Friday, September 26, 2014

Utalii wa Wanyamapori na Maendeleo ya Jamii: Mambo yenye uhusiano wa asili na wa moja kwa moja

Balozi wa Marekani Nchini Tanzania,
Mark Childress
Siku ya Kimataifa ya Utalii ambayo huadhimishwa tarehe 27 Septemba inatupa fursa ya kutafakari manufaa na matokeo ya jitihada za uhifadhi wa wanyama pori na utalii kwa jamii zinazozunguka maeneo ambapo shughuli hizi zinafanyika na kwa Tanzania kwa ujumla. Kwa watu wengi duniani kote, kutembelea Tanzania ni jambo la kipekee na la kihistoria katika maisha yao. Kwa Tanzania ziara za watalii hao ni chanzo cha mapato na kichocheo cha uchumi, ambacho kwa makadirio ya mwaka 2013 kililiingizia taifa takriban Dola za Kimarekani Bilioni 1.9. Wengi wa watalii hawa hutembelea Tanzania ili kujionea wanyama pori. Hata hivyo kwa bahati mbaya jambo hili hivi sasa linakabiliwa na kitisho.

Ujangili na utoroshwaji wa wanyama pori unatishia kuendelea kuwepo kwa mali asili hii adhimu na ya kipekee na mchango wake kwa uchumi. Ninapongeza jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kukabiliana na kitisho hiki. Mimi mwenyewe binafsi nimedhamiria kwa dhati kabisa kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na ujangili na utoroshwaji wa wanyama pori.

Serikali ya Marekani itaendelea na ushirikiano wake wa muda mrefu na Tanzania katika eneo hili na imepanga kutoa zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 40 katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kusaidia shughuli mbalimbali za uhifadhi na usimamizi wa wanyama pori. tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wanajamii katika maeneo husika, sekta binafsi na hata wafadhili wengine katika kusaidia jitihada hizi zinazoongozwa na Watanzania wenyewe.

Utalii unaweza kabisa kujenga mstakabala mwema na endelevu kwa wote kwa kupitia maendeleo ya jamii. Shughuli za kitalii zinazoendeshwa na kuwahusisha wanajamii na wakazi wa maeneo husika katika kufanya maamuzi muhimu huwawezesha wanajamii hao kunufaika kutokana na mapato yatokanayo na shughuli hizo na miradi mingine ya maendeleo. Jambo hili huwaleta wanajamii pamoja, huzalisha ajira na kuboresha utawala katika ngazi husika. Hali kadhalika, hutoa vivutio vya kijamii na kiuchumi kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi.

Pale ambapo jamii zinanufaika kutokana na utalii unaohusisha wanyamapori husaidia sana katika kulinda mali asili hizo. Kwa sababu hiyo, pale inapowezekana, miradi ya uhifadhi inayofadhiliwa na Marekani hulenga pia kuhusisha kikamilifu jamii zinazozunguka maeneo hayo.

Mathalan, toka mwaka 1998 Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Ushirikiano wa Kimataifa (USAID) imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Tanzania, wabia wa maendeleo na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi ili kuanzisha maeneo ya hifadhi ya wanyama pori yanayosimamiwa na jamii (WMAs). Jumla ya WMAs 19 zimeanzishwa nchini kote na kuzijengea uwezo jamii husika kusimamia, kulinda na kunufaika kutokana na maeneo hayo ya hifadhi.

Maeneo yote yaliyohifadhiwa na kuwekwa chini ya usimamizi wa jamii husika ni zaidi ya hekta milioni 3.2 au asilimia 3 ya eneo lote la ardhi ya Tanzania. Miradi mingine

iliyofadhiliwa na Marekani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ni pamoja na ile ya kusaidia ufuatiliaji na ulinzi wa tembo na faru. Miradi hii iliyogharimu Dola za Kimarekani 676,000 ni pamoja na ule wa kuwasaidia askari wa doria wa hifadhi (village game scout patrols) katika WMA ya Waga inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kuendesha shughuli za doria katika eneo lao na ule wa kutoa elimu ya hifadhi ya mazingira kwa shule na vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

Ni lazima pia wananchi washirikishwe kikamilifu katika michakato ya kufanya maamuzi na kuona manufaa ya moja kwa moja ya kiuchumi ya shughuli za utalii katika maeneo yao. Tunapongeza uamuzi wa Tanzania wa kuwekea msisitizo ushiriki wa jamii katika usimamizi wa mali asili, hususan katika WMAs kama mojawapo ya vipaumbele vikuu vitatu katika mkakati wake dhidi ya ujangili na utoroshwaji wa wanyamapori.

Tunaamini kuwa ili kupata mafanikio yaliyokusudiwa ni lazima WMAs ziajiri askari wa doria (Village Game Scouts) wa kutosha ili kuwalinda wanyama pori na kuwawezesha wananchi kuanzisha biashara mbalimbali zinazohusiana na shughuli za kitalii ili manufaa ya jitihada za uhifadhi yafike hadi ngazi ya kaya. Hivi sasa ni sehemu ndogo tu ya mapato yatokanayo na utalii ndiyo yanayorudishwa kwa jamii ili kusaidia shughuli za uendeshaji na uendelezaji wa miradi ya kibiashara.

Kuziwezesha WMAs kubaki na sehemu kubwa ya mapato inayoyapata kutokana na shughuli za utalii kutazihamasisha zaidi jamii zinazohusika na kuzisaidia kuimarisha jitihada za uhifadhi. Wakati huo huo , kuziruhusu WMAs hizi kukusanya mapato yake moja kwa moja kutaimarisha zaidi uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa WMA kama njia ya kusaidia uhifadhi wa wanyama pori nchini kote Tanzania.

Pamoja na kuongezeka kwa ushiriki wa jamii katika ulinzi na uhifadhi wa wanyama pori, ujangili umefika kiwango cha kutisha sana katika maeneo mengi ya nchi. Kila mwaka majangili wanaua maelfu ya tembo wa Tanzania kiasi kwamba nchi ipo katika hatari ya kupoteza kabisa maliasili hii adhimu na manufaa yake ya kiuchumi. Ni lazima tufanye kazi kwa pamoja ili kukomesha hali hii.

Kama nilivyojadili na Rais Kikwete na maafisa wengine wa serikali pamoja na viongozi wa taasisi za kiraia na sekta binafsi, kukomesha janga hili kunahitaji mchakato unaoijumuisha serikali yote kwa ujumla wake (a whole-of-government approach). Kidole kimoja hakivunji chawa.

Mojawapo kati ya wabia wetu muhimu na anayeweza kusaidia kwa ufanisi jitihada zetu za uhifadhi na ulinzi wa wanyama pori ni jamii zinazoishi kuzunguka maeneo ya hifadhi au zile zinazoishi miongoni mwa maliasili hizo, Ni lazima tuhakikishe kuwa jamii hizo zinanufaika kikamilifu kutokana na shughuli za utalii na tunashirikiana nazo kikamilifu katika kulinda wanyama pori wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment