Saturday, October 4, 2014

BALOZI SEIF AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA MAREKANI, AKAGUA UJENZI WA BARABARA WETE, PEMBA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Alik Iddi alisema ushirikiano ulioonyeshwa kati ya wananchi wa Wete – Gando na Mjenzi wa Bara bara ya Wete Gando umesaidia kufanikisha ujenzi wa bara bara hiyo kwa zaidi ya asilimia Thamanini.
 Balozi Seif alisema hayo wakati akizungumza na wajenzi wa bara bara hiyo Kampuni ya Mecco, wahandisi wa Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano Zanzibar pamoja na Wananchi wa Gando mara baada ya kuitembelea Bara bara hiyo kutoka Wete hadi Gando.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajitajidi kuwa na miundo mbinu mizuri na ya kisasa  ya mawasiliano na Bara bara  katika kiwango kinachokubalika Kimataifa ili watumiaji wake waendelee kufaidikia nayo katika kujiharakishia maendeleo ya Kiuchumi na ustawi wa Jamii.
“ Tunahitaji kuwa na Bara bara zilizo katika kiwango kinachostahiki kimatumizi ili wananchi waendelee kufaidika katika kujiletea maendeleo yao ya kiuchumi na kiustawi wa Jamii “. Alisema Balozi Seif.
Aliupongeza Uongozi wa Kampuni ya Mecco chini ya Mkandarasi wake kwa juhudi inayochukuwa ya ujenzi wa Bara bara hiyo ambayo kukamilika kwake italeta ukombozi mkubwa na kuwaondoshea usumbufu wa usafiri wananchi wa ukanda wa kaskazini mwa Kisiwa cha Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi wa Kampuni ya Mecco kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kadri ya uwezo uliopo katika kuipatia fedha za vifaa Kampuni hiyo ili ikamilishe ujenzi wa Bara bara hizo kwa wakati.
Balozi Seif alimuomba Mkandarasi wa ujenzi huo aendelee kuwa mstahamilivu kwa vile ameonyesha muelekeo mkubwa wa uzalendo wa kusimamia maendeleo ya kiuchumi katika sekta ya mawasiliano kwa upande wa bara bara.
Akitoa maelezo Meneja wa Kampuni ya Mecco Bwana Abdullkadir Mohamed Bujeti alisema mradi huo umepangwa kukamilika kazi zilizobakia mwezi Disemba mwaka huu iwapo fedha za ununuzi wa vifaa vilivyobakia zitapatikana kwa wakati.
Bwana Bujeti alisema hadi sasa gharama za ujenzi huo kwa awamu ya kwanza zimeshafikia Shilingi za Kitanzania Bilioni sita wakati zile zinazohitajika kwa ununuzi wa vifaa hivyo ni kiwango hicho hicho cha shilingi Bilioni Sita.
Meneja huyo wa Mecco alivitaja vifaa vitakavyohitajika katika ukamilishaji huo ni pamoja na lami, mafuta, rangi  pamoja na vifaa vya kuashiria uwepo wa sehemu za hatari katika bara bara hiyo.
Mapema msimamizi wa ujenzi wa Bara bara hiyo kutoka Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar Mhandishi Japhet Malambi alisema kasi ya utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa bara bara ya Wete – Gando imekuwa kubwa na ya kuridhisha ikizingatia viwango.
Mhandishi Japhet alisema mkandarasi wa ujenzi huo aliamua kusitisha shughuli zote za ujenzi na kusababisha kudorora kwa mradi huo baada ya kutokuwa na mhandisi Mkaazi ambae ndie msimamizi na mshauri wa mradi.
Alisema hatua hiyo iliyochukuwa muda mrefu imepelekea wananchi wa wanaotumia bara bara hiyo kupoteza matumaini ya kukamilikwa kwa mradi wa bara bara hiyo.
Mhandisi Japhet Malambi alitahadharisha kwamba ili kunusuru hasara nyengine inayoweza kutokea endapo mradi huo utasimama tena ni vyema Serikali ikajikita katika upatukanaji wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kukamilisha kazi hiyo.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif Ali Iddi alikuwa na mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ms Shimoja kutoka Jimbo la Michigan Nchini Marekani Dr. Robert Shumake.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika chumba cha watu mashuhuri { VIP } kilichopo kwenye uwanja wa ndege wa Pemba ambapo Balozi Seif aliwasili akitokea Mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la Katiba.
Katika mazungumzo yao Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Ms Shimoja Dr. Robert Shumake ambaye amepata heshima ya kuwa Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani alielezea kuridhika na mazingira mazuri ya uwekezaji kisiwani Pemba.
Dr. Shumake alisema Uongozi wa Kampuni yake utaangalia maeneo ambayo inaweza kuwekeza vitega uchumi kama alivyomuahidi Balozi Seif wakati wa ziara yake katika Jimbo la Seattle Nchini Marekani mwaka jana.
“ Muda wangu mfupi niliopata kutembelea maeneo tofauti ya Tanzania ikiwemo Zanzibar umenipa faraja na shauku ya kuangalia fursa zilizopo za uwekezaji na namna  uongozi wa Kampuni yangu utakavyochangamkia fursa hiyo “. Alisema Dr. Robert Shumake.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia Uongozi wa Kampuni hiyo ya Ms. Shimoja kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuupa msaada wakati unaohitaji kuwekeza hapa Zanzibar.
Balozi Seif alimueleza Dr. Shumake kwamba Zanzibar tayari imetoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza miradi na vitega uchumi vyao ili kusaidia kunyanyua pato la taifa sambamba na kuongeza soko la ajira.
Alisema yapo maeneo na sekta ambazo Kampuni ya Ms Shimoja inaweza kuyatumia kuwekeza akiyataja kuwa ni patoja na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Pemba, Bandari ya Wete, Sekta ya utalii pamoja na nyumba za mkopo nafuu.
Alifahamisha kwamba miradi ya nyumba za mikopo nafuu kwa kiasi kikubwa inaweza kuwasaidia zaidi vijana wenye ajira mpya  ili wajenge hatma bora ya maisha yao ya baadaye.
Dr. Robert Shumake Mkurugenzi wa Kampuni ya Ms. Shimoja ambae pia ni Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani alikuwepo Nchini Tanzania kutia saini mkataba wa uanzishwaji wa treni iendapo kwa mwendo wa kasi kati yake na Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania.
Treni hiyo itakapokamilika itakuwa ikitoa huduma ya usafiri kati ya Dar es salaamu na pugu kwa kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere.
 Imetolewa na:
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
4/10/2014.

No comments:

Post a Comment