazini, kati, Kusini, Kusini Maghalibi, Maghalibi, Mashariki na Ziwa Victoria” alisema Mtui.

Aidha,Wakala kwa kushirikiana na Ofisi za Madini ulibuni matumizi ya “Hati ya Mauzo” kwa lengo la kudhibiti shughuli za uzalishaji na mauzo ya madini, mkakati ambao ulianza kutumika mwezi Juni, 2011 utakaohusisha Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Pia, Wakala ulifanya ukaguzi na uhakiki wa madini yaliyozalishwa na kuuzwa na migodi mikubwa ya madini nchini, ikiwa na lengo la kupata mrabaha na takwimu sahihi za madini yaliyozalishwa na migodi hiyo.

Akitaja migodi iliyofanyiwa ukaguzi alisema ni Mgodi wa dhahabu wa Geita, Golden Pride, Bulyanhulu, Tulawaka, North Mara, Buzwagi na New Luika iliyowezesha kukusanywa kwa jumla ya Dola za Marekani milioni 427.98 Akizungumzia kuhusu hatua wanazochukuliwa baadhi ya wamiliki wa migodi wanaokiuka taratibu za “Hati ya Mauzo” Mkaguzi wa Madini ya Ujenzi na Viwandani Abubakari Jihango alisema kuwa hadi sasa kuna kuna kesi 53 mahakamani, na kama itadhihirika ukiukwaji wa sheria, taratibu za kisheria zitafuatwa.
Meneja wa Maabara kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) Mhandisi Mvunilwa Mwarabu akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) mashine ya kupimia kiwango cha madini inayoitwa Atomic Absorption Spectroscopy (AAS) walipotembelea Maabara ya Wakala huo jijini Dar es Salaam leo.
Mkemia Alfred Aloyce kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) sampuli ya jiwe la dhahabu iliyotayarishwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara ili kubaini kiasi cha madini ya dhahabu kwenye jiwe hilo.
Madini ya ujenzi aina ya kokoto zilizo tayari kwa matumizi ya ujenzi wa aina  mbalimbali. Kupitia TMAA Madini hayo kwa sasa yanaipatia Serikali zaidi ya shilingi bilioni 5 kwa mwaka.
Waandishi wa habari waliotembelea ofisi za Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) wakipata maelezo kuhusu mafanikio ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini katika ukusanyaji wa mirabaha ya madini kutoka kwa Mkurugenzi wa Fedha wa wakala huo Bw. Bruno Mteta.
Kaimu Mkurugenzi Uzalishaji na Usafirishaji kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) Bw. Conrad Mtui akiwaeleza waandishi wa habari mikakati ya ukusanyaji wa mirabaha ya madini ya ujenzi wakati walipotembelea kituo cha ukaguzi wa madini hayo kilichopo wilayani Bagamoyo.
Mashine ya Kuyeyusha sampuli za Madini(Fusion and cuppelation Funances)  inayotumika kwenye Maabara ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) Picha na Fatma Salum-MAELEZO

No comments:

Post a Comment