Monday, August 11, 2014

'HAKUNA DINI YA KWELI INAYOCHOCHEA MAUAJI'

Katibu Mkuu wa UPF, Bw. Tageldin Hamad akifurahia zawadi za majani ya chai, korosho na kahawa alizopewa leo (Agosti 11, 2014) na Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda kwenye ukumbi wa Mkutano wa Dunia kuhusu Amani na Usalama unaoendelea jijini Seoul, Korea Kusini.
 Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda  akifuatilia mada iliyowasilishwa leo asubuhi (Agosti 11, 2014)  kuhusu amani na usalama barani Afrika katika Mkutano wa Dunia kuhusu Amani na Usalama unaendelea jijini Seoul, Korea Kusini
  Balozi wa Kudumu wa AU kwenye Umoja wa Mataifa, Bw. Antonio Tete akitoa mada kuhusu amani na usalama barani Afrika leo asubuhi (Agosti 11, 2014)   katika Mkutano wa Dunia kuhusu Amani na Usalama unaendelea jijini Seoul, Korea Kusini
 Mjumbe wa Baraza la Uendeshaji la UNESCO, Dk. Mary Mbiro Khimulu akitoa mada kuhusu amani na usalama barani Afrika leo asubuhi (Agosti 11, 2014)   katika Mkutano wa Dunia kuhusu Amani na Usalama unaendelea jijini Seoul, Korea Kusini
 Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda (kulia) akibadilishana mawazo na  mke wa Rais wa zamani wa Uruguay, Bibi Mercedes Menafra de Batlle wakati akisubiri kushiriki mkutano wa Shirikisho la Wanawake na Amani Duniani  (WFWP) kwenye ukumbi wa Jumba la Makumbusho la Kimkoo, jijini Seoul, Korea Kusini leo 
  Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda (kulia) akisalimiana na Rais wa Shirikisho la Wanawake na Amani Duniani (WFWP), Prof. Yeon Ah Moon, wakati akisubiri kushiriki mkutano wa shirikisho hilo kwenye ukumbi wa Jumba la Makumbusho la Kimkoo, jijini Seoul, Korea Kusini leo mchana (Agosti 11, 2014). Katikati ni mke wa Rais wa zamani wa Uruguay, Bibi Mercedes Menafra de Batlle.
 Baadhi ya washiriki wa mkutano wa siku moja ulioandaliwa na Shirikisho la Wanawake na Amani Duniani  (WFWP), wa kwanza mstari wa mbele ni Rais wa WFWP,  Prof. Yeon Ah Moon akifuatiwa na Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Dk. Lan Young Moon kwenye ukumbi wa Jumba la Makumbusho la Kimkoo, jijini Seoul, Korea Kusini leo mchana
 Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda (wa tatu kushoto) akiwa na viongozi wakuu wakifuatilia mada kwenye mkutano wa siku moja ulioandaliwa na Shirikisho la Wanawake na Amani Duniani  (WFWP) kwenye ukumbi wa Jumba la Makumbusho la Kimkoo, jijini Seoul, Korea Kusini leo mchana (Agosti 11, 2014). Kutoka kushoto ni Balozi wa Uruguay nchini Korea, Alba Rosa Legnani, Mke wa Rais wa visiwa vya Marshall, Bibi Lieom Anono Loeak na wa kwanza kulia ni mke wa Rais wa zamani wa Uruguay, Bibi Mercedes Menafra de Batlle.
 Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda (wa pili kulia) akiwa na viongozi wa Shirikisho la Wanawake na Amani Duniani (WFWP) pamoja na wake wa Marais mara baada kumaliza mkutano wa siku moja ulioandaliwa na Shirikisho hilo kwenye ukumbi wa Jumba la Makumbusho la Kimkoo, jijini Seoul, Korea Kusini leo mchana (Agosti 11, 2014). (PICHA NA IRENE BWIRE WA OWM).

MJUMBE wa Baraza la Uendeshaji la UNESCO linalosimamia ukuzaji wa utamaduni, Dk. Mary Mbiro Khimulu amesema machafuko na mauaji hayana uhusiano wowote na dini ambayo ni ya kweli.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Agosti 11, 2014) wakati akishiriki mjadala wa jinsi ambavyo bara la Afrika linakabiliana na migogoro inayotokea barani humo kwenye mkutano wa Dunia unaojadili masuala ya Amani, Usalama na Maendeleo jijini Seoul, Korea Kusini.

Dk. Khimulu ambaye ni raia wa Kenya, alisema: "Dini ya kweli haiwezi kuruhusu umwagaji wa damu, hakuna dini ya kweli inayochochea mauaji wala kuruhusu mapigano. Ninawasihi wote mliopo hapa, msiruhusu dini zenu zitumike kufanya mambo mabaya."

Dk. Khimulu alisema ili kuepuka migogoro ya dini, anashauri diplomasia ya utamaduni (cultural diplomacy) itumike kuleta amani, usalama na maendeleo barani Afrika. "Kwa kuitumia diplomasia ya utamaduni, tuangalie ni kwa njia gani mijumuiko ya pamoja ya kidini (inter-faith communities) inaweza kutumika kuleta amani, upendo na mshikamano kwenye jamii tunazoishi," alisema.

Vilevile, Dk. Khimulu alisema kwa kutumia diplomasia ya utamaduni tunaweza kuvunja chuki na kuleta mshikamano na umoja miongoni mwa watu wetu, watu wakatembeleana kupitia michezo, nyimbo au matamasha, na wakajenga mahusiano ya kuheshimiana kidugu.

Alisema kwa kuwa vita huanzia akilini mwa mwanadamu, ni humo humo ambamo mawazo ya kuacha mapigano ama machafuko yanapaswa kuingizwa. "Kwa hiyo tuitumie diplomasia  ya utamaduni kama njia pekee ya kujenga mahusiano ya karibu kwenye jamii zetu na itusaidie kufikia malengo yetu ya kupata amani na usalama kwa watu wetu,"aliongeza.

Mapema, Balozi wa Kudumu wa AU kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Antonio Tete alisema wakati Umoja wa Afrika unaanzishwa mwaka 1963, baadhi ya wakuu wa nchi walikuwa na ndoto ya kuwa na jeshi moja barani  Afrika ambalo lingekuwa na kazi ya kukabili migogoro yote barani humo.

"Kutokana na mabadiliko ya wakati na kadri muda ulivyosonga mbele, matarajio yao hayakutumia. Viliundwa vikosi vya muda navyo havikudumu. Tumeshuhudia miaka ya 90 kwenye migogoro ya Rwanda na ya Somalia. Hakuna jeshi lilipelekwa wala hakuna askari waliokuja kutoka nje," alisema.

Alisema Umoja wa Afrika unakabiliwa na changamoto ya kukosa fedha za kujiendesha kubwa likiwa ni la kusimamia amani na usalama wa nchi wanachama. “Tunayo programu ya ulinzi na usalama lakini asilimia 90 ya mpango huu inachangiwa na wafadhili kutoka nje ya nchi. Hii siyo kazi rahisi... huwezi kujiendesha namna hii,” alisema.

Changamoto nyingine aliyoitaja ni kuwepo kwa vikund vya kigaidi. “Hawa wanaendesha mambo yao tofauti na kwa teknolojia ya hali ya juu, hata ungekuwa na jeshi la aina gani si rahisi kuwashinda... huwezi kutumia njia za kawaida za kupambana na uhalifu unapokabiliana na makundi ya aina hii,” alisema.

Katika hatua nyingine, Balozi Tete aliwaomba baadhi ya washiriki wafikirie kuwekeza barani Afrika kama njia mojawapo ya kuleta amani ya kudumu katika bara hilo. “Kwa muda mrefu bara hili limetumika kama chanzo cha malighafi kwa viwanda vya Ulaya na Amerika. Ni wakati sasa tubadili muelekeo na tufikirie kuwekeza katika bara hili kwani kwa kufanya hivyo mtasaidia kutengeneza ajira nyingi kwa vijana wa Afrika kupitia viwanda ambavyo mtavijenga.”

“Kukiwa na ajira za kutosha, mtaleta maendeleo na mtaleta amani kwa vile mtapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro na machafuko yanayotokana na kugombea rasilmali haba zilizopo,” alisema.
  
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 11, 2014





No comments:

Post a Comment