Sunday, September 7, 2014

WELEDI NA KUZINGATIA MAADILI YA UANDISHI WA SHUGHULI ZA BUNGE MAALU LA KATIBA KUTALETA TIJA KWA WAANDISHI WA HABARI


Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.


Kanuni za Bunge Maalum hususani Kanuni ya 77 inawataka waandishi wa habari kuandika habari za Bunge Maalum kwa weledi mkubwa na kuzingatia maadili ya uandishi wa habari ili kujiepusha na uandishi wenye utashi na ushabiki wa kisiasa, msukumo binafsi, chuki ama uchochezi na wakati mwingine uongo wa makusudi.

Aidha, katika Kanuni hiyo hiyo ya 77(3) inatamka bayana ya kuwa “Katibu anaweza wakati wowote kuondoa ruhusa aliyotoa kwa mwakilishi wa Chombo chochote cha habari iwapo chombo hicho kitatoa taarifa yoyote kuhusu shughuli za Bunge Maalum ambayo kwa maoni ya Bunge Maalum inapotosha ukweli au vinginevyo inakiuka Kanuni, taratibu au haki za Bunge Maalum”.

Vyombo vya habari vina haki ya kupata habari ili viweze kuhabarisha umma juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea nchini has katika Bunge Maalum la Katiba, lakini katika kufanya hivyo waandishi wa habari wanapaswa kutenganisha kati ya siasa na uandishi wa habari, hivyo wanapaswa kubainisha na kuainisha dhana ya uandishi wa habari za kibunge wenye tija kwa taifa ambayo ni weledi katika uandishi wa habari, uelewa kuhusu matarajio ya wananchi pamoja na uelewa juu ya dhima na dhamira ya Bunge katika taifa.

Uandishi wa habari ni vema usitumiwe kama njia ya kufikia malengo ya kisiasa ama mtu binafsi, makundi au chama na kitendo cha mwanasiasa kuvaa koti la uandishi wakati ni mwanasiasa kunajenga chuki, kunaharibu heshima ya uandishi wa habari na maisha ya waandishi.

Endapo siasa zitaingizwa katika uandishi wa habari basi kuna hatari ya kuilisha jamii yetu uongo. Mfano, kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinavyotafsiriwa kisiasa.

Bila shaka vyombo vya habari ni kama mshipa wa damu wa siasa na demokrasia nchini. Hakuna chama cha siasa kinachoweza kufanya siasa kwa ufanisi pasipo kushirikiana na vyombo vya habari, hivyo waandishi wa habari wanakuwa vijumbe wa kubeba ujumbe wa wanasiasa, kuupeleka kwa wananchi na kubeba mrejesho wa wananchi na kuupeleka kwa wanasiasa juu ya sera na mienendo yao.

Akizungumza wakati wa Semina iliyoandaliwa kwa ajili ya waandishi wa habari kuhusu namna bora ya uandishi wa habari za shughuli za Bunge, semina iliyoandaliwa na Ofisi ya Habari ya Bunge kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la UNDP ambayo ilifanyika tarehe 6 Septemba, 2014 mjini Dodoma, Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Itifaki wa Bunge Maalum, Bw. Jossey Mwakasyuka alisema kuwa lengo la semina hiyo ilikuwa ni kuweza   kujadiliana na kubadilishana uzoefu juu ya uandishi wa habari kwa waandishi ili kuweza kuandika habari zilizo sahihi zinazohusu Bunge hilo kwa manufaa ya taifa.

Katika semina hiyo waandishi wengi watakuwa wameelimika vya kutosha kwani ni mambo mengi yenye umuhimu yaliwasilishwa na watoa mada waliobobea katika mambo ya uandishi na siasa hali ambayo itawafanya waandishi wengi nchini kuzingatia weledi na maadili pindi wanapokuwa wanaandika habari zinazohusiana na bunge hilo ili kuhabarisha umma.

Katika semina hiyo, watoa mada waliweza kugusia mambo mbalimbali yakiwemo uandishi wa habari za Bunge na Siasa wenye tija, athari za siasa katika uandishi wa habari za Bunge, madhara ya Vyombo vya habari kutumika, miiko na maadili ya kuzingatia katika uandishi huo.

Akitoa mada wakati wa semina hiyo, Mhariri Mtendaji wa Jamhuri Media Limited, Bw. Deodatus Balile amezitaja athari mbalimbali za siasa katika uandishi wa habari za Bunge huku akisema kuwa vyombo vya habari vimekuwa vikitumiwa katika kuzalisha chuki katika jamii kwa kuchochea mbunge Fulani, Rais, Diwani au Chama Fulani kiangushwe, pia hutumika kuchochea umwagaji damu na kuondosha amani nchini na lengo kubwa ni kwamba wanasiasa wengi wanafahamu kuwa vyombo vya habari vinaweza kuwasaidia kuharibu majina ya watu.

Balile aliongeza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kufuata miiko na maadili ya uandishi wa habari kwa kutofautisha kati ya habari na maoni, kutoa haki ya asili kwa kila anayetuhumiwa, kuthibitisha habari kupitia vyanzo vitatu ili habari iwe nzuri lakini pia suala la upendeleo si sehemu ya habari.

“Usichanganye wasomaji, wasikilizaji au watazamaji wako kwa maslahi ya kisiasa kwa kutoa taarifa potofu au picha zisizoakisi ukweli, tujiepushe na athari hizo kwa kutovaa sare za vyama vya siasa wakati wa kampeni za uchaguzi na tujiepushe na chuki kwa viongozi ili kuepusha migogoro dhidi yao”, alisema Balile.

Aidha, Balile aliwataka waandishi wajenge urafiki wa kikazi na wanasiasa lakini si utarishi, ukuwadi wala uwakala bali wawe na mshikamano, kuhabarisha kuhusu habari za maendeleo, umoja na amani, pia zipewe kipaumbele na kuepuka kuchapisha habari za uchochezi, lakini mbali na hayo aliwasisitiza waandishi kuhusu kujiendeleza kielimu na kuzifahamu vyema taratibu, mienendo ya ripoti za Bunge na matarajio halali ya Wabunge.

Kwa upande wa mtoaji mada mwingine katika semina hiyo, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Kamati za Bunge, Bw. Athuman Hussein aligusia masuala muhimu kwa waandishi hasa kuhusiana na uandishi wa habari za kibunge wenye tija kwa taifa.

Bw. Hussein alisema kuwa dhana ya uandishi wa habari wenye tija kwa taifa inajadilika kwa namna nyingi, namna ya kwanza ni kubainisha tanzu za maudhui na ya pili ni kuainisha nadharia kuhusu maudhui na kisha kusanisi maarifa. Aidha, alisema pia dhana ya uandishi wa habari za kibunge wenye tija inahusisha Wabunge na sekretariati, Waandishi wa Habari pamoja na Msimamizi wa tasnia.

“Hatuwezi kuwa na uandishi wa habari za kibunge wenye tija kwa taifa kama hatuna weledi katika uandishi wa habari, hatuelewi matarajio ya wananchi kwa bunge na kama hatuelewi dhima na dhamira ya Bunge”, alisema Hussein.

Akizungumiza kuhusu weledi katika uandishi wa habari, Bw. Hussein alisema kuwa weledi katika uandishi wa habari za kibunge ni jambo la msingi na hujengwa na kukuzwa kwa tabia ya kujielimisha kuhusu Bunge, tabia ya kujielimisha kuhusu tasnia ya habari, ufuatiliaji kuhusu matarajio ya wananchi kwa Bunge pamoja na uelewa kuhusu sayansi ya maadili.

Mtoa mada hapa anamaanisha kuwa hakuna namna ya kuwa mwandishi wa habari za kibunge mwenye tija kwa taifa kama mwandishi huyo ameacha kujielimisha kuhusu masuala ya bunge, ameacha kufuatilia ipasavyo yanayohusu matarajio ya wananchi kuhusu bunge na kama mwandishi huyo hazingatii mutukutiko katika mazingira ya tasnia aliyopo.

Sambamba na hayo, Bw. Hussein aliendelea kwa kufafanua juu ya tanzu za weledi katika uandishi wa habari za kibunge akizitaja tanzu hizo zikiwemo maarifa ya kutosha kuhusu masuala ya kibunge, uelewa mzuri kuhusu bunge, uelewa kuhusu taratibu, matukio, mila, desturi, mwenendo na misingi, uelewa kuhusu uwezo wa jamii kupokea na kupokesha, uelewa kuhusu mfumo jamii uliopo pamoja na uelewa kuhusu hali ya kisiasa na mwenendo wake.

“Msisitizo ninaouweka katika hili ni kwamba, hakuna anayeweza kuwa mwandishi wa habari za kibunge kama;- Hana weledi wa uandishi wa habari, lazima aelewe matarajio ya waandishi, hakuna mwandishi yeyote anayeweza kuleta tija kama haelewi dhima ya bunge na dhamira ya bunge”, alisisitiza Hussein.

Uandishi wa habari za kibunge unaweza kuwa mzuri wenye maadili kama umezingatia madhumuni ya kuripoti habari za kibunge, na yatupasa kujua kwamba maadili katika uandishi wa habari za kibunge ni kuhusu uamuzi wa kimantiki unaopendeza kwa mtizamo mpana kuhusu masuala ya bunge.

Jamii nayo inatarajia mambo mengi kutoka katika Bunge yakiwemo Bunge kutunga sheria zinazokidhi mahitaji ya ustawi wa jamii zinazotatua pengo la kimfumo wa kisheria kwa maslahi ya umma, bunge linaridhia mikataba, makubaliano na itifaki zenye tija kwa ustawi wa jamii, pia bunge linasimamia serikali katika kuhakikisha kuwa inajali mahitaji ya wananchi wake, inajielekeza kwenye huduma bora za jamii, inajielekeza kwenye misingi ya utawala na inaepuka ubadhirifu.

Tarajio kubwa lingine ambalo wananchi wanakuwa nalo ni lile la Bunge kuhidhinisha bajeti ya serikali kwa kuisukuma kwenye mwelekeo wa kutatua matatizo ya watu, kuimarisha ustawi wa watu pamoja na kuwezesha maisha bora kwa wananchi.

Uandishi wa habari za kibunge utakuwa na tija iwapo waandishi wanakuwa na weledi, wanafahamu masuala ya kibunge, wanaelewa matarajio ya wananchi kiujumla na kitaasisi, hivyo uandishi wa habari za kibunge ni sehemu ya tasnia ya uandishi wa habari na jambo muhimu katika hilo ni kujali maadili na weledi kuhusu uandishi na maarifa kuhusu bunge hilo.

Ni vema sasa waandishi tukalisaidia taifa kwa kuandika habari za kweli kuhusiana na Bunge hili Maalum na kuelimisha umma na kujiepeusha na ushabiki unaoweza kuliingiza taifa katika matatizo ambayo kiuhalisia yanayweza kuepukika.

No comments:

Post a Comment