Thursday, October 2, 2014

Mahakama yaiamuru SCBHK, TANESCO kutokuwabugudhi wamiliki wa IPTL

Katibu na Mwanasheria mkuu wa kampuni ya ufuaji umeme ya IPTL, Bw. Joseph Makandege akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) nakala ya hukumu iliyotolewa na mahakama kuu ya Tanzania ikizuia benki ya Standard Chartered ya Hong Kong na Tanesco kuendelea kuwabugudhi wamiliki wa IPTL na kuingilia uendeshaji wa mitambo yake. Kushoto ni Meneja Rasilimali watu wa IPTL Bw. Aidan Kaude. 

·         Yasema Bw. Sethi kuendelea kusimamia mitambo ya ufuaji umeme ya Tegeta.

Mahakama Kuu ya Tanzania imeiamuru Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong na Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (TANESCO) kuacha kuingilia utulivu, umiliki, usimamizi na utawala wa Mitambo ya ufuaji umeme ya Bw. Harbinder Singh Sethi iliyopo Tegeta, na kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya msingi.

Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions Limited (PAP) zilifungua kesi kwa kuhoji uhalali wa maamuzi ya Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) dhidi ya Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) na Martha Renju (anaedaiwa kuwa msimamizi wa mali zake), ijulikanayo kama "Decision on Jurisdiction and liability" iliyotolewa katika kesi ya ICSD namba ARB / 10/20.

Katika hukumu hiyo yenye kurasa 16 iliyoandikwa na Mhe. Dk. Fauz Twaib (Jaji) na kusomwa kwa niaba yake na Mhe. Amri Msumi Hamisi (Jaji), mahakama kuu jana iliwazuia SCBHK na / au Tanesco kuendelea kuwabugudhi IPTL na PAP -zinazomilikiwa na Bw. Sethi – mpaka pale uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya msingi itakapo amuliwa.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama mbele ya Bw. Sethi  (mmiliki wa IPTL / PAP) na Kieren Day (Mkurugenzi wa SCB-HK), Mhe. Dk Twaib aliamuru Tanesco kutofanya biashara yoyote na SCB-HK au Martha Renju kwa niaba ya IPTL / PAP bila ya idhini ya kimaandishi kutoka IPTL / PAP.
 
"Wadaiwa kwa pamoja wanazuiliwa kufanya utekelezaji wa maamuzi iliyotolewa katika chombo cha kimataifa ya ICSD yenye namba ARB / 10/20 na kusambazwa kwa wahusika mnamo tarehe  12 mwezi Februari mwaka 2014, kwa namna yoyote ile, na kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya mdai, " inasomeka sehemu ya hukumu hiyo.

Tanesco ambayo iliwakilishwa na Wakili wake Bw. Urassa, pia imezuiwa kutolipa kwa SCB-HK na Martha Renju malipo yoyote wanayostahili IPTL / PAP bila ya idhini ya maandishi kutoka kwa IPTL / PAP.
Mahakama pia imeizuia Tanesco kutotekeleza au kukubaliana na au kuyatekeleza maamuzi ya ICSID, na kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya msingi.

Jaji Mhe. Dk Twaib alitupilia mbali hoja ya mwanasheria wa SCB-HK, Bw.Charles Morrison, ambaye alisema kuwa mahakama kuu ya Tanzania haipaswi kusikiliza na kutoa maamuzi juu ya ombi hilo sababu Tanzania ni mwanachama wa Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ambayo pia inajulikana kama Washington Convention au ICSID .

Kwa mujibu wa hakimu Dr. Twaib, Wakili Morrison alionya kuwa kama Tanzania aitotii wajibu huo, itajiweka sehemu mbaya katika nyanja ya kimataifa.

"Kwa heshima kubwa, nashindwa kuona mantiki ya utetezi wa Bw. Morrison na jinsi gani litaathiri mamlaka ya Mahakama hii la kuikubali ombi hili. Japokuwa Bw. Morrison amekwepa kusema moja kwa moja, maoni yake yamelenga kusema kwamba mahakama hii haina mamlaka ya kutoa amri husika.

"Ninashindwa kuelewa ni jinsi gani serikali ya Tanzania, ambayo si sehemu ya kesi hii, itakuwa imevunja Mkataba wa Washington kwa sababu tu ya wananchi wake wawili ambao ni wafanyabishara binafsi, wametafuta amri ya kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa ICSID kwa misingi ya udanganyifu. Sioni ni jinsi gani, kwa kutumia mamlaka yake katika kutoa maagizo hayo, mahakama hii itakuwa inaingilia majukumu ya kimataifa ya Tanzania chini ya Mkataba wa Washington," inasomeka hukumu ya Jaji Twaib.

Sababu ya pili ya Bw. Morrison ya kuoma mahakama isikubali ombi hilo ilikuwa kwamba madai hayo yanaweza kuwa yametolewa “miaka mingi iliyopita” wakati kesi ya ICSID ilipoanza na kubainisha kuwa hii ni kesi iliyokufa (tort case), ingekuwa imefanyiwa kazi ndani ya miaka mitatu ya tarehe ile.

Jaji Twaib alitupilia mbali hoja hiyo kwa kusema, "Kwa heshima kuba kwa Bw. Morrison, hoja hii haina nguvu ya kisheria. Kama ilivyosemwa na mwanasheria wa waombaji (Bw. Joseph Makandege na Bw. Melkzedek Lutema), madai hayo yanatoa changamoto kwa uamuzi wa ICSID ambayo ulitolewa mwezi Februari, 2014. Madai, hayo baada ya kushindwa Aprili 2014, haiwezi ukasema imepitwa na wakati. Nitaitupilia mbali pingamizi hilo.”

Kuhusu ombi kuwa shauri hilo lisikilizwe katika mahakama ya Hong Kong na fedha zote zipelekwe hiko, wanasheria wote Bw. Makandege na Bw. Lutema walisema kuwa litakuwa sio kutenda haki kwa mteja wao, sababu kuna kiasi kikubwa cha fedha kinahusika, ambayo itakuwa vigumu kuirejesha na kuwa itakuwa vigumu kwa IPTL/PAP kurejea katika hali yake kwa sababu SCB-HK ni ya nje na haina mali zozote kubwa Tanzania.

Hii inampa Bw. Sethi ushindi kwa mara nyingine miongoni mwa kesi kadhaa ambazo zimekuwa zikianzishwa na SCB-HK dhidi ya IPTL/PAP.

3 comments:

  1. This is great news kwa IPTL/PAP wasife moyo kwa kelele za wanasiasa sababu penye jambo jema siku zote lazima shetani awe katikati.
    Watanzania tunawatakia utendaji mzuri IPTL/PAP ili kutupunguzia tatizo la umeme kwenye nchi yetu
    Natambua kazi nzuri pia inayofanywa na TANESCO chini wazira ya Nshati na Madini chini ya Prof. Muhongo wanafanya kazi kubwa sana kuhakikisha watanzania tunapata umeme wa uhakika by 2015. Kinyerezi oyeeeee!!

    ReplyDelete
    Replies
    1. Now nimeanza kuujua ukweli akina kafulila wanatumika vibaya sana kwa maslahi ya mafisadi wa kibiashara na Iptl

      Delete
  2. Hongera PAP, We need hizo 500 MW tupumue na sisi Dar es salaam. Fanyeni kazi waachieni siasa wanasiasa.

    ReplyDelete