Friday, September 19, 2014

LIBENEKE LA MJENGWABLOG LATIMIZA MIAKA MINANE LEO

Ndugu zangu,

LEO ni Septemba 19, ni Siku ya Kuzaliwa Mtandao wa Mjengwablog.

Kwa mwanadamu, hakupaswi kuwapo na ukomo wa kujitahidi kufanya yalo mema kwa jamii yako.

Na katika kujitahidi kuyafanya yalo mema, basi, mwanadamu uwe tayari kukumbana na changamoto nyingi. Na kama ilivyo kwa maji ya mto, yanapokutana na mwamba, basi, kasi yake huongezeka maradufu.

Leo blogu yako hii ya Mjengwablog imetimiza miaka minane. Miaka minane si haba. Kwa mtoto, aweza kuwa darasa la Pili. Na kwetu wa Mjengwablog ni miaka minane ya kujifunza, kukosea, kujifunza kutokana na makosa, na kisha kusonga mbele.

Kwa niaba ya timu nzima ya Mjengwablog nachukua fursa hii kuwashukuru, kwanza kabisa, mke wangu mpenzi, Mia, ambaye, bila yeye, kazi hii yangu ya kuitumikia jamii ingelikuwa ngumu sana. Pili, niwashukuru kwa dhati wanangu wanne, Olle, John, Manfred na Gustav. Wanawangu hawa wamekuwa na mchango mkubwa pia, ikiwamo kufanya utani na mimi baba yao, ilimradi niwe na wakati wa kucheka, hata pale nilipoona kazi ni ngumu na kukutana na vikwazo.

Na kwa dhati kabisa, naishukuru timu nzima ya Mjengwablog. Nawashukuru kwa upekee kabisa Wanafamilia wote wa Mjengwablog, ukiwamo wewe unayesoma maandiko haya sasa, maana, bila nyinyi, kusingekuwa na maana ya kuifanya kazi hii. Mmekuwa nasi katika hali zote. Hivyo basi, kutuunga mkono.

Naam, ni miaka minane ya kuwa mtandaoni karibu katika kila siku inayotujia na kupita. Ni miaka minane ya mapambano magumu ya kuitumikia jamii na kuhakikisha kuwa tunabaki hai.

Maana, unapoamua kuitumikia jamii bila kuegemea upande, basi, ina maana pia ya kujiweka katika mazingira ya hatari sana. Yumkini kuna maua mengi ya upendo yanaweza kurushwa kwako, lakini, kuna mishale michache ya sumu ambayo pia itarushwa kwako. Kwamba kuna maadui pia.

Na ukimwona nyani ametimiza miaka minane , basi, ujue kuna mishale kadhaa ameikwepa. Lakini, na anavyozidi kuendelea kuishi, yumkini kuna mishale mingine inaandaliwa. Na nyani hatakiwi kuishi kwa kuogopa mishale ya wanadamu. Vinginevyo, ajitundike mtini, afe.

Lililo jema na kutia faraja ni kutambua, kuwa kuna walio wengi wenye kufaidika na kazi hii ya kijamii ambayo Mjengwablog inaifanya. Ni hawa ndio wenye kututia nguvu ya kuendelea kuifanya kazi hii pamoja na changamoto zake nyingi.

Ndugu zangu,

Ilikuwa ni Jumanne, Septemba 19, 2006. Ni siku hiyo ndipo kwa mara ya kwanza niliingiza picha ya kwanza kwenye mjengwablog na kuashiria uzinduzi wa blogu. Ni picha hiyo inayoonekana hapo juu. Niliipiga eneo la Kinondoni Shamba. Tangu siku ya kwanza, niliweka wazi kwenye fikra zangu, kuwa Mjengwablog iwe jukwaa litakalomtanguliza mtu wa kawaida. Iwe sauti ya wale ambao sauti zao hazisikiki.

Na Mjengwablog ikawa chachu ya kuanzishwa kwa gazeti la michezo na burudani la ’ Gozi Spoti’, ikawa chachu pia ya kuanzishwa gazeti la ’ Kwanza Jamii’.

Na kuna miongoni mwetu wenye kufikiri, kuwa mwenye kumiliki gazeti ni lazima awe Mhindi au Mtanzania ’ mweusi’ Mfanyabiashara tajiri. Nakumbuka kuna hata ambao hawakuwa tayari kuchangia kiuandishi kwenye ’ Gozi Spoti’ na ’ Kwanza Jamii’ kwa vile linamilikiwa na ’ Mswahili mwenzao!’Na hata kupata matangazo kukawa na ugumu mkubwa. Gozi Spoti lilisimama kuchapwa baada ya mwaka mmoja mitaani. Kwanza Jamii, nalo likasimama kuchapwa. Likarudi tena baada ya kuingia ubia na Shirika la Daraja. Baada ya miaka miwili na baada ya aliyepelekea kuingia ubia kuondoka nchini na kurudi kwao Uingereza, basi, Kwanza Jamii nalo ’ likaandaliwa’ mazingira ya kuondoka mitaani.

Hata hivyo, Kwanza Jamii, gazeti dogo, ambalo naamini ni muhimu kwa jamii, limerudi tena kwa kutolewa bure kanda ya Nyanda za Juu Kusini na kwa kupitia mtandaoni. Mipango iko mbioni kuliimarisha zaidi katika siku zijazo.

Ndugu zangu,

Changamoto zipo ili tukabiliane nazo, na si kukata tamaa. Mjengwablog inatimiza miaka minane leo kwa vile tulishaamua, kuwa tutapambana hadi risasi ya mwisho. Hivyo pia, tutapambana hadi pumzi ya mwisho.

Maana, tunaamini kuwa kazi tuifanyayo ni yenye manufaa kwa jamii pana. Na tuna haki ya kuifanya. Tunavumilia sauti zenye kutushutumu na kutukosoa. Kuna tunayojifunza kutoka kwa wakosoaji wetu. Tunawashukuru sana na tunawaomba waendelee kutukosoa kila wanapoziona kasoro.

Chini hapa ni maoni ya kwanza kabisa kutumwa na mtembeleaji. Na anachoandika mtembeleaji huyu kutoka India kinaakisi dhamira niliyokuwa nayo.

Bwana huyu anasema; { fakir005 } at: Tue Sep 19, 06:32:00 PM EAT said... This looks like an African blog. Once the TV showed an African milk his cow. The cow had so stretched tits. I've never seen so much stretching. The african as really stretching further to twice the original length to get any drop of milk he could get. It was obvious the cow was dry because it was too long after the birth of her calf and needed to be inseminated again.The cow just stood there while the African worked the Tits. The picture does not show anycows. But the man in the picture and the house remind me of the TV scene in the gone years."

Maggid,
Mwenyekiti Mtendaji.
Mjengwablog.com

No comments:

Post a Comment