Monday, September 1, 2014

Wanamazingira wahamasishwa kuwalinda binadamu, viumbe hai

Kamishna Msaidizi wa Nishati Mbadala kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Leonard Ishengoma akisoma hotuba ya ufunguzi (kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, Eliakim Maswi) wa semina ya mafunzo kwa Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, juu ya mpango kazi wa mazingira wa sekta za nishati na madini, Septemba 1, 2014.
Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa katika picha ya pamoja na Maafisa na Viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini baada ya ufunguzi wa semina ya mafunzo ya siku tatu kwa Wanamazingira hao Septemba 1, 2014 jijini Mwanza. Kutoka kushoto (waliokaa) ni Kamishna Msaidizi na Afisa Madini Kanda ya Ziwa Magharibi, David Mulabwa, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Mbadala, Leonard Ishegoma na Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Gideon Kasege.
Afisa Misitu Mkuu kutoka Kitengo cha Mazingira – Wizara ya Nishati na Madini, Theodory Silinge akisisitiza jambo wakati wa semina ya mafunzo kwa Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, inayofanyika jijini Mwanza.
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Gideon Kasege akizungumza na Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, Septemba 1, 2014 jijini Mwanza, wakati wa semina ya mafunzo kwa wanamazingira hao.
Afisa Mazingira wa Mji wa Kahama, Martin Masele akiuliza swali wakati wa semina ya mafunzo kwa Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini jijini Mwanza.
Wajumbe wa Sekretariet wakiandika kumbukumbu za Semina ya Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, Septemba 1, 2014 jijini Mwanza. Kutoka Kushoto ni Nassor Abdullattif na Emmanuel Shija.
Kamishna Msaidizi na Afisa Madini wa Kanda ya Ziwa Magharibi, David Mulabwa akifafanua jambo kwa wajumbe wa semina ya Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, Septemba 1, 2014 jijini Mwanza. Semina hiyo ya siku tatu imeandaliwa na Kitengo cha Mazingira cha Wizara ya Nishati na Madini.
Afisa Sheria kutoka Wizara ya Nishati na Madini Renatus Damian, akitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na shughuli za utunzaji mazingira wakati wa semina kwa Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, Septemba 1, 2014 jijini Mwanza.

Na Veronica Simba

Maafisa Mazingira nchini kote wamepewa changamoto kuhakikisha kuwa uwekezaji mkubwa unaoendelea hivi sasa katika sekta za nishati na madini, hauathiri binadamu na viumbe hai wengine.

Changamoto hiyo imetolewa leo jijini Mwanza na Kamishna Msaidizi wa Nishati Mbadala kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Leonard Ishengoma wakati akifungua semina ya mafunzo kwa Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa Viktoria, juu ya mpango kazi wa mazingira wa sekta za nishati na madini.

Akifungua semina hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara husika, Eliakim Maswi, Kamishna Msaidizi amesema hivi sasa, sekta za nishati na madini zinapata uwekezaji mkubwa sana na kutolea mfano sekta ya nishati ambapo shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi zinaendelea na hivyo kuwataka wanamazingira hao kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha mazingira hayaathiriwi na shughuli husika.

Ameongeza kuwa, upande wa sekta ya umeme, uwekezaji unategemewa kuongezeka kwa kiwango kikubwa pia kwa siku za hivi karibuni ikiwa ni mikakati ya Wizara kuhakikisha inakidhi mahitaji ya nishati hiyo kwa wananchi na hivyo amesema uwekezaji huo utaleta changamoto nyingi za kimazingira, kiuchumi na kijamii.

Akizungumzia sababu nyingine zinazochangia kuharibu mazingira, hususan zinazohusiana na sekta za nishati na madini, Ishengoma amesema matumizi ya nishati yanachangia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha madhara mbalimbali kama vile majanga ya mafuriko, ukame na maradhi ya milipuko.

Kwa upande wa sekta ya madini, Kamishna Msaidizi Ishengoma amesema kwa miaka ya hivi karibuni, sekta hiyo imekua kwa kasi kubwa sana, hususan uchimbaji na uzalishaji wa madini, shughuli ambazo zinachangia katika uharibifu wa mazingira.

Vilevile, amesema wengi wa wachimbaji wadogo na wa kati wa madini wana mwamko mdogo sana katika kuhifadhi mazingira katika maeneo yao ya kazi na ameongeza kwamba hata baadhi ya wawekezaji wakubwa wanakwepa kutimiza taratibu za utunzaji wa mazingira kwa lengo la kupata faida kubwa.

“Ni kwa sababu hiyo, Wizara ya Nishati na Madini imeandaa Mpango Kazi wa Mazingira Kisekta ambao utekelezaji wake utaenda hadi ngazi ya wilaya ili kuhakikisha shughuli za maendeleo zinazofanyika, haziathiri mazingira,” amesisitiza Ishengoma.

Aidha, amewahamasisha Maafisa Mazingira kuhakikisha wanahuisha masuala ya mazingira katika mipango na bajeti zao za wilaya kwa kuwa wana nafasi nzuri katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwani huko ndiko kuliko chimbuko la maendeleo.

Semina hiyo ya Mafunzo kwa Maafisa Mazingira, ni mwendelezo wa semina zinazotolewa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kitengo chake cha Mazingira ili kuongeza uelewa na hivyo kutekeleza kwa dhati azma ya utunzaji mazingira.

Maafisa Mazingira wanaoshiriki katika semina hiyo ya mafunzo ya siku tatu ni kutoka Wilaya 18 za mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Mara, Kigoma na Tabora.

No comments:

Post a Comment