Friday, October 17, 2014

MPANGO WA UCHANGIAJI WA HIARI WA PSPF NI MKOMBOZI

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu Bw. Peter Ilomo amewashauri watanzania kujiunga na Mpango wa Uchangiaji wa Hiari wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF ili kujiongezea kipato na hatimaye kuishi ya staha.

Bw. Ilomo alisema hayo Mjini Bagamoyo wakati wa semina iliyoandaliwa na Mfuko wa Pensheni wa PSPF kwa ajili ya Maafisa Rasilimali Watu kutoka wakala mbalimbali za Serikali

Kutokana na mabadiliko kwenye sekta ya hifadhi ya jamii, PSPF ilianzisha Mpango wa Uchangiaji wa Hiari maarufu kama PSS ili kuweza kuwahudumia Watanzania wote ambao wanahitaji huduma za hifadhi ya jamii ambao walikosa fursa hiyo huko nyuma.

“Mpango huu ni mkombozi kwani unazidi kukuongezea kipato na kukufanya uishi maisha yenye staha sasa na hata wakati wa ustaafu wako. Mpango huu pia unatoa ruksa kwa mtu asiye raia wa Tanzania lakini anafanyakazi hapa nchini kihalali kuwa mwanachama” alisema Bw. Ilomo.

Akizungumzia juu ya ujio ya kanuni moja ya ukokotoaji wa mafao, Bw. Ilomo alisema, “Kuwepo kwa kanuni moja ya ukokotoaji mafao ni changamoto kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwa kuwa kigezo kikubwa cha kuvutia wanachama kitakuwa ni ubora katika huduma na mafao ya muda mfupi. Hivyo, nawaagiza watendaji wote wa PSPF kuhakikisha mnatumia vyema fursa hii kutoa elimu sahihi kwa watendaji hawa muhimu katika utumishi wa umma hapa nchini”.

Kutokana na Wizara ya Kazi na Ajira kutangaza kuwa Mifuko yote ya Hifadhi ya itakuwa ikitoa mafao yanayolingana, alisema wanachama wa PSPF waliokuwepo hadi tarehe 30/6/2014 watalipwa kwa utaratibu wa zamani na wote walioajiriwa kuanzia Julai 1, 2014 watalipwa mafao yao kwa mujibu wa kanuni mpya.

Katibu Mkuu huyo kutoka ofisi ya Rais aliipongeza PSPF kwa kuandaa semina hiyo na kuongeza, “ Semina hizi ni muhimu kwani zinatoa fursa ya kuonana na wadau na kutoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali kwa manufaa ya Mfuko na wanachama wake”.

Awali akizungumza katika semina hiyo Mkurugenzi Mkuu wa PSPF Bw. Adam Mayingu aliwahakikishia washiriki wote wa semina hiyo kwamba PSPF itahakikisha inafikia dira yeke ambayo ni kuwa mtoa huduma bora wa hifadhi ya jamii nchini, na kufanyakazi kwa mujibu wa dhima ya Mfuko ambayo ni kutoa huduma zenye ushindani katika sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa wateja wake kwa kutumia watumishi wenye ari ya kazi na teknolojia inayofaa.

Katika kuhakikisha inafikia dira yake na kuishi dhima yake, Bw. Mayingu aliahidi kwamba PSPF itaendelea kutekeleza majukumu yetu ya utendaji wa kila siku ikiongozwa na uwajibikaji, wajibu, muitikio, nidhamu, juhudi, uwazi na unyenyekevu kwa wote.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Adam Mayingu, akizunfumza wakati wa semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mfuko huo kwa maafisa rasilimali watu kutoka wakala za serikali iliyofanyika mjini Bagamoyo mkoa wa Pwani Alhamisi Oktoba 16, 2014.
Katibu Mkuu Ikulu,Peter Ilomo akitoa hotuba ya ufunguzi wa Semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mfuko wa Pensheni wa PSPF, kwa maafisa rasilimali watu huko Bagamoyo mkoani Pwani, Alhamisi Oktoba 16, 2014. Warsha hiyo ililenga kuwapatia elimu waajiri kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na Mfuko huo kwa wanachama wake.
Mmoja wa washiriki wa semina hiyo, akizungumza.
Washiriki wa semina wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa na wataalam wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na Mfuko huo kwa wanachama wake, Semina hiyo ilifanyika mjini Bagamoyo Alhamisi Oktoba 16, 2014.
Katibu Mkuu Ikulu, Peter Ilomo, (Kulia), akiongozana na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Gabriel Silayo, wakati wa mapumziko ya chai baada ya kufungua semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mfuko huo kwa maafisa rtasilimali watu huko Bagamoyo mkoani Pwani, Alhamisi Oktoba 16, 2014.

No comments:

Post a Comment